Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Omary Ahmad Badwel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Primary Question

MHE. OMARY A. BADWEL (K.n.y. MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE) aliuliza:- Je, ni lini barabara ya kutoka Mpunguzi kupitia Nagula, Mpwajungu, Ituzi hadi Ilangali itapandishwa hadhi kuwa ya Mkoa ambayo itasimamiwa na Mkoa kwa maana ya TANROADS?

Supplementary Question 1

MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza kwa kuwa Serikali imeunda chombo kinaitwa TARURA na wakati huo kabla ya kuunda TARURA barabara zilizokuwa zinahudumiwa na Halmashauri ikaonekana utekelezaji wake si bora. Kwa kuwa tayari Serikali imeunda chombo hiki TARURA na lengo lake lilikuwa ni kuzifanya hizi barabara za mijini na vijijini kufikia hadhi kama hii ambayo tunaiomba kupandishwa hadhi kwa barabara. Je, nataka kujua bado kuna haja ya kuendelea kuomba kupandishwa hadhi barabara zetu au TARARU ielekezwe kuchukua nafasi ya kutengeneza barabara hizi vizuri kama ilivyokuwa inatengeneza TANROADS? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imeunda chombo hiki kwa ajili ya kuboresha hizi barabara lakini bado kuna tofauti ya TARURA na TANROADS kwa maana ya asilimia ya fedha wanazopewa na Serikali ambapo TANROADS wanapata asilimia 70 na TARURA wanapata asilimia 30. Je, ni lini sasa Serikali itazigawia sawa kwa sawa taasisi hizi mbili kwa maana ya TARURA wapate asilimia 50 na TANROADS wapate asilimia 50 ili utengenezaji wa barabara hizi uwe katika kiwango kinachokusudiwa? (Makofi)

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Badwel, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na kilio cha Waheshimiwa Wabunge kutaka barabara zao zipandishwe hadhi ili ziweze kuhudumiwa na TANROAD. Pia ni ukweli usiopingika kwamba tangu tumeanzisha chombo hiki cha TARURA ambacho kimsingi kinafanya kazi nzuri, kuna umuhimu wa kutathmini kama iko haja ya kutaka kupandishwa tena barabara hizi. Naamini kinachotakiwa ni kuhakikisha kwamba barabara hizi zinajengwa kwa viwango ili zilingane na zile ambazo zinazojengwa na TANROADS.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusu mgawanyo, iko haja lakini ni vizuri pia tukazingatia kwamba barabara nyingi ambazo zinajengwa na TANROADS zinajengwa kwa kiwango cha lami na barabara ambazo zinazojengwa kwa kiwango cha lami zinauhitaji mkubwa wa fedha ukilinganishwa na ambazo nyingi zinajengwa kwa changarawe na udongo. Kwa hiyo, ukifika wakati ambapo haja ikawepo kwamba tugawanye 50 kwa 50, naamini kwa mujibu wa taratibu zitakazofuatwa na Bunge lako likiidhinisha kwa mujibu wa sheria tutafika huko kwa siku za usoni.