Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:- Kilimo cha Tanzania hutegemea mvua za msimu ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji. Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi?

Supplementary Question 1

MHE. MWATUM DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri aliyoyatoa yenye kila aina ya vinjonjo. Napenda kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa programu hizi katika sekta ya kilimo linahusiana na suala la kuhimili mabadiliko ya tabianchi; je, Serikali ina mkakati gani kutoa elimu kwa wakulima ili waende sambamba na mabadiliko ya tabianchi? (Makofi)

Name

Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Mwatum ambaye amekuwa akifuatilia sana masuala ya mazingira na hasa mambo haya ya mabadiliko ya tabianchi. Namhakikishia kwamba pamoja na mipango hii ambayo Serikali tumekuwa tukiifanya, hata kule Unguja na Pemba tunashirikiana na Taasisi za Kimataifa USAID pamoja na FAO katika miradi ya kilimo ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kutoa elimu, nimhakikishie Mheshimiwa Mwantum tayari mpaka sasa Serikali ilishatoa mwongozo pamoja na mafunzo kwa watu wapatao 192 wakiwemo Maafisa Kilimo, Maafisa Uvuvi, Maafisa Mifugo pamoja na Maafisa Mipango kutoka kwenye Halmashauri za Wilaya na kuwaelekeza kwamba katika mipango wanayoipanga Wilayani pamoja na bajeti waweze kushirikisha mipango hiyo ya kilimo himilivu cha mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, elimu hii tayari tulishaipeleka kwa wananchi na bado tunaendelea katika mpango huu tuliosema endelevu wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi, ni element ambayo pia inahusishwa. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais alizindua juzi hapa ASDP II, vilevile kuna element ya kutoa mafunzo ya kilimo himilivu kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Name

Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Primary Question

MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:- Kilimo cha Tanzania hutegemea mvua za msimu ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji. Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi?

Supplementary Question 2

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapema mwaka 2017 niliwasilisha andiko la mradi ujulikanao kama Commitment Bush Fire Management and Livehood Improvement kwa lengo la kudhibiti uchomaji moto ovyo. Ni lini Wizara yenye dhamana itaweza kuwezesha mradi huu kwa kutoa fedha ili tuweze kutekeleza kikamilifu kwa kuanzisha zao ambalo ni rafiki na mazingira lakini pia na ufugaji wa nyuki? (Makofi)

Name

Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Answer

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, mapema katika Mkutano uliopita Mheshimiwa Gashaza aliuliza swali la nyongeza kuhusiana na mradi wake huu.
Napenda nimhakikishie kwamba sasa hivi Ofisi ya Makamu wa Rais inaandaa maandiko mbalimbali kwa ajili ya kuomba fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunahamasisha Halmashauri za Wilaya waweze kuandika maandiko ambayo watayaleta Ofisi ya Makamu wa Rais ili tuweze kuwatafutia fedha katika kutekeleza miradi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Gashaza, andiko lake tumelipitia ni muhimu sana. Pia aliweza kuwahusisha wananchi wa Jimboni kwake kupitia michezo wakiwa na kauli mbiu ya kwamba mazingira ni uchumi ili waweze kucheza ligi ile na kauli mbiu hiyo waweze kuhakikisha kwamba wanajihusisha na ufugaji wa nyuki pamoja na kilimo ili wasiendelee kuchoma misitu ambayo inaendeleza uharibu wa mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Gashaza kwamba hata hiyo ligi yake, baada ya kupata fedha mimi mwenyewe nitaenda kumsaidia kuizindua ili iwe kichocheo kwa nchi nzima ili wananchi wengine nao wafanye hivyo. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Primary Question

MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:- Kilimo cha Tanzania hutegemea mvua za msimu ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji. Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi?

Supplementary Question 3

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nasikitika kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri hajajibu hili swali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuathirika kwa kilimo ni matokeo ya athari za tabianchi. Tuambie Serikali ina mikakati gani ya kukabiliana na athari hizi? Maziwa yanakauka, mito inakauka, misitu inapotea. Mna mkakati gani mliouchukua au ndiyo mko kwenye mipango tu? Ndiyo jibu tunalolitaka kutoka kwako. Nakushukuru.

Name

January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ambalo Mheshimiwa Mwantum Dau Haji alitaka kujua Serikali tuna mipango na mikakati gani; nimeeleza kwamba mkakati wa kwanza tulionao tuliuandaa mwaka 2007 ambao unahusu uhimilivu katika mabadiliko ya tabianchi kwenye suala la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimejibu hapa kwamba mwaka 2012 tuliandaa mpango mwingine wa mabadiliko ya tabianchi tofauti na ule wa mwanzo. Vilevile nimejibu hapa kwamba mpaka sasa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na kupitia wataalam tunaandaa na tunakaribia kumaliza kupata sasa mpango mkakati endelevu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwenye suala la kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo kwamba mikakati haipo, nimeieleza hapa. Pia nimeelezea hapa kwamba hata juzi Mheshimiwa Rais amezindua ASDP Awamu ya Pili ambamo ndani mwake pia kuna mikakati mingi sana imezungumziwa. Pia mikakati na mwongozo niliousema ambao tumepeleka kwenye Halmashauri ambapo Maafisa Mipango wanatakiwa kuweka kwenye bajeti zao, tumeelezea kuhusu utafiti wa mbegu ambayo inahimili kwenye ukame pamoja na kilimo cha umwagiliaji na umwagiliaji wa matone.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mikakati hii ipo, Mheshimiwa Yussuf mtani wangu wa kisiasa, naomba uelewe Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni Serikali makini, ni Serikali ambayo inaongoza kwa kuwa na mikakati, tena mikakati ambayo inatekelezeka. Ahsante sana.

Name

Dr. Immaculate Sware Semesi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:- Kilimo cha Tanzania hutegemea mvua za msimu ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji. Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi?

Supplementary Question 4

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikipokea fedha mbalimbali kutoka kwa wafadhili ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kila mwaka. Miaka miwili iliyopita walikabidhiwa takribani shilingi bilioni 224 kwa ajili ya shughuli hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri anaongelea kuhusu mikakati; je, kuna utekelezeji wowote wa mikakati hii ya kuhusisha mabadiliko ya tabianchi na kuboresha kilimo chetu kwa kutumia hizi fedha za wafadhili ambazo zinagusa hususan mabadiliko ya tabianchi? Ahsante. (Makofi)

Name

January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Sware ni mwanamazingira na ni kweli anafahamu kabisa kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais tumekuwa tukipata fedha ambazo zinasaidia miradi mbalimbali ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Amesema sasa mbali na mikakati, fedha hizi namna gani tunazi-link.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie kwamba mojawapo ya miradi ambayo tumeihusianisha na hiki kilimo kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ukienda kule Rufiji tayari katika Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji tulikuwa tunatekeleza mradi ukiwa ni pamoja na kupanda mikoko na kuwawezesha wananchi wahimili mabadiliko ya tabianchi kwa kilimo cha mboga pamoja na matunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, ukienda kule Pemba Kisiwa Panza mbali na kujenga ukuta, vilevile tulikuwa tunawasaidia wananchi waweze kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kilimo cha mboga na matunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo sasa hivi tuna Mikoa kama Tabora, Singida, Kagera, Morogoro, Tanga ambako tayari tunatekeleza miradi mbalimbali ya kutumia fedha hizi ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wakulima wa namna wanavyoweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanatumia zile fedha katika kilimo cha mboga pamoja na matunda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni pamoja pia na Bonde la Kihansi kule Kilombero, vilevile tumeweza kutoa fedha ili wananchi wahimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kilimo katika lile mbonde.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Sware kwamba siyo mikakati tu ambayo Serikali inaishia, ni pamoja na fedha hizi. Tumetoa fedha nyingine shilingi milioni 200 sasa ambazo zinapeleka maji kule Shinyanga na yale maji yatatumika pia katika kusaidia umwagiliaji kwenye kilimo. Hiyo ni katika kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Ahsante sana. (Makofi)