Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Primary Question

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Mpemba hadi Ileje kwa kiwango cha lami ili kuunganisha na kuboresha mpaka wa Malawi na Tanzania katika eneo la Isongole?

Supplementary Question 1

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri yanayotoa faraja kwa wananchi wa Tunduma pamoja na Ileje, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wananchi wa Kata ya Bupigu, Kata ya Malangali, Kata ya Isoko na Kata ya Ikinga katika Wilaya ya Ileje wamekuwa na adha kubwa sana ya kuamka Saa nane ya usiku na kusubiri usafiri kuja makao makuu ya Mkoa wa Songwe. Ni lini Serikali itajenga barabara hii ya kutoka Isongole mpaka Ikinga, ili kuondoa adha hii ya Wananchi wa Ileje?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna kipande cha barabara kilometa 1.6 kimejengwa katika Mji wa Tunduma na kimejengwa kwa sababu, wananchi wa Mji wa Tunduma wakati Mheshimiwa Rais akiwa Waziri wa Ujenzi, wakati anapita anakwenda Rukwa, walimsimamisha pale na wakamwomba barabara ile ijengwe haraka iwezekanavyo na sasa Serikali imejenga kipande kile cha kilometa 1.6, lakini kipande kile kimejengwa chini ya kiwango. Je, ni lini Serikali itakuja kuhakiki kipande kile cha barabara ili wananchi wa Tunduma waweze kufurahia mpango wa ujenzi wa barabara kwenye Mji wa Tunduma?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kama anavyouliza, anapenda kujua katika swali lake la kwanza, katika hizi Kata za Lupingu, Malangali na Ikinga, kuna sehemu ambayo ina uharibifu mkubwa, kwamba, kwa kweli, maeneo mengi tumekuwa na uharibifu kutokana na mvua zimekuwa nyingi, lakini kama tulivyopitishiwa bajeti na Bunge lako, tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya matengenezo, ili kuhakikisha kwamba, maeneo haya yanapitika.
Mheshimiwa Spika, kabla hatujapata kipande cha lami katika eneo hili nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Tunduma kwa ujumla kwamba wakati hizi mvua zinapungua tumejipanga kwa ajili ya kufanya marekebisho makubwa ili maeneo haya yapitike. Kwa hiyo, nimtoe tu wasiwasi kwamba tutafanya marekebisho ili wananchi waendelee kupata huduma ili waondokane na hii adha ambayo wanaipata.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kuhusu kile kipande cha kilomita 1.6 ambacho Mheshimiwa Mbunge anaona kwamba hakikujengwa katika standard inayotakiwa; niseme tu kwa sababu nitakuwa na ziara ya maeneo yale kwamba tutayaona kwa pamoja ili tuone kwamba hii kilomita 1.6 ina shida gani ili tuone kama kweli ni kiwango hakikuwa kimefikiwa au labda saa nyingine ndiyo ilikuwa kuna shida tofauti ya hapo kwa sababu kuna wakati mwingine barabara zinajengwa lakini mazingira ambayo hayakutegemewa yanaweza yakatokea barabara ikaharibika.
Mheshimiwa Spika, tutaiona kwa pamoja na Mheshimiwa Mbunge halafu tuone tutachukua hatua kama kutakuwa na shida yoyote kuhusu kipande hiki ambacho umekitaja.