Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:- Katika kuelekea uchumi wa viwanda Tanzania, Serikali imedhamiria kuwepo kwa viwanda vya kimkakati. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Kiwanda cha Kuchakata ao la Tumbaku kinajengwa katika Mkoa wa Tabora?

Supplementary Question 1

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora na Kanda ambazo tunalima tumbaku kwa miaka zaidi ya 10 tumekuwa tunaomba kiwanda cha tumbaku kijengwe Mkoa wa Tabora na ikithibitika kabisa kwamba asilimia 60 ya tumbaku ya Tanzania inalimwa Mkoa wa Tabora, lakini mwaka jana tu Serikali imeruhusu kiwanda cha pili kujengwa Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokuwepo kwa kiwanda cha Tumbaku Mkoa wa Tabora kwanza kumewanyima ajira vijana wetu wa Tabora, lakini kubwa zaidi ni kwamba wakulima wa tumbaku wanachajiwa gharama za kusafirisha tumbaku kutoka Tabora kupeleka Morogoro, kwa hiyo wanaongezewa maumivu. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali iliruhusu sasa mwaka jana kiwanda kipya kujengwa Mkoa wa Morogoro ambako hakulimwi tumbaku, iko tayari sasa kushawishi kile kiwanda kimoja kihamishiwe Mkoa wa Tabora ili wakulima wa Tabora nao pia waweze kunufaika na zao lao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwenye jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kawmba uzalishaji umepungua, ni kweli umepungua lakini umepungua kutokana na wakulima hawapewi makisio na kampuni. Wana lengo la kulima, wanakopa hata msimu huu wenyewe tu Kaliua peke yake zaidi ya Vyama vya Msingi sita vimekosa makisio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zao hili ni zao la uchumi wa Taifa na Mkoa wa Tabora, je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kwamba Vyama vya Msingi ambavyo vimekosa makisio mwaka huu vinapatiwa makisio? Kwa sababu uchumi wa Tabora unategemea tumbaku na uchumi wa familia unategemea tumbaku? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na dhamira nzuri ya Serikali na wananchi wa Tabora kupenda kujenga Kiwanda cha Kuchakata Tumbaku Tabora lakini pia Muwekezaji huwa anaangalia mazingira ya yanayoweza kumuwezesha kupata faida zaidi na kufanya shughuli zake vizuri zaidi. Kwa hiyo kama tulivyosema awali tutaendelea kuhamasisha lakini pia kuwakatisha tamaa wale ambao wameamua kuwekeza Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu kutoa makisio; kwa kweli kama kuna zao ambalo linapambana na changamoto ni pamoja na hili la tumbaku. Fikiria mteja anaanza kwanza kuhamasishwa “uvutaji wa sigara ni hatari kwa maisha yako” lakini pia uweze kufanya biashara. Kwa hiyo kwa misingi hii unakuta hata kampuni wakati mwingine zinashindwa kufikia malengo kutokana na mazingira kama hayo. Hata hivyo, nizidi kuwaomba wananchi wa Tabora, wote kwa pamoja tutaendelea kufuatilia na kuona kwamba hali ya bei yanzuri kwa upande wa wakulima inapatikana. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:- Katika kuelekea uchumi wa viwanda Tanzania, Serikali imedhamiria kuwepo kwa viwanda vya kimkakati. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Kiwanda cha Kuchakata ao la Tumbaku kinajengwa katika Mkoa wa Tabora?

Supplementary Question 2

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali ya Awamu ya Tano imejinasibu kwamba ni Serikali ya viwanda na tunataka kuhakikisha tutakapofikia mwaka 2025 tuwe kwenye nchi ya kipato cha kati. Sasa nataka kufahamu kutoka kwa Waziri; tulipofanya vikao vya Kamati alikuwa anatueleza kwamba maghala ya korosho yaliyopo Masasi yamegeuzwa, tunafahamu, kufanywa maghala badala ya viwanda na kwamba kuna kesi zilizoko mahakamani kwa sababu ya kutanzua migogoro iliyoko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba, mpaka sasa hivi wamefikia hatua gani ya kesi hizi zilizoko mahakamani ili kuhakikisha viwanda vile vinafufuliwa badala ya kuendelea kutumika kama maghala na wale watu waliovinunua wakati huo? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza katika majibu yangu ya hapo awali niliahidi kutembelea eneo hilo, nasikitika kuliarifu Bunge kwamba sikuweza kutembelea. Hata hivyo, kama ambavyo nimekuwa nikizungumza siku zote, Wizara kwa kushirikiana pia na Kamati yetu ya Viwanda, Biashara na Mazingira tupo katika kuendelea kuhakikisha kuona kwamba wawekezaji wanatimiza wajibu wao, lakini pia kuhakikisha maeneo yote ambayo yanalima korosho basi korosho hiyo iweze kubanguliwa au kuongezwa thamani kabla ya kusafirishwa. Kwa hiyo tupo katika mchakato na mchakato wa kisheria kawaida huwa hatuuingilii.

Name

Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:- Katika kuelekea uchumi wa viwanda Tanzania, Serikali imedhamiria kuwepo kwa viwanda vya kimkakati. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Kiwanda cha Kuchakata ao la Tumbaku kinajengwa katika Mkoa wa Tabora?

Supplementary Question 3

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa tumbaku nyingi inayolimwa Mkoa wa Tabora inatoka Wilaya ya Urambo, Kaliua, Uyui na kwingineko. Je, Serikali iko tayari kuja kuona eneo ambalo lilishatengwa kwa ajili ya kiwanda Wilayani Urambo? Kwa kuwa wakulima wanapoteza kilo nyingi sana kusafirisha tumbaku kutoka Tabora kupeleka Morogoro.

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tutakapopata nafasi tutaweza kuja kuona na kushauri kadri itakavyowezekana japo kama ambavyo hapo awali nimeeleza changamoto zinazojitokeza.