Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Hivi karibuni Serikali ilikusanya vitabu vyenye dosari vilivyosambazwa shule za msingi nchini. i. Je, Serikali imepata hasara kiasi gani kutokana na dosari hiyo? ii. Je, ni hatua zipi zimechukuliwa kwa waliosababisha hasara hizo?

Supplementary Question 1

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza hapo hapo awali tulikuwa na chombo ambacho kilikuwa kinapitia hivi vitabu na vifaa vya elimu EMAC kabla ya kwenda mashuleni. Na kwa kuwa EMAC ilifutwa rasmi, sasa niulize Serikali ina mpango gani wa kuanzisha chombo kingine au chombo mbadala ambacho kitakagua vitabu na vifaa vya elimu kabla ya kwenda mashuleni? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni dhahiri kwamba sasa hivi kuna upungufu mkubwa sana wa vitabu kwa shule za msingi hasa darasa la kwanza mpaka la tatu; je, Serikali ina mpango gani wa haraka ili kutatua changamoto hii?

Name

Prof. Joyce Lazaro Ndalichako

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Answer

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli Serikali ilivunja EMAC ambayo ni Education Management Approve Committee iliyokuwa inahusika na kupitisha machapisho na vitabu vya elimu baada ya chombo hicho kushindwa kutekeleza wajibu wake vizuri na tulishuhudia kwamba pamoja na kuwepo kwa chombo hicho, lakini bado vitabu vilikuwa na makosa mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba sasa hivi kazi ya kupitisha vitabu inafanywa na Taasisi ya Elimu Tanzania, lakini niseme kwamba Serikali itaangalia namna ya kuangalia utaratibu mwingine, baada ya kuondoa EMAC kwa sababu pia Taasisi ya Elimu inakuwa inaelemewa na kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa vitabu, naomba nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba sasa vitabu vimekwishafanyiwa marekebisho na zaidi ya nakala 9,000 za vitabu vya kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu vimekwishasambazwa shuleni, kwa hiyo, sasa hivi tatizo hilo Serikali imekwishasambaza vitabu vilivyorekebishwa.