Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi walio kwenye vijiji vilivyopo kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa kuwarahisishia upatikanaji wa vitabu vya usajili Wilayani?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, hata hivyo nina maswali mawili mafupi.
Swali la kwanza; katika baadhi ya Wilaya, Vijiji pamoja na Kata mpango huu wa kupima ardhi mpaka kupata hatimiliki unachukua muda mrefu kiasi wananchi wanasumbuka, wanahangaika wakifuatilia hati zao. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi hawa kusudi waweze kutumia muda mfupi wasitumie muda mrefu na Hatimiliki zao ziweze kupatikana kwa muda mfupi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; napongeza Serikali kwa kuanza kupima ardhi kwenye Mkoa wa Morogoro katika Wilaya za Ulanga, Kilombero pamoja na Mvomero; na huu mpango wa kupima ardhi unapunguza migogoro ya ardhi kwa upande wa wafugaji pamoja na wakulima.
Je, nauliza Serikali, mpango huu utakamilika lini kwa kupima ardhi kwenye Mkoa wote wa Morogoro kwenye Wilaya zake saba ambazo itasaidia kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekithiri kwa muda mrefu katika Mkoa huu wa Morogoro? Ahsante.

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA YA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza amesema kwamba mpango wa matumizi bora ya ardhi unachukua muda mrefu na hatimaye watu wanachelewa kupata hati zao. Napenda tu nilifahamishe Bunge lako, mpango wa matumizi bora ya ardhi hauwezi kwenda kwa kasi kama tunavyotarajia kwa sababu inategemea pia maridhiano kati ya wanakijiji na matumizi yao katika maeneo yale ambapo unapoandaa mpango huo lazima uhusishe makundi yote ya wafugaji, wavuvi na kila watu walioko pale na lazima pia waangalie ukubwa wa ardhi yao waliyonayo na mpango wanaotaka kuweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima uende taratibu kuhakikisha kila mmoja ameshirikishwa na amekubaliana na mpango, sasa hatuwezi kwenda kwa kasi kwa sababu unashirikisha. Pengine labda elimu iendelee kutolewa hata kabla hatujafika sisi basi elimu iendelee kutolewa ili watu waone umuhimu wa kupanga mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yao ili kuepusha migogoro ambayo mara nyingi inajitokeza.
Swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anaulizia ni lini tutakamilisha kupima ardhi yote katika Mkoa wa Morogoro na kuondoa migogoro iliyopo. Napenda nimhakikishie tu kwamba mpango wa Wizara tulionao siyo wa Morogoro tu, Morogoro ilikuwa ni eneo la mfano katika zile Wilaya tatu ambazo zilikuwa na migogoro pia ili kuweza kujua gharama za upimaji tukitaka kupanua mpango huu utatugharimu kiasi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naona kwamba zoezi lile pale limekwenda taratibu sana kwa sababu linahusisha Wananchi na pia kuweza kujua tunawezaje kukamilisha kupima katika nchi nzima. Ni mpango wa Wizara kuhakikisha kila kipande kinapimwa sasa uzoefu wa Morogoro utatusaidia ku-scale up upimaji na kuweza kujua gharama halisi zinazoweza kutumika na mpango huu tunaendelea nao na kwenye bajeti pia tumeonesha hivyo naomba tu Waheshimiwa Wabunge wawe na subira wakati Wizara inajipanga vizuri.