Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Janet Zebedayo Mbene

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ileje

Primary Question

MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:- Wilaya ya Ileje imejaliwa kuwa na rasilimali ya makaa ya mawe ya Kiwira na Kabulo na STAMICO imekaririwa kuanza rasmi kuuza makaa hayo kwa kasi ili kukidhi mahitaji ya viwanda vya saruji na kukuza pato la Taifa, aidha, STAMICO ilianza uzalishaji wa majaribio ya makaa ya mawe katika Mgodi wa Kabulo tarehe 30/04/2017. (a) Je, Mgodi wa Kabulo utaendelea kuchimba baada ya majaribio hayo na ni nani anayefanya uchimbaji huo? (b) Je, kuna makubaliano gani na Wilaya ya Ileje juu ya mrahaba na uchumi kwa wana Ileje? (c) Je, ni lini Mgodi wa Kiwira utaanza kufanya kazi na ni nini hasa kinachokwamisha?

Supplementary Question 1


MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, kwa kuwa mradi huu ni mradi ambao unatambulika kuwa ni mradi wa kimkakati na kwa kiasi mpaka 2013 ulikuwa unatengewa fedha ya maendeleo lakini kuanzia mwaka wa fedha 2014/2015 hadi sasa hivi hakuna fedha yoyote ambayo imekuwa ikitengewa mradi huu ilhali sasa hivi mradi huu umeanza kufanya kazi na tayari mbia amepatikana na wiki hii ameshaweka saini pamoja na STAMICO ya kuanza kuchimba makaa ya mawe katika Mgodi wa Kabulo.
Je, Serikali imeuondoa mradi huu katika miradi ya kimkakati? Na kama ni hivyo, je, hiyo fedha ya kuendeleza hasa ukarabati wa Mgodi wa Kiwira wenyewe inayohitajika sasa hivi kwa sababu tayari mbia ameshapatikana itapatikana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa mradi huu ambao umekuwa kwa muda mrefu ukinufaisha Wilaya nyingine ya jirani sasa hivi umeanza kutambulika rasmi kuwa ni mradi wa Ileje na kwa urahisi wa kuufikia mradi huu kuna daraja katika Mto Mwalisi ambalo liliharibika kwa muda mrefu la kilometa karibu saba na barabara yake, imesababisha mradi huu sasa kuwa unatumia njia ndefu ya kupitia Kyela ambayo ni karibu kilometa 36 na kuleta gharama kubwa na kuongeza gharama kubwa kwa mradi huu.
Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kuwa hii barabara pamoja na Daraja la Mwalisi ambalo ndilo linalounganisha Wilaya ya Ileje na Mradi wa Kiwira na Kabulo inatengenezwa haraka sana ili mwekezaji huyu sasa hivi aanze kufanya kazi bila matatizo?

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya. Ni mama ambaye yuko makini, anafuatilia sana majukumu yake ya kuwawakilisha wananchi wa Ileje kama Mbunge. Ni kweli mama huyu amejitosheleza sana katika jimbo hilo, Mungu ambariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kwamba je, Mradi huu wa Kiwira tumeuondoa katika miradi ya kimkakati? Jibu jepesi kabisa na la haraka ni kwamba bado mradi huu tunautambua kwamba ni mradi wa kimkakati ikiwa ni pamoja na miradi mingine mikubwa ambayo kwa kweli tunafahamu kama Serikali kwamba miradi ya kimkakati ni ile miradi mikubwa ambayo inawezesha miradi mingine au sekta nyingine kufanya kazi. Na kwa sababu sasa hivi tunataka nchi yetu iende katika kuwa nchi ya viwanda, makaa ya mawe ni kitu muhimu sana katika uendelezaji wa viwanda vyetu na hasa viwanda vya simenti. Kwa hiyo, mradi huu bado ni mradi wa kimkakati tunautambua kama miradi mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini sasa Serikali tutaiwezesha kujenga barabara hii ya Kiwira – Kabulo. Sisi kwa kushirikiana na TARURA, Wizara ya Madini tumekwishawaandikia TARURA barua ya kuhakikisha kwamba kilometa zile saba zinajengwa katika mradi huu ili kupunguza kilometa 36 ambapo mwekezaji huyu anatumia kwa maana ya kupeleka kusafirisha makaa ya mawe, inaingiza gharama kubwa kwa sababu tunatambua kuwa makaa ya mawe ni bulky mineral, ni mzigo mkubwa. Kwa hiyo unapoweka katika hali ya kusafirisha mwendo mrefu gharama inakuwa ni kubwa na mtumiaji wa mwisho analipa gharama kubwa kiasi kwamba inamfanya huyu mwekezaji apate shida katika kuendeleza mradi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumelitambua hilo na imetengwa shilingi bilioni 2.5 ya kujenga kilometa saba na vilevile imetengwa bilioni 1.5 ya kujenga daraja ambalo liko pale.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, sisi tunaendelea kulisimamia na sisi kama Wizara ya Madini tunahakikisha kwamba tuko pamoja na Serikali kuwawezesha wawekezaji wote katika sekta ya madini wafanye kazi kwa faida na wasifanye kazi kwa hasara. Ahsante sana.