Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Primary Question

MHE. MUSSA B. MBAROUK aliuliza:- Kumekuwa na sintofahamu kwa baadhi ya wafanyabiashara na TRA kuhusu mashine za EFDs hususani bei za mashine na aina za mashine. (a) Je, bei halali ya mashine ya EFD kulingana na aina na ubora wake ni shilingi ngapi? (b) Kwa kuwa mashine za EFDs zinafanya kazi kwa niaba ya TRA, je, kwa nini Serikali isitoe mashine hizo bure kwa wafanyabiashara?

Supplementary Question 1

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ndiyo, maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, risiti ni supporting document katika masuala ya mahesabu. Sasa risiti zetu za EFD machines zina tabia ya kufutika maandishi baada ya muda mfupi, TRA tulipokutana nao katika Kamati yetu ya PAC walikiri kwanza kwamba karatasi wanazotumia ni dhaifu lakini wakasema kwamba watafanya marekebisho ya karatasi hizo ili zisifutike maandishi kwa muda mfupi. Mpaka leo, tarehe 10 Septemba, bado marekebisho hayo hayajafanyika.
Mheshimiwa Spika, nataka kujua sasa TRA tuipe muda gani ili iweze kufanya marekebisho ya karatasi hizi za risiti?
Pili, mwaka 2017 mwanzoni wafanyabiashara wa Mkoa wa Mbeya waligoma baada ya baadhi yao kwenda China na kubaini kwamba mashine zile gharama yake ni sawasawa na shilingi 90,000 ya Kitanzania kwa mujibu wa vyombo vya habari vilivyoripoti wakati ule. Sasa nataka kujua, je, hizi mashine bei yake halisi hasa na taarifa hizi zina ukweli kiasi gani?(Makofi)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kuhusu karatasi zinazofutika, napenda kuliambia Bunge lako tukufu kwamba Serikali ilishatoa taarifa kwa wafanyabiashara wote kuhusu wapi pa kununua karatasi hizi kwa ajili ya kutoa risiti za mashine za EFD. Zipo karatasi fake, hatukatai, zipo sokoni, lakini tumewaelekeza wafanyabiashara wote waende kununua karatasi hizi kutoka kwa mawakala waliothibitishwa na kuidhinishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania ili kuepuka tatizo hili la karatasi kufutika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, anasema wawape muda mpaka lini, hatuhitaji kupewa muda kwa sababu tatizo hili tulishalishughulikia tayari kama Serikali.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili; nashukuru umenisaidia kumjibu kwamba gharama za mashine ndizo nilizozitaja hapa kulingana na aina ya mashine na aina ya biashara mfanyabiashara anayoifanya. Kwa hiyo, hizo nyingine za kwenye vyombo vya habari, hizo kama Serikali hatuzijui, tunazojua ni hizi nilizozisema, ndiyo kauli na taarifa sahihi kutoka Serikalini. (Makofi)