Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Primary Question

MHE. ENG. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaunga mkono wananchi wa Kata ya Haneti kwa kumalizia ujenzi wa chumba cha upasuaji ambacho kilianzishwa kwa nguvu za wananchi na Mfuko wa Jimbo?

Supplementary Question 1

MHE. ENG. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri yanayotia matumaini kwa wananchi wa Kata zote tano za Tarafa ya Itiso ambayo wanapata huduma pale pamoja na Wilaya ya jirani ya Chemba ambayo pia wanapata huduma katika Kituo cha Afya cha Haneti. Hata hivyo pamoja na majibu hayo mazuri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kituo hiki na chumba hiki kiweze kufanya kazi vizuri kunahitajika kuwe na vifaa tiba vinavyohudumia mle ndani. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba jengo linapoisha basi na vifaa tiba viweze kupatikana ili wananchi waweze kupata huduma?
Mheshimiwa Mwenyekitil, pili wataalam husika ni wachache sana. Hata katika Kituo cha Afya cha Haneti madaktari na wataalam wengine ni wachache. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha kwamba kituo na jengo hili litakapoikwisha la upasuaji wataalam pia wanakuwa wanapatikana wa kutosha wa kuweza kuwahudumia wananchi?

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya swali la kwanza uwepo wa vifaa vya upasuaji na vifaa vingine pale ambapo Kituo cha Afya cha Haneti kitakuwa kimekamilika ili viweze kuanza kufanya kazi, naomba nimhakikishie, kwanza, katika Kituo cha Afya cha Haneti tayari vifaa vya upasuaji vimeshanunuliwa vipo tayari. Kwa hiyo tunasubiri tu kikishakamilika na vifaa vingine vitaongezwa ili kianze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anauliza kutaka kupata uhakika pale ambapo vituo vya afya vinakamilika wataalam/watumishi wawepo wa kutosha. Ni azma ya Serikali maana itakuwa hakuna sababu ya kumalizia majengo yakawa mazuri halafu tukakosa watu wakuweza kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba pale vituo vinavyokamilika na watumishi watapelekwa. Ndiyo maana hivi karibuni kuna nafasi ambazo zilishatangazwa kwa ajili ya watu wa afya waweze kuomba na waweze kuajiriwa.

Name

Omary Ahmad Badwel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Primary Question

MHE. ENG. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaunga mkono wananchi wa Kata ya Haneti kwa kumalizia ujenzi wa chumba cha upasuaji ambacho kilianzishwa kwa nguvu za wananchi na Mfuko wa Jimbo?

Supplementary Question 2

MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa kunipa nafasi na mimi ya kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maelekezo ya Serikali sasa ni kujenga zahanati katika kila kijiji na bahati nzuri wananchi katika maeneo mbalimbali wameitikia ujenzi wa zahanati hizo na wako katika hatua mbalimbali. Hata hivyo kwa bahati mbaya sana zaidi ya miaka minne, mitano baadhi ya vijiji wamejenga hizo zahanati na wamefika hatua mbalimbali hakuna fedha ya Serikali ambayo imekwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kama alivyosema Mheshimiwa Waziri Serikali ilitoa maelekezo kwa Wakurugenzi kupitia upya bajeti ya fedha za CBG ili kupata miradi michache ambayo itakuwa na matokeo ya haraka na baadhi ya sehemu hizo katika Wilaya ya Bahi kwa mfano Kijiji cha Chonde tumezitengea fedha hizo lakini mpaka sasa fedha hizo hazijaja na mwaka unakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inawaambia nini Watanzania na Bunge hili kwamba ni lini sasa fedha hizi za CBG ambazo zimefanyiwa marekebisho zitakuja kwenye Halmashauri zetu na kuweza kufanya kazi ambayo imekusudiwa?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwanza niwapongeze Wabunge wengi wametumia mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kusaidia kwa kuungana na wananchi katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, hii ni pongezi kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tunafahamu kwamba ni kweli, tulikuwa na kikao maalum ambacho kilihusisha Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Mipango, watu wa manunuzi especially na baadhi ya Wenyeviti wa Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikiri wazi kwamba takribani wiki mbili zilizopita niliwasiliana na wenzangu, nilikuwa na kikao cha watu watatu, mimi hapa, Mheshimiwa Jenista Mhagama na Waziri wa Fedha kuhusu upatikanaji wa hizo fedha kwa ajili ya kwenda kumalizia hiyo miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo imani yangu kubwa ni kwamba kabla hatujafunga mwaka huu; kwa sababu pesa zile tunaenda kujenga kwa kutumia force account jambo hili litakamilika vizuri. Lengo kubwa miundombinu hii twende tukalimalize katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. (Makofi)