Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amina Saleh Athuman Mollel

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:- Mfuko wa Watu wenye Ulemavu ulianzishwa kwa Sheria Na.9 ya mwaka 2010 na lengo la mfuko huo ni kusaidia Baraza la Watu Wenye Ulemavu kufanya kazi zake kwa ufanisi, kuendesha tafiti mbalimbali na kubaini changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu. Hata hivyo mfuko huo haukutengewa fedha katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya mfuko huo ili uweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa?

Supplementary Question 1

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nashukuru kwa majibu kutoka kwa pacha wangu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Watu Wenye Ulemavu ni haki na ni wajibu kwa sababu liko katika makubaliano ya utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2006, ambao ni matokeo ya Sheria Namba 9 ya mwaka 2010. Hata hivyo tangu Baraza lilivyoteuliwa tayari limeshamaliza muda wake, lakini mpaka hivi sasa bado Serikali kupitia Waziri mwenye dhamana hawajateua tena na kulitangaza Baraza ili liweze kushughulikia changamoto na tafiti mbalimbali kwa ajili ya kuweza kuisaidia na kuishauri Serikali, katika suala zima la watu wenye ulemavu.
Ningependa kufahamu ni lini sasa Serikali itaunda hilo Baraza na kulitangaza ili liweze kufanya kazi zake na liweze pia kuishauri Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa maswala ya watu wenye ulemavu sasa tayari yapo kwenye Wizara hii husika katika Ofisi ya Waziri Mkuu na katika vyama hivi vya watu wenye ulemavu na kutokuwepo kwa hilo Baraza, imekuwa ni changamoto pia kwamba Serikali, haivisaidii kwa kiasi kikubwa hivi vyama; kwa mfano, Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo mpaka sasa hakina viongozi na matokeo yake ni kwamba mambo hayaendi kama yalivyo sawa, wameunda Kamati.
Sasa je, ni lini wataona umuhimu wa kuvisaidia hivi vyama kuvipa ruzuku kama ilivyokuwa hapo awali viweze kufanya mambo yao katika utaratibu unaotakiwa? Ahsante.

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Amina Mollel kwa jinsi anavyofuatilia masuala ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maswali yake mawili nikianza na hili la kwanza, nikiri wazi kwamba kweli muda wa wajumbe wa Baraza la Ushauri umekwisha na sisi kama Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ofisi yenye dhamana na masuala ya watu wenye ulemavu tayari tulishaviandikia vyama mbalimbali vyote. Kwa maana ya kwamba sisi kama Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu hatuwateui wale wajumbe kutoka hewani, lazima tushirikishe vyama husika na wadau mbalimbali. Kwa hiyo sasa hivi hatua iliyopo, ni kwamba tayari barua tulishasambaza kwa vyama, na vyama tayari vimesha-respond kwa kutuletea majina mbalimbali. Sasa hivi kinachoendelea ni mchakato wa ndani wa ofisi yetu kuhakikisha kwamba sasa tunateuwa watu ambao wateweza kweli kusaidia watu wenye ulemavu, kwa masuala yanayowahusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia swali lingine ameuliza suala la ruzuku. Nipende kumthibitishia kwamba Serikali yetu ina nia ya dhati kabisa, katika kuhakikishwa kwamba masuala ya watu wenye ulemavu yanatekelezeka vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na suala hili la ruzuku, tukiangalia huu Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu, ambao sasa katika jibu langu la msingi nimeshaliongelea kwamba tuko katika hatua nzuri, kwamba tumekwisha kutenga fedha kwa ajili ya uanzishwaji wa huu mfuko. Miongoni mwa kazi za huu mfuko ni pamoja na kuhakikisha kwamba hivi vyama ikiwemo pamoja na ruzuku za vyama zinatekelezeka vizuri. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hizi ruzuku zitaendelea kutolewa kwa vyama pindi huu mfuko utakapokaa vizuri, na pindi ambapo zoezi zima la uteuzi wa wajumbe utakapokamilika.

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:- Mfuko wa Watu wenye Ulemavu ulianzishwa kwa Sheria Na.9 ya mwaka 2010 na lengo la mfuko huo ni kusaidia Baraza la Watu Wenye Ulemavu kufanya kazi zake kwa ufanisi, kuendesha tafiti mbalimbali na kubaini changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu. Hata hivyo mfuko huo haukutengewa fedha katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya mfuko huo ili uweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi na naomba uniruhusu nimpongeze Naibu Waziri Mheshimiwa Stella Ikupa. Tangu amechaguliwa, amekuwa ni faraja na sauti yenye matumaini kwa walemavu wenzake na bidii yake ya kazi hapa Bungeni sote tunaiona. Kwa hiyo, namwombea Mwenyezi Mungu aendelee hivyo hivyo kwa sababu hata sisi walemavu watarajiwa tunawiwa kwake. (Makofi)
Sasa swali langu, katika jimbo langu kuna Chama cha Walemavu na kilikuwa kinapata ufadhili kutoka kwa mama mmoja Elizabeth kutoka Sweden. Chama hiki kiliingia kwenye mgogoro wa uongozi na kusababisha yule mfadhili akarudi nyuma, na baadhi ya walemavu pia wakarudi nyuma, kwa sababu ya kugombea baadhi ya vitu ambavyo walikuwa wanafadhiliwa.
Sasa nataka nimwombe Mheshimiwa Naibu Waziri, je, uko tayari utakapopata nafasi kuja Rombo ili tusaidiane kutatua ule mgogoro na kuwaweka wale walemavu vizuri katika chama chao. Ili wale wafadhili waweze kurejea na kuwasaidia?

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo ameeleza kwamba anashughulikia masuala ya watu wenye ulemavu kwenye jimbo lake. Nimhakikishie kwamba baada ya Bunge hili nitaendelea na ziara, na miongoni mwa ziara ambazo nitafanya kama alivyoniambia au kama alivyoniomba, nitafika kwenye jimbo lake kwa ajili ya suala ambalo amelieleza mbele yako. Ahsante. (Makofi)