Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:- Mwaka 2016 Serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi aliahidi kuipatia Wilaya ya Mbulu Baraza la Ardhi la Wilaya:- • Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa na hatimaye Wilaya ya Mbulu kuwa na Baraza la Ardhi la Wilaya? • Je, ni kwa nini Serikali isipime ardhi ya wananchi wa Wilaya ya Mbulu na kuwapatia hati ili kuondoa migogoro ya ardhi?

Supplementary Question 1

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, kwanza niipongeze Serikali kupitia Waziri wa Ardhi kwa kazi kubwa inayofanya Wizara hii. Pili niulize maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, kwa kuwa tatizo kubwa linalowakabili akina mama wajane, watoto, ambao wamepoteza wapendwa wazazi wao ni katika tatizo hili la kesi na mashtaka ya ardhi; na kwa kuwa familia nyingi zinazopata matatizo hayo hazina uwezo wa kifedha kuweka wanasheria. Je, ni kwa namna gani sasa Serikali itatafuta msaada wa kisheria kwa akina mama wajane na watoto warithi wa ardhi katika familia mbalimbali zinazopoteza wazazi wao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, majibu ya Wizara yameniridhisha kwa kiasi kikubwa, je, ni kwa namna gani Wilaya ya Mbulu ambayo hivi sasa kesi nyingi zinazoendeshwa katika Baraza la Ardhi la Babati zinapata nafasi ya fursa ya kupimiwa ardhi kwa msaada wa Serikali, wananchi na wadau wengine ili tatizo hili la mashtaka mengi ya ardhi katika Baraza la Babati yapungue na hata kwa Mbulu kwa sababu hata tukipata Baraza bado tatizo litakuwa kubwa kwa mashtaka yatakayoendelea kutokana na hali hii ya kunyang’anyana ardhi kwa wale wenye uwezo na wasio na uwezo? (Makofi)

Name

William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Answer

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali inao mkakati wa kutoa msaada wa kisheria kwa makundi kadhaa yenye shida kama hizi, lakini kwanza kwa Mbulu tulifikiri kitu cha muhimu tusogeze huduma na kuanzisha Baraza la Ardhi kwa sababu tusingeweza kufikiria huduma za kisheria wakati huduma yenyewe haitolewi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba kwanza atuvumilie, mwaka huu Mungu akipenda lazima lile Baraza ambalo amelipigania kwa muda mrefu Mbulu Mjini litaanzishwa.
Mheshimiwa Spika, pia lile Baraza la Babati linaendelea kufanya kazi. Tutahakikisha kesi zote za Mbulu ambazo ni nyingi sana, tukishamuweka pale Mwenyekiti pale Mbulu kesi zote za Mbulu zitarudi Mbulu kutoka Babati ili angalau iwarahisishie hawa akina mama na watu wasio na uwezo waweze kupata hii huduma karibu na mahali wanakoishi. (Makofi)

Name

Willy Qulwi Qambalo

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Karatu

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:- Mwaka 2016 Serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi aliahidi kuipatia Wilaya ya Mbulu Baraza la Ardhi la Wilaya:- • Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa na hatimaye Wilaya ya Mbulu kuwa na Baraza la Ardhi la Wilaya? • Je, ni kwa nini Serikali isipime ardhi ya wananchi wa Wilaya ya Mbulu na kuwapatia hati ili kuondoa migogoro ya ardhi?

Supplementary Question 2

MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, Mabaraza haya ya Ardhi hasa yale ya ngazi ya Kata yanafanya kazi kubwa sana kwa sababu yako karibu na wananchi lakini mabaraza haya yamekuwa na changamoto kubwa hususani eneo la maslahi yao kwa maana ya posho za usafiri na posho za vikao pamoja na vitendea kazi. Nini kauli ya Serikali juu ya kuhakikisha Mabaraza yale ya Kata yanawezeshwa ili yafanye kazi zao kwa ufanisi mkubwa? Mheshimiwa Spika, ahsante.

Name

William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Answer

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli katika muundo huu wa Mabaraza tunaanza na Mabaraza hayo ya Kata na kwa muundo wake Wajumbe wengi wa Baraza lile ni wenyeji wa maeneo yale. Kazi hii kwa kweli ni ya kujitolea kwa sababu inarahisisha na inaondoa kero ya watu wao, hatuna mtumishi wa kudumu kwenye Baraza la Kata.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunatarajia wananchi wajue hilo na ikiwezekana Halmashauri za Vijiji vinavyozunguka Kata ile wafanye utaratibu wa kuchangia uendeshaji wa lile Baraza la Kata, kwa sababu Baraza lile la Kata linatakiwa kusimamia na kusuluhisha migogoro kadhaa inayokuwepo katika maeneo yanayozunguka pale kwenye Kata. Baada ya hapo rufaa huwa zinaenda kwenye Baraza la Wilaya, kutoka kwenye Baraza la Wilaya rufaa zinakwenda Mahakama Kuu.
Mheshimiwa Spika, nataka nimuarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatuna posho kwenye Mabaraza ya Kata. Tunataraji kwamba viongozi wanaopendekezwa na wenzao kufanya kazi ile ni wale ambao wana uwezo na wana uwezo wa kujitolea.