Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Primary Question

MHE. JOHN J. MNYIKA (K.n.y. MHE. JOHN W. HECHE) aliuliza:- Wilaya ya Tarime ni miongoni mwa Wilaya zinazoongoza kwa wakazi wake kuwa na kesi za kubambikiwa hasa za wizi wa kutumia silaha na mauaji, kitendo kinachokuwa na sura ya kumpa mtuhumiwa wakati mgumu sana kupata msaada wa kisheria. Je, ni kwa nini Serikali isisaidie upatikanaji wa msaada wa kisheria kwa mahabusu hao ambao kitakwimu ni wengi katika Gereza la Tarime kuliko mashauri mengine yoyote?

Supplementary Question 1

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kwamba sheria imetungwa tangu mwaka 2007 lakini mpaka sasa Serikali haijaanza kutoa msaada wa kisheria.
Sasa kwa kuwa mazingira ya Tarime ni maalum; kuna Mgodi wa North Mara pale Nyamongo na wananchi wengi wanabambikiziwa kesi za unyang’anyi na mauaji kutokana na mgogoro na mgodi; kuna mbuga ya Serengeti pale na wananchi wanabambikiziwa kesi za mauagi na unyang’anyi kutokana na mgogoro na mbuga, je, Serikali iko tayari kuagiza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakati huo mwongozo ukisubiriwa iende Gereza la Tarime ili ufumbuzi wa haraka uweze kupatikana?
Mheshimiwa Mwenyekitil, swali la pili, nilikuwa mahabusu ya Segerea na matatizo haya ya ubambikiziwaji wa kesi yapo Tarime lakini yapo Segerea na mahabusu nyingine. Sasa kwa kuwa hali hii imekithiri magereza mengi sana, ili hali hii ya kubambikiza kesi iweze kukoma Serikali ni lini itaanza kutoa fidia kwa wananchi waliobambikiziwa kesi ili utamaduni huu wa kubabikiwa kesi ukome? (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, kwanza nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge si kweli kwamba Sheria hii ya Huduma za Kisheria imetungwa mwaka 2007.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria hii ni ya mwaka 2017, imepitishwa mwaka jana ni Sheria Namba Moja ya mwaka 2017, kwa hiyo na hivi sasa ndiyo imeanza utekelezaji wake. Hoja iliyoletwa hapa kwamba kuiomba Tume ya Haki za Binadamu kwenda katika eneo la Tarime kwa ajili ya kwenda kushughulika na hawa ambao wamebambikiziwa kesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliopo ni huu kwamba huduma za msaada wa kisheria hizi zinatolewa na organization mbalimbali ambazo zimesajiliwa kwa mujibu wa sheria hii. Mpaka sasa ninavyozungumza tayari tunazo 66 ambazo zinafanya kazi hii. Kinachosubiriwa hapa ni muongozo kati ya Polisi na Wizara ya namna bora ya kuweza kutoa huduma ya kisheria kwa mahabusu walipo vituoni kwa mujibu wa kifungu cha 36(1) cha sheria, lakini si kweli kwamba watu hawapati huduma za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika historia ya nchi yetu mpaka ninavyozungumza hivi sasa ni kazi kubwa sana imefanyika katika eneo hili. Kwa sababu huduma hii ya kisheria imeanza mwaka 1969 ikianzia katika Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini baadae ikatungwa sheria Namba 21 ya mwaka 1969, lakini baadae mwaka 1984 kwenye Katiba yetu tukaingiza Bill of Human Rights ikawa enshrined na baadae ikatungwa sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ukiangalia Serikali imekuwa ikifanya kazi hii kwa kiwango kikubwa sana, na mpaka hivi sasa ninavyozungumza tayari wananchi wameweza kupata huduma za kisheria kupitia hizo organizations.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ameuliza kuhusu watu wanaobambikiziwa kesi na namna ambavyo Serikali inaweza kuwalipa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kimahakama uko wazi na unajieleza vizuri kabisa. Inapotokea mtu yeyote ameshitakiwa mahakamani na baadae ikagundulika kwamba amebambikiziwa kesi utaratibu wa kisheria upo wa kumtaka yeye kufungua kesi ya madai, lakini Serikali hailipi suo moto moja kwa moja. Kwa hiyo wale wote wanahisi wamebambikiziwa kesi utaratibu upo na wafuate sheria.

Name

Rev. Peter Simon Msigwa

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Iringa Mjini

Primary Question

MHE. JOHN J. MNYIKA (K.n.y. MHE. JOHN W. HECHE) aliuliza:- Wilaya ya Tarime ni miongoni mwa Wilaya zinazoongoza kwa wakazi wake kuwa na kesi za kubambikiwa hasa za wizi wa kutumia silaha na mauaji, kitendo kinachokuwa na sura ya kumpa mtuhumiwa wakati mgumu sana kupata msaada wa kisheria. Je, ni kwa nini Serikali isisaidie upatikanaji wa msaada wa kisheria kwa mahabusu hao ambao kitakwimu ni wengi katika Gereza la Tarime kuliko mashauri mengine yoyote?

Supplementary Question 2

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tabia hii ya polisi kutumia vibaya madaraka na kubambika kesi imekithiri sana katika nchi yetu. Mimi mwenyewe ni muathirika wa kubambikiwa kesi. Mfano mzuri ni RCO (Afisa Upelelezi) wa Mkoa wa Iringa ambaye amekuwa akibambikiza kesi na kuwalazimisha hasa wanachama wa CHADEMA wahame chama cha CHADEMA waingie Chama cha Mapinduzi ili wasifunguliwe mashtaka.
Je, Serikali itakuwa tayari kufanya uchunguzi kwa RCO huyu ambaye anatumitumia madaraka yake vibaya mfano mzuri ni mimi mwenyewe nimebambikiziwa kesi nimekuwa muathirika? (Makofi)

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Msigwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, madai hayo Mheshimiwa Msigwa amekuwa akiyatoa mara kwa mara Bungeni na binafsi nimeshamuomba mara kadhaa kama ana vithibitisho wa tukio lolote la aina hii alilete lakini mpaka leo hajaleta.
Kwa hiyo, narudia tena maelezo ambayo Mheshimiwa Msigwa nimekuwa nikikupa mara nyingi wakati mwingine nje hata ya Bunge kwamba kama una uthibitisho wa jambo kama hilo lilete tulifanyie kazi.
Kwa taarifa zilizopo mpaka sasa hivi hakuna askari polisi ambaye amemzungumza ambaye amefanya matukio kama hayo kinyume na utaratibu wa sheria.