Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Saed Ahmed Kubenea

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Ubungo

Primary Question

MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:- Serikali katika Bunge la Kumi iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ambayo ilidhihirika kuwa na upungufu na baadhi ya wadau waliona kuwa kama sheria ikipita inaweza kuifanya nchi kuwa adui wa matumizi ya mtandao wa teknolojia ya habari na mawasiliano na sheria hiyo sasa inawaathiri watumiaji wa mitandao, kompyuta, simu za mikononi, saa, televisheni na vifaa vingine vinavyofanana na hivyo:- Je, ni lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa kuifanyia Marekebisho Sheria hiyo inayobana uhuru wa mwananchi wa kupata habari?

Supplementary Question 1

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika Kesi Na. 9 iliyofunguliwa na Jebra Kambone katika Mahakama Kuu ya Tanzania iliyokuwa ina-challenge baadhi ya vifungu vya sheria hii, Mahakama Kuu ilisema kifungu Na. 50 kinachozungumzia nguvu ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kuunganisha makosa na kumpa mtu haki ya kukiri mbele yake inakiuka Katiba na hadi sasa sheria hiyo haijafanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kesi iliyofunguliwa na Jamii Forum, pia Mahakama ilisema sheria hii inatafsiriwa vibaya na Jeshi la Polisi. Swali la kwanza, je, kwa maelezo hayo ya Mahakama, Serikali haioni kwamba kuendelea na sheria hii ni kukiuka Katiba ambayo yenyewe imeapa kuulinda na kuitetea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sheria hii imeleta mgogoro mkubwa na malalamiko mengi ndani na nje ya nchi wakiwemo nchi wahisani. Kwa nini Serikali inatafuta ugomvi mwingine na makundi mengine ambayo inaweza kuepukana nayo? (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Kubenea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge akubaliane nami kwamba sheria hii imesaidia sana na imetatua matatizo mengi. Kama zilivyo sheria nyingine, upo utaratibu wa kufanya marekebisho. Lazima Serikali ipitie hatua kadhaa kabla haijaleta marekebisho Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kujibu swali lake, niseme tu kwamba hizi kesi ambazo amezitaja ni mahsusi na yumkini inaweza ikasaidia pia kufanya marekebisho. Kwa hiyo, tunaichukua tu kama ni kitu ambacho lazima tupitie kama Serikali kwa maana ya kutazama mbele ya safari. Ni kawaida sheria ambazo zipo kufanyiwa marekebisho mbalimbali. Kama ilivyozoeleka, zipo sheria nyingi kila wakati inapohitajika, kwa sababu sheria siyo static, inavyotazamwa na marekebisho yataweza kuja kwenye Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili aliposema ni kwamba yapo malalamiko ambayo yanaweza yakaleta ugomvi. Niseme kwamba siyo kweli kwa sababu sisi ni kama Taifa na kama nchi, lazima tuangalie taratibu zetu. Ni lazima tuhakikishe kwamba sheria tulizonazo wa kwanza kunufaika nazo ni wananchi wenyewe na Taifa. Kwa hiyo, hili ni suala la kulitazama tu kwa upana wake, lakini hatuwezi kwenda kutunga sheria kwa kufuata shiniko la mtu, tutatunga sheria ili kuleta haki kwa wananchi na Tanzania kwa ujumla.

Name

Joseph Osmund Mbilinyi

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbeya Mjini

Primary Question

MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:- Serikali katika Bunge la Kumi iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ambayo ilidhihirika kuwa na upungufu na baadhi ya wadau waliona kuwa kama sheria ikipita inaweza kuifanya nchi kuwa adui wa matumizi ya mtandao wa teknolojia ya habari na mawasiliano na sheria hiyo sasa inawaathiri watumiaji wa mitandao, kompyuta, simu za mikononi, saa, televisheni na vifaa vingine vinavyofanana na hivyo:- Je, ni lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa kuifanyia Marekebisho Sheria hiyo inayobana uhuru wa mwananchi wa kupata habari?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Niwatakie mfungo mwema ndugu zangu Waislam ndani ya Bunge na nchi nzima. Kwa wale ambao ni viongozi watumie Mwezi huu Mtukufu kujitathmini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii pamoja na sheria nyingine mbovu za habari, siyo tu zinabana wananchi kupata habari, bali zinatumika pia kufunga watu jela ovyo kisiasa. Mfano, mimi nilifungwa kwa kujadiliana na wananchi wangu taarifa za watu kupigwa risasi, watu kutekwa, maiti kuokotwa kwenye viroba, watu kutokuwa na uhuru wa kuongea na kadhalika…
Kitu ambacho siyo mimi tu niliyejadili, kwa sababu kilishajadiliwa ndani ya Bunge hili na pia Maaskofu wa Katoliki pamoja…
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, ni lini sheria hizi zitafutwa ili kulinda Katiba ya nchi hususani Ibara ya 18? (Makofi). Maslahi mapana ya demokrasia nchini. (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sugu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii nimkaribishe Mheshimiwa Sugu hapa kwenye Jumba, karibu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake linasema kwamba zipo sheria ambazo wakati mwingine zinatakiwa kutazamwa. Kama nilivyojibu kwenye swali la nyongeza lililotangulia ni kwamba sheria zote, siyo hiyo sheria moja, Serikali inayo mechanism ya kuzitazama wakati wowote. Kama kuna maeneo ambayo yanahitaji marekebisho au kuunganisha sheria au kuiondoa, ni Bunge hili linapata nafasi hiyo ya kufanya hivyo. Kwa hiyo, labda kama kuna eneo mahsusi Mheshimiwa Sugu kwa sababu umekuja, tuonane ili nami nipate kwa upana unachokizungumza, halafu baadaye sisi kama Serikali tutatazama kwa nia nzuri ya kuweza kufanya sheria iwe bora zaidi.