Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:- Upatikanaji wa maji safi na salama katika Mji wa Kasulu bado ni changamoto kubwa sana, kwani maji yanayotoka kwenye mabomba ni machafu. Je, ni lini Serikali itatoa pesa kwa ajili ya kununua chujio la maji ili wananchi waweze kupata maji safi na salama?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; katika Kata ya Mwilamvya ndipo yalipo machinjio ya ng’ombe, mbuzi na kondoo. Eneo hilo hupata maji mara mbili kwa wiki au mara tatu, lakini hivi sasa ninavyoongea eneo hilo halina maji na ni muda wa mwezi mzima maji hayapatikani katika eneo hilo.
Je, Serikali iko tayari kutoa pesa kwa mpango wa dharura ili eneo hilo la machinjio liweze kupatiwa maji? (Makofi)
Swali langu la pili, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu DC ipo miradi ya maji ambayo haijakamilika, imefikia asilimia 85 mpaka 95 lakini imekwama kwa ajili ya ukosefu wa pesa; je, ni lini sasa Serikali itamalizia miradi hiyo kwa kupeleka pesa ili miradi hiyo iweze kukamilika na wanawake waweze kuondolewa adha ya upatikanaji wa maji? (Makofi)

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, ni mama shupavu, jasiri, mfuatiliaji na mhangaikaji wa matatizo ya wananchi wa Kigoma hasa katika suala zima la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kwa wananchi wako wa Mwilamvya hususan katika eneo hilo la Machinjio katika kuhakikisha wanapata maji safi ili waendelee na usafi, wakati mwingine usafi ni uhai wa mwanadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu suala zima la miradi ambayo haijakamilika, nitumie nafasi hii kulishukuru Bunge lako tukufu na wewe mwenyewe kwa Wizara yetu ya Maji kuidhinishiwa fedha na katika Mji huo wa Kasulu umetengewa kiasi cha shilingi 1,466,000,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na sisi Wizara na viongozi katika kuhakikisha tunasimamia fedha zile ili ziende zikamilishe miradi ambayo haijakamilika ili wananchi wake waweze kupata maji, salama na yenye kuwatosheleza.