Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songea Mjini

Primary Question

MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO (K.n.y. MHE. PROSPER J. MBENA) aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kutoka Bigwa – Mvuha – Kisaki katika Wilaya ya Morogoro Vijijini kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kutokana na umuhimu wa barabara hii ambao unatupeleka kwenye Stiegler’s Gorge na kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Pwani katika maeneo ya Kibiti, je, ni lini barabara hiyo itakamilika kwa kiwango cha lami ili masuala ya kiuchumi ya Stiegler’s Gorge, kilimo na utalii yaweze kunufaika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tatizo hilo linafanana na tatizo lililopo la kuunganisha kati ya Wilaya ya Malinyi Mkoa wa Morogoro na Namtumbo Mkoa wa Ruvuma. Je, ni lini barabara hiyo inayounganisha Malinyi, Kilosa Mpepo, Londo mpaka Lumecha itaweza kujengwa angalau ipitike kwa kiwango cha changarawe kwa sababu sasa hivi haipitiki kabisa? (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaona umuhimu wa kutengeneza barabara hizi ambazo zinaelekea eneo hili la Stiegler’s Gorge kwa kutokea Kibiti hali kadhalika ile barabara inayotokea upande wa Morogoro kama nilivyojibu katika swali la msingi. Mheshimiwa Mbunge atakumbuka pia katika mwaka wa fedha kuna kiasi cha shilingi bilioni 5 zilitengwa na kupitishwa na Bunge kwa ajili ya kuboresha barabara hii kutoka Kibiti kuelekea sehemu ya Stiegler’s Gorge.
Mheshimiwa Spika, jambo kubwa niseme kama Serikali tumejipanga kwanza kuhakikisha barabara hii inapitika ili iweze kutoa huduma kwa shughuli ambazo zitakuwa zinaendelea kufanyika katika eneo hili. Ule utaratibu wa kujenga katika kiwango cha lami utafanyika katika siku za usoni.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, barabara inayotoka upande wa Malinyi, Kilosa kwa Mpepo kwenda Lumecha kule Namtumbo ukitokea Ifakara (km 499) usanifu ulishakamilika, Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kujenga barabara hii. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira pindi fedha zitakapopatikana barabara hii muhimu itaanza kujengwa. Hata hivyo, kuhusu kuboresha barabara hii ipitike Mheshimiwa Mbunge anafahamu yako maeneo ambayo ni hatari, yana milima mikali, tunajipanga ili kuhakikisha kwamba tunafungua barabara hii ili iweze kupitika muda wote kabla hatujaijenga kwa kiwango cha lami.

Name

Christopher Kajoro Chizza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Primary Question

MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO (K.n.y. MHE. PROSPER J. MBENA) aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kutoka Bigwa – Mvuha – Kisaki katika Wilaya ya Morogoro Vijijini kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 2

MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, kwanza niruhusu niipongeze Serikali kwa siku za karibuni imeongeza kiwango cha usimamizi wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Nyakanazi kuelekea mpaka Kabingo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa barabara hiyo inajengwa na inaishia katika kijiji cha Kabingo; na kwa kuwa kipande cha kutoka Kabingo kwenda mpaka Kibondo, Kasulu hadi Kidahwe bado ni vumbi. Je, kwa muendelezo huohuo ambao Serikali imetuonyesha, ina mpango gani sasa kipande cha kutoka Kabingo kwenda Kibondo, Kasulu mpaka Kidahwe kiweze kutekelezwa ili Mkoa wa Kigoma uweze kufunguka? (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Chiza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Chiza kwa kuchaguliwa na wananchi wa Buyungu kuwa Mbunge na Mwakilishi wao na namkaribisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utaratibu wa kujenga barabara katika Mkoa wa Kigoma. Nafahamu na Mheshimiwa Chiza anafahamu pia kwamba barabara ya kutoka Nyakanazi kuja eneo lake ujenzi unaendelea, lakini utaratibu ule wa manunuzi unafanyika na hivi karibuni kilomita karibu 87 hivi zitaanza kujengwa zikipita katika eneo hili la Kabingo kama alivyolitaja. Pia kilomita zote 300, Serikali iko katika hatua nzuri ya kujenga kwa maana ya kutoka sasa upande wa Kakonko, Kibondo kwenda Kasulu na viunga vyake vinavyoenda kuunganisha nchi ya Burundi kwa maana ya Manyovu na kipande kile cha Mabamba.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatua iliyofikiwa ni nzuri na kwa vile Mheshimiwa Mbunge yupo nafikiri itakuwa ni vizuri sasa tuzungumze ili angalau nikupe picha ili uweze kuona na kutimiza wajibu wako kama Mbunge wakati ukiwawakilisha wananchi wako kwamba Serikali imejipanga vizuri kujenga barabara hizi.