Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LUCIA M. MLOWE aliuliza:- Wapo Watumishi katika sekta ya afya, hususan Madaktari na Wauguzi ambao waliajiriwa katika miaka ya 1980 kupitia Serikali Kuu, lakini wakati ule hapakuwa na makato ya mfuko wa kijamii na kuanzia mwaka 1999, Serikali ilianza kuwakata mishahara yao kwenye Mfuko wa PSPF:- Je, Serikali inawafikiriaje Watumishi hao ambao fedha zao hazikukatwa na mifuko ya kijamii wakati huo hususan Mfuko wa PSPF?

Supplementary Question 1

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwenye jibu lake la msingi kwamba watumishi wanapaswa kulipwa mafao yao hata kama hawakuwa wanakatwa, lakini hilo halifanyiki. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba hawa watumishi wanapata mafao yao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa watumishi wastaafu wanapata pensheni yao ndogo sana, kuna watumishi wanapata Sh.50,000 kwa mwezi, kwa kweli kiasi hicho ni kidogo sana. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inaongeza kiasi hicho cha pensheni? (Makofi)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba hili jambo analosema halifanyiki, siyo sahihi. Kwa sababu watumishi wote ambao waliajiriwa na walikuwa hawachangii kabla ya Mfuko wa Pensheni wa PSPF kuanzishwa walikuwa wakilipwa na Serikali Kuu kupitia Hazina. Kwa sasa kile kilichokuwa kinalipwa kupitia Hazina ndicho kimeunganishwa na malipo yao ya PSPF na wanalipwa pensheni yao yote kama ambavyo wanastahili kulipwa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, sina uhakika sana labda nikae na Mheshimiwa Mbunge ni wastaafu gani wanaolipwa pensheni ya Sh.50,000, kwa sababu Serikali iliongeza pensheni ambayo ni kiwango cha chini kutoka Sh.50,000 kwenda Sh.100,000 na Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii inalipa Sh.100,000 kwa watumishi wote kama kiwango cha chini. (Makofi)

Name

Joseph Osmund Mbilinyi

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbeya Mjini

Primary Question

MHE. LUCIA M. MLOWE aliuliza:- Wapo Watumishi katika sekta ya afya, hususan Madaktari na Wauguzi ambao waliajiriwa katika miaka ya 1980 kupitia Serikali Kuu, lakini wakati ule hapakuwa na makato ya mfuko wa kijamii na kuanzia mwaka 1999, Serikali ilianza kuwakata mishahara yao kwenye Mfuko wa PSPF:- Je, Serikali inawafikiriaje Watumishi hao ambao fedha zao hazikukatwa na mifuko ya kijamii wakati huo hususan Mfuko wa PSPF?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ukiacha waaguzi lakini pia wafanyakazi wengi wa Idara zingine Serikalini wanacheleweshewa sana mafao. Mfano ni Askari Magereza wanastaafu lakini wanakaa zaidi ya miaka miwili hawajaenda kwao. Wanaganda kwenye zile kota za Magereza lane, mafao hamna, mtu kastaafu miaka miwili anadhalilika kwao Tanga, kwao Kilimanjaro, kwao wapi, hawezi kwenda kwa sababu hajapewa mafao yao wala pensheni.
Mheshimiwa Spika, sasa hii Serikali inawaangalia kwa jicho lipi hawa Askari Magereza kwa sababu, wao wamezoea kuwa-support Polisi ambao wanatukamata, lakini wahalifu wako maeneo mbalimbali, wanakusanywa yale maeneo mbalimbali, wanapelekwa eneo moja ambalo ni Magereza. Wale jamaa wana kazi ngumu sana kuwatunza mle, lakini wanafanya utumishi wao, wanakuja wanastaafu, mtu anakaa Police Lane miaka miwili hajapewa pension wala mafao yake, kwa nini wanawafanyia hivi Askari Magereza? (Makofi/Kicheko)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ameuliza, kuhusu mkakati wa Serikali yetu, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbilinyi, mkakati wa kwanza wa Serikali yetu ilikuwa ni kulipa madeni yote ya michango ya mwajiri ambayo Serikali ilikuwa ikidaiwa na mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba, mpaka leo ninapoongea madeni yote yaliyokuwa yanadaiwa ya michango Serikali yetu ya Awamu ya Tano tayari imeshalipa zaidi ya shilingi bilioni 282 ili kuhakikisha wastaafu wetu wanalipwa mafao yao kwa muda muafaka.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa pili, ilikuwa ni kuona jinsi gani ya kuunganisha Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii, ili pesa zilizopo ziweze kutumika inavyotakiwa na kuwanufaisha wastaafu wetu pale wanapostaafu. Namwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Julai Mosi, mifuko yote imeshaunganishwa na sasa tuna mifuko miwili, tatizo hili litaondoka bila wasiwasi wowote.