Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Primary Question

MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:- Tatizo la maji Wilaya ya Momba halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu mpaka sasa. Je, ni lini Serikali ya Awamu ya Tano itamaliza tatizo hilo katika Wilaya ya Momba?

Supplementary Question 1

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Unavyoona Wabunge wamesimama ujue ndiyo hali ya maji nchini tatizo jinsi lilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu amekiri kabisa kwamba tatizo la maji lipo Wilaya ya Momba na sio tu Momba peke yake lipo nchi nzima. Sasa kauli mbiu ya ahadi ya kumtua mama ndoo kichwani imekuwa ngumu kweli kweli kutekelezeka kama ilivyo ahadi ya kupeleka milioni 50 kwa kila kijiji. (Makofi)
Je, Serikali inaweza ikatueleza kwa nini imekuwa rahisi kununua ndege ama Bombadier kuliko kupeleka maji safi na salama kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya mijini maji tunayotumia ku-flash kwenye vyoo ni bora kuliko maji ambayo wanatumia wananchi wa vijijini kwa sababu maji yale wananywea ng’ombe na wananchi wa kawaida wanakunywa huko huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini sasa Serikali isiwe na huruma kwa wananchi wa vijijini nchi nzima ili muweze kutatua hili tatizo la maji na sisi tuondokane na hii kero ambayo wananchi wamekuwa wanauliza kila siku wanahitaji maji safi na salama? Ahsante.

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza napenda nimjibu Mheshimiwa Mbunge kuwa Mungu anaposema kwamba yapaswa kushukuru kwa kila jambo, Serikali inafanya jitihada kubwa sana katika kuhakikisha inatatua matatizo ya maji. Tunaona miradi mikubwa ambayo inatekelezwa, tunatoa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Tabora pamoja na miji ya Igunga, tunaona Mheshimiwa Rais anavyozindua miradi kila kukicha Nansio na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji jukumu letu ni kuhakikisha tunwapatia wananchi maji kwa maana ya maji safi, salama na yenye kuwatosheleza na nimefanya ziara katika Mkoa wa Songwe kwa kuona changamoto hiyo, tumetenga kiasi cha shilingi bilioni tisa na katika Jimbo lako tumetenga bilioni 1.77 katika kuhakikisha tunatatua tatizo hilo la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kazi ya Mbunge ni kusimamia. Naomba asimamie fedha hizo katika kuhakikisha wananchi wako wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, lengo la Wizara yetu sio kuwapa wananchi maji masafi. Niwaombe sana wataalam wetu kwa maana ya wahandisi wa maji, wabuni miradi ambayo itakuwa na tija kwa wananchi wetu katika kuhakikisha wanapata maji yaliyo safi na bora ili kuhakikisha wanapata huduma hii muhimu.

Name

Dr. Immaculate Sware Semesi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:- Tatizo la maji Wilaya ya Momba halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu mpaka sasa. Je, ni lini Serikali ya Awamu ya Tano itamaliza tatizo hilo katika Wilaya ya Momba?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Kwa kuwa upatikanaji wa maji safi na salama huathiri afya, muda wa uzalishaji na hivyo huathiri uchumi wa kaya au jamii kwa ujumla. Sasa Serikali yetu tunajua dhahiri kuna changamoto ya maji nchini.
Je, mnajua kwamba bila kutatua changamoto ya maji nchini hatutakaa kufikia lengo la uchumi wa kati 2020/ 2025? (Makofi)

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwa maana ya kwamba tunatambua sasa hivi nchi yetu inaenda katika nchi ya viwanda kwa maana ya uchumi wa kati na tunajua kabisa maji ni rasilimali muhimu sana na maji hayana mbadala sio kama chai ukikosa chai labda utakunywa uji. Tunajua viwanda vinahitaji maji, wananchi wanahitaji maji, kwa hiyo tutaongeza jitihada kubwa sana katika kukarabati, kujenga na kuunda miradi mikubwa katika kuhakikisha tunatatua tatizo hili la maji na tuwe na vyanzo vya kutosha ili mwisho wa siku azma iweze kutimilika. (Makofi)

Name

Dr. Mary Michael Nagu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Primary Question

MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:- Tatizo la maji Wilaya ya Momba halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu mpaka sasa. Je, ni lini Serikali ya Awamu ya Tano itamaliza tatizo hilo katika Wilaya ya Momba?

Supplementary Question 3

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo; vijiji vingi vya Wilaya ya Hanang havina maji na vile ambavyo vimebahatika kuchimbiwa visima, visima havijakamilika.
Je, Mheshimiwa Waziri ananiambia nini ili kuhakikisha vile visima vilivyochimbwa vinakamilika na wale waliobahatika kuwa na visima hivyo waweze basi kunywa maji na kutumia kwa matumizi mengine? Ahsante.

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza napenda nimpongeze sana mama yangu Mheshimiwa Nagu amekuwa ni mtetezi mkubwa sana wa wananchi wake katika suala zima la maji. Amekuwa analipigania na amekuwa akifuatilia katika Wizara yetu ya Maji na Waziri wangu ambaye ni Mheshimiwa Kamwelwe aliwaagiza watu wa DDCA kwenda kuchimba visima vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie kwamba tutawaagiza watu wetu wa DDCA katika kuhakikisha vile visima wanavikamilisha kwa wakati, ili wananchi wako waweze kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza. (Makofi)