Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Primary Question

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya kujenga uwanja wa ndege mbadala katika Mji wa Tunduru baada ya uwanja uliokuwepo awali kuhamishwa kutoka katikati ya mji?

Supplementary Question 1

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa majibu yake mazuri na yenye kuleta matumaini. Pia niipongeze Serikali bila hata kumung’unya maneno kwa namna ambayo kutokana na ujenzi wa barabara ya lami iliyounganisha Wilaya ya Tunduru na wilaya zingine na kuufanya Mkoa wa Ruvuma vilevile uweze kuungana na mikoa mingine kwa barabara ya lami. Wananchi wa Wilaya ya Tunduru kwa ujumla wanaipongeza na kuishukuru sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kuwa miundombinu ya usafirishaji inafanya kazi kwa kutegemeana, kusaidiana na kwa kushirikiana; baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara tumepanua fursa na kuweka mazingira ya kiuchumi na kijamii kuwa bora zaidi kwa maana ya kuvutia wawekezaji, lakini pia kuwahamasisha wananchi katika eneo hili. Sasa Uwanja wa Ndege wa Tunduru unauona umuhimu wake sasa zaidi kuliko hata ilivyokuwa hapo kabla. Je, Serikali itaingiza lini kwenye mipango ya ujenzi wa viwanja vya ndege, Uwanja wa Tunduru ukawa ni mmojawapo? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, lakini kwa kuwa Serikali pia imekiri kwamba uwanja uliopo haujafungwa rasmi na unaweza ukaendelea kutumika na sisi tunahitaji utumike kwa kuwa mahitaji ni makubwa, wawekezaji wanashindwa kusafiri umbali mrefu sana kwa kutumia njia ya usafiri wa barabara. Je, uboreshaji wa kiwanja kilichopo ambacho kwa sasa hivi hali yake ni mbaya hakiwezi kutumika utafanyika lini kwa maana ya kwamba si uzio tu peke yake, runway na taxiway zinatakiwa kufanyiwa marekebisho lakini pia hata kibanda kwa ajili ya kupokea na kuruhusu abiria kuondoka?

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Engineer Ramo Makani kwa jinsi ambavyo mara nyingi sana anafuatilia masuala mbalimbali yanayohusu ujenzi, uchukuzi na mawasiliano kwa Jimbo lake la Tunduru Kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna mradi wa ujenzi wa uwanja mpya kwa eneo ambalo tumeoneshwa na watu wa Halmashauri ya Mji wa Tunduru, lakini bado kuna masuala ya fidia ndogo ndogo kwa wananchi. TAA ambao ni Wakala wa Viwanja vya Ndege wanaendelea kufanya tathmini ya malipo kwa wananchi ambao wanadai fidia zao kwa maeneo ambayo tutayachukua kwenye huu uwanja mpya ambao tunategemea kuujenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nimhakikishie Mheshimiwa Ramo Makani kwamba taratibu za ulipaji wa fidia kwa wananchi hao zitakapokamilika tutahitaji sasa tupate hati ya kumiliki uwanja huo kabla ya kuanza mradi wa ujenzi wa uwanja huo. Taratibu nyingine zote zitafuata baada ya kupata taratibu muhimu kutoka Halmashauri ya Mji wa Tunduru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anauliza lini uboreshaji wa uwanja utaanza. Nimhakikishie Mheshimiwa Ramo Makani kwamba tayari timu ya wataalam kutoka TAA imekwishatembelea pale kama nilivyoeleza kwenye swali la msingi tangu mwaka jana mwezi wa Nne na wameshaona eneo la uwanja huo. Mahitaji muhimu kwa ajili ya kuboresha uwanja huo yameshaainishwa sasa hivi tupo kwenye taratibu za manunuzi kwa ajili ya kwenda kuuboresha uwanja huo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)