Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Halima Abdallah Bulembo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HALIMA ABDALLAH BULEMBO aliuliza:- Mkoa wa Kagera upo karibu na Ziwa Victoria lakini una uhaba mkubwa wa Maji:- Je, ni kwa nini Wizara isibuni mradi mkubwa wa kutoa Maji Ziwa Victoria kupeleka Kagera kama ule wa kutoa Maji Ziwa Victoria kwenda Tabora?

Supplementary Question 1

MHE. HALIMA ABDALLAH BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Moja ya changamoto mbalimbali za maji ni ukosefu wa vyanzo vya maji, lakini sisi Mkoa wa Kagera Mwenyezi Mungu ametujaalia tuna vyanzo vingi vya maji. Ukiachilia mbali Ziwa Victoria tuna mito mingi ukiwemo Mto Kagera, lakini shida ya maji imekuwa ni kubwa zaidi na kuna wakati Wilaya ya Ngara kuna wanafunzi walilipotiwa kukosa masomo kwa sababu ya kutafuta maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo Serikali imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa ya maji nchini lakini Mkoa wa Kagera umekuwa ukiwekwa pembeni. Waziri atakubaliana na mimi sasa umefika muda Mkoa wa Kagera uwe una mradi mkubwa mmoja wa maji ili uweze kusambaza maji katika vijiji vyote vya Mkoa wa Kagera na huyo Mkandarasi Mshauri atakubali suala hili la kimkakati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu langu la pili, Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la AFD lilikubali kufadhili Mradi wa Maji Bukoba Mjini. Je, Serikali ipo tayari kuwaomba Serikali ya Ufaransa iendelee kufadhili Mkoa wa Kagera ili waweze kutatua tatizo la maji kuwasaidia wananchi hasa hasa akinamama na watoto wa Mkoa wa Kagera? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILAIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekati, napenda kumpongeza mdogo wangu Mheshimiwa Halima Bulembo; ni miongoni mwa Wabunge makini sana katika Bunge hili na amekuwa ni mtetezi mkubwa sana kwa akinamama na watoto katika suala zima la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie, jukumu la Wizara ya Maji ni kuhakikisha Wanakagera wanapata maji na si maji tu, ni kwa maana ya maji safi salama na yenye kuwatosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu kwa kuona hali ya changamoto ya maji kwa Mkoa wa Kagera tumetekeleza Mradi mkubwa sana katika Mji wa Kagera zaidi ya bilioni thelathini na mbili katika kuhakikisha wananchi wa Bukoba wanapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; tuna mradi mwingine katika miji 17, tunaenda kujenga mradi mkubwa sana katika Mji wa Kayanga kwa kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa katika kuhakikisha wananchi wa Kagera wanaenda kupata maji hayo. Kingine, katika Bajeti ya mwaka 2018/ 2019 tumetenga zaidi ya Sh.13,520,000,000/= katika kuhakikisha wananchi wa Kagera wanapata maji. Niwaombe sana wataalam wetu wa maji wa Mkoa wa Kagera wasilale na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Kagera wasimamie fedha hizi katika kuhakikisha zinaenda kutatua tatizo la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili nataka nimtie moyo Mheshimiwa Mbunge; ukisoma Mathayo-7 inasema ombeni nanyi mtapewa, bisheni hodi nanyi mtafunguliwa. Tumeshawafungulia wananchi wa Kagera, sisi tuko tayari kuendelea kuwatafuta wafadhili katika kuhakikisha tunaenda kutatua tatizo la maji Kagera. Ahsante sana. (Makofi)