Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Primary Question

MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:- Serikali iliahidi kuweka mipaka ya kutenganisha Vijiji vya Jimbo la Mlimba na RAMSAR SITE kwa kuwashirikisha wanavijiji wa maeneo husika lakini kazi hiyo haikufanyika badala yake wakulima waliambiwa mwisho wao kwenye maeneo hayo ni mwezi Agosti na wafugaji mwisho wao kwenye maeneo yao ni Julai:- • Je, kwa nini Serikali haikutekeleza jukumu lake la kuweka mipaka badala yake wakulima na wafugaji wamepewa barua ya kusitisha kutumia maeneo hayo na kusababisha taharuki kubwa kwa wananchi? • Kwa kuwa wananchi hao walifungua kesi kupinga maonevu hayo mwaka 2015 kesi Na. 161 kuhusu mgogoro huo na bado kesi hiyo haijakwisha, kwa nini Serikali imewasitisha wananchi hao kuendelea kutumia maeneo hayo kabla ya kesi haijakamilika?

Supplementary Question 1

MHE.SUZAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya Naibu Waziri. Mheshimiwa Waziri, amezungumzia suala la Malinyi na Ulanga, swali langu lilijikita zaidi Jimbo la Mlimba lenye kata 16 na kuna kata zisizopungua 14 ambazo zinatakiwa ziende zikafanyiwe marekebisho; na jibu lake limejikita kwenye kata tatu tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pamoja na mpango huo wa Serikali kutaka kuhifadhi hilo eneo, wananchi hatukatai, lakini kuna barua zimeshasambazwa kwamba, wananchi wanatakiwa waondoke, wafugaji na wakulima mwisho tarehe 30 mwezi Agosti. Zoezi la uelimishaji kweli limefanyika katika vijiji hivyo saba na imeundwa timu ya watu 15, lakini kiangazi ndiyo hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waliahidi tangu mwezi Agosti watamaliza hilo zoezi kwenye hizo kata 14, ona, wamefikia kata tatu hata kata tatu wameunda tu timu lakini hawaenda kuweka vigingi. Je, lini sasa Serikali itaenda kuweka vigingi kwa kisababisho kwamba hamna hela? Kwa nini wanatufanyia hivi jamani? Lini watakwenda, hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wananchi hawana uhakika wa maeneo haya kama yataenda kwenye hifadhi ama watabaki nayo, katika kata zote 14 wananchi wanagoma kuchangia maendeleo ya kujenga shule na zahanati kwa sababu hawajui hatima yao katika maeneo hayo. Sasa Serikali kwa nini wanaleta kigugumizi hawapeleki hela? Wanatunyang’anya maeneo lakini wanasema hawana hela za kwenda kuweka mipaka na kiangazi ndio hiki je, ikifika wakati wa mvua watakwenda huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako tayari kwenda lini waniahidi hapa jamani? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza kwa kuamua kushirikiana vizuri kabisa na Serikali kwamba kuna haja ya kuweka hivyo vigingi ili mipaka ieleweke kwa wananchi kusudi waendelee kushughulika na shughuli zao na maeneo ambayo yamehifadhiwa yaendelee kuhifadhiwa, nampongeza sana kwa msimamo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuweka vigingi ni kweli kabisa kwamba tulisimamisha kwa sababu ya mgogoro uliokuwepo, lakini kuna hatua kadhaa ambazo tulikuwa tumezichukua. Hatua ya kwanza tuliunda Kamati ya watu 22 wa kupitia wilaya zote tatu ili waweze kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, namna bora ya kuhakikisha kwamba vile vingingi vinawekwa na kupunguza migogoro ambayo ilikuwepo. Kamati hiyo tunatarajia kwamba itamaliza kazi yake na italeta ripoti wiki mbili zijazo kuanzia leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwenda kutenga fedha naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zimetengwa, fedha zipo; na nitumie nafasi hii kweli kuungana naye kwamba ni kipindi muafaka kwa sababu mvua zikianza itakuwa ni vigumu sana kwenda kuweka mipaka katika lile eneo hasa kipindi cha mvua, lakini kipindi hiki ndio kipindi muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutahakikisha kwamba ndani ya mwezi huu wa 10 mipaka hiyo inawekwa na nitaagiza taasisi zinazohusika zihakikishe kwamba hili zoezi linakamilika na wananchi wanashirikishwa na yeye mwenyewe Mbunge anashiriki kikamilifu katika hilo zoezi ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawasawa.

Name

Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Primary Question

MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:- Serikali iliahidi kuweka mipaka ya kutenganisha Vijiji vya Jimbo la Mlimba na RAMSAR SITE kwa kuwashirikisha wanavijiji wa maeneo husika lakini kazi hiyo haikufanyika badala yake wakulima waliambiwa mwisho wao kwenye maeneo hayo ni mwezi Agosti na wafugaji mwisho wao kwenye maeneo yao ni Julai:- • Je, kwa nini Serikali haikutekeleza jukumu lake la kuweka mipaka badala yake wakulima na wafugaji wamepewa barua ya kusitisha kutumia maeneo hayo na kusababisha taharuki kubwa kwa wananchi? • Kwa kuwa wananchi hao walifungua kesi kupinga maonevu hayo mwaka 2015 kesi Na. 161 kuhusu mgogoro huo na bado kesi hiyo haijakwisha, kwa nini Serikali imewasitisha wananchi hao kuendelea kutumia maeneo hayo kabla ya kesi haijakamilika?

Supplementary Question 2

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Suala la migogoro ya ardhi, misitu, maliasili na wananchi inazidi kuongezeka kila siku hapa nchini hali ambayo inaipatia Serikali hasara kubwa ya kuweka ulinzi katika maeneo hayo, halikadhalika wananchi wanaathirika sana kwa kuchomewa majumba yao na mali zao kuharibiwa kutokana na zoezi hilo. Sasa inaonekana hii dhana ya ushirikishi inayotumika hapa labda inatumika vibaya au hawajashirikishwa kwa dhati. Je, Mheshimiwa Waziri na Serikali yake wako tayari sasa kuja Zanzibar kujifunza mbinu walizotumia katika haya na wakafanikiwa?

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

NAIBU WAZIRI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba niseme kwamba tuko tayari kabisa kwenda kujifunza mbinu bora za kuhakikisha migogoro hii haipo. Kama walivyofanya Zanzibar basi na sisi tungependa tutumie mbinu hizo hizo kuhakikisha kwamba huku migogoro yote inamalizika.