Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Primary Question

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:- Takwimu za Mpango wa Maendeleo 2016/2017 zimeonesha kuwa Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa Mikoa mitano (5) iliyo maskini zaidi nchini:- • Je, Serikali inafanya nini kuhakikisha Mikoa hiyo inapata rasilimali fedha na watu ili iweze kuondokana na hali hiyo ya umaskini? • Je, nini kifanyike kwa Mkoa wa Kigoma ili kujenga ulinganifu katika maendeleo? • Je, kwa nini Serikali isitenge shilingi bilioni 5 kwa kila mwaka kwa kila Mkoa ili kuondoa kitisho cha Mikoa hiyo kuachwa nyuma kimaendeleo?

Supplementary Question 1

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, naomba kwa ruhusa yako kabla sijauliza maswali yangu mawili madogo ya nyongeza, kwanza niwashukuru timu ya kampeni iliyotoka Kakonko, uniruhusu niwapongeze Wabunge wote wa CCM na Upinzani waliokuja Kakonko kwa kampeni. Tunasema tunashukuru sana kwa changamoto mlizotupa na tunaendelea kumpongeza Mheshimiwa Chiza kwa ushindi mnono alioupata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno machache ya utangulizi, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, msingi wa swali langu ni mikoa ile mitano ambayo iko nyuma, ndiyo msingi wa hoja na si suala la Ilani ya Uchaguzi ya CCM, si suala la Mpango wa Miaka Mitano. Hoja ni mikoa mitano iliyoko nyuma ambayo inahitaji kupata special attention, inahitaji equalization ili iweze kulingana na mikoa mingine ndiyo msingi wa swali.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la nyongeza ni kwamba miradi yote aliyoitaja ukiacha ujenzi wa reli ya kati, hiyo miradi haijatekelezwa na mingine ina miaka 20. Hiyo mikoa mitano iliyoko nyuma inahitaji kubebwa, kusaidiwa itoke katika maeneo yale ili iweze kuwa sawa sawa na mikoa mingine. Je, ni nini mkakati wa Serikali kwa mikoa hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza ni kwamba hiki kinachoitwa North-West Grid, ni mradi ambao una urefu wa kilometa 2,500 kutoka Tunduma – Nyakanazi kupitia Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Kasulu – Kibondo mpaka Nyakanazi. Je, mradi huu utakapoanza kutekelezwa kwa nini usiwe na wakandarasi zaidi ya watatu ili uishe kwa haraka ili wananchi tupate umeme katika maeneo haya? (Makofi)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza amesema msingi wa swali lake ni mikoa mitano maskini, lakini alikwenda specific na kuutaja Mkoa wa Kigoma na ndiyo maana na mimi nilijibu specifically kwa Mkoa wa Kigoma, nini ambacho Serikali yetu inafanya.
Mheshimiwa Spika, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba kupitia miradi ya maendeleo kama nilivyoitaja ndiyo fursa a kiuchumi hufunguliwa kwa ajili ya wananchi wetu kwenye mikoa husika. Kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo, mpango wa maendeleo wa mwaka mmoja mmoja, Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ndiko vipaumbele huwekwa kulingana na geographical location ya mikoa yetu na aina ya umaskini. Kwa hiyo, miradi hupangwa kulingana na miongozo hiyo niliyoitaja. Kwa hiyo, naomba tu Mheshimiwa Daniel akubaliane na jibu hili kwamba hatuwezi kupanga bajeti nje ya miongozo na mipango inayotuongoza.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili ametoa pendekezo, tutakaa kama Serikali na Wizara ya Nishati kuona jinsi gani mradi huu wa North – West Grid utatekelezwa kwa haraka ili kurahisisha maendeleo ambayo tunayataka yafike kwa wananchi wetu.