Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Primary Question

MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:- Jeshi la Polisi kupitia IGP Ernest Mangu ambaye alifanya ziara Wilayani Kahama mapema mwezi Agosti, 2016 alitangaza kuanzisha Mkoa mpya wa Kipolisi wa Kahama na Wilaya za Kipolisi za Msalala, Ushetu na Kahama; na wilaya hizo mpya za kipolisi zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa askari na vitendea kazi vyao hasa vyombo vya usafiri:- i. Je, ni watumishi wangapi wamepangwa Wilaya mpya ya Kipolisi ya Msalala? ii. Je, Serikali iko tayari kusaidia vyombo vya usafiri hasa magari na pikipiki Wilaya ya Kipolisi ya Msalala? iii. Je, Serikali imejipangaje kujenga ofisi za polisi wilaya na nyumba za makazi kwa askari katika Wilaya za Msalala, Ushetu na Kahama Mjini?

Supplementary Question 1

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na hasa hili la kukubali ombi la kutuletea angalau gari moja kwa ajili ya kusaidia shughuli za polisi. Pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kutambua kwamba Jeshi la Polisi lina idadi ndogo sana ya askari, wananchi wa Msalala pamoja na kanda nzima ya ziwa walishaanzisha utaratibu wa ulinzi wa jadi (Sungusungu) ambao ni askari wa kujitolea na husaidia sana shughuli za polisi kukabili matukio pale ambapo polisi wanakuwa hawajafika. Kwa bahati mbaya sana Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi limekuwa likitoa ushirikiano mdogo sana kwa watu hawa ambao wanafanya kazi kwa kujitolea na mara nyingi wamekuwa wakiwa-harass pale tukio linapotokea badala ya kuwatafuta wahalifu wanakwenda kukamata wale viongozi wa Sungusungu na kuwalazimisha au kuwataka kwamba wasaidie kutaja au kutoa taarifa ambazo zingeweza kusaidia Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua Serikali au Wizara inachukua au ina mkakati gani wa kushirikiana na Jeshi la Sungusungu ili kusaidia jitihada ambazo tayari zipo kwa sababu pia askari wenyewe wa polisi si wengi kama ambavyo jibu limejitokeza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwepo na matukio mengi ya askari polisi kubambikizia wananchi kesi mbalimbali jambo ambalo limekuwa likiwavunja moyo sana wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi, jambo hili limekuwa likijitokeza kwenye vituo mbalimbali hasa vilivyoko Kata ya Isaka , Kata ya Bulige na hata Kata ya Bulyanhulu. Je, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri atakuja kukutana na wananchi wa maeneo hayo ili kuweza kusikia kero hii na kuweza kukemea askari hao wenye tabia mbaya? (Makofi)

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba siku zote tumekuwa tukihamasisha na tunaona umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika kushirikiana na vyombo vya dola kukabiliana na uhalifu nchini na ndiyo maana kupitia Kamisheni yetu ya Polisi Jamii ambayo tunayo, tumekuwa tukiandaa utaratibu mzuri, ili utaratibu huo ambao umekuwa ukitumika wa kushirikisha wananchi, ikiwemo Polisi Jamii, ikiwemo Sungusungu, uweze kufuata misingi ya kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia Kamisheni yetu hii ya Polisi Jamii tumekuwa tukitoa miongozo mbalimbali, ili wananchi waweze kutekeleza majukumu yao bila kukinzana na sheria za nchi yetu. Kama kutakuwa kuna mambo yametokea ambayo yanaweza kuwa yamesababishwa aidha na kutokana na uelewa mdogo wa ufahamu wa sheria wa jinsi ya hawa ambao wanaisaidia Polisi kutekeleza hizi shughuli za Polisi Jamii ama itakuwa mengine yametokea labda kwa makosa mengine, labda Mheshimiwa Mbunge labda atuwasilishie tuweze kuyashughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili kuhusiana na ubambikaji kesi, binafsi nilifanya ziara katika Mkoa wa Shinyanga na moja katika mambo ambayo niliyakemea baada ya kutembelea baadhi ya vituo na magereza katika maeneo ya Mikoa ile ya Kanda ya Ziwa na kupata malalamiko ya baadhi ya wananchi ambao walikuwa wamesema wamebambikiwa kesi, moja ni jambo hili ambalo tulilichukulia kwa uzito unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ombi lake la kutaka nifanye ziara katika jimbo lak mahususi, kwa ajili ya kufanya kazi hii ambayo tumeshaifanya katika maeneo mengine ya Mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine nchini ambayo imesaidia sana kupunguza malalamiko haya kwa wananchi tutaifanya baada ya Bunge hili kumalizika tutaandaa hiyo ziara ya kwenda jimboni kwake kwa ajili ya kushughulikia jambo hili mahususi.

Name

Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Primary Question

MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:- Jeshi la Polisi kupitia IGP Ernest Mangu ambaye alifanya ziara Wilayani Kahama mapema mwezi Agosti, 2016 alitangaza kuanzisha Mkoa mpya wa Kipolisi wa Kahama na Wilaya za Kipolisi za Msalala, Ushetu na Kahama; na wilaya hizo mpya za kipolisi zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa askari na vitendea kazi vyao hasa vyombo vya usafiri:- i. Je, ni watumishi wangapi wamepangwa Wilaya mpya ya Kipolisi ya Msalala? ii. Je, Serikali iko tayari kusaidia vyombo vya usafiri hasa magari na pikipiki Wilaya ya Kipolisi ya Msalala? iii. Je, Serikali imejipangaje kujenga ofisi za polisi wilaya na nyumba za makazi kwa askari katika Wilaya za Msalala, Ushetu na Kahama Mjini?

Supplementary Question 2

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Swali langu la nyongeza. Sasa hivi Kibiti imekuwa Kibiti salama, je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha maslahi ya Polisi?

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba, inaboresha maslahi na mazingira ya utendaji kazi wa vyombo vyetu vya Polisi hatua kwa hatua na kadiri ya uchumi wa nchi utakavyokuwa unaimarika.