Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Ali Abdallah

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tumbe

Primary Question

MHE. RASHID ALI ABDALLAH aliuliza:- Ni jambo la kusikitisha sana kwa wananchi wanaosumbuliwa na saratani kuchelewa kupatiwa huduma katika Hospitali ya Ocean Road:- Je, Serikali inalifahamu jambo hilo na inachukua hatua gani dhidi ya tatizo hilo?

Supplementary Question 1

MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri, nitakuwa na maswali mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, makundi ya Watanzania ambao wapo Ocean Road kusubiri matibabu ya ugonjwa hatari wa saratani, wagonjwa hao, ukifika pale Ocean Road utatokwa na machozi. Daktari hawezi kufanya matibabu kama hajafanya planning baada ya kuwekewa x-ray. Kuna mashine ya C-Arm ambayo ni mbovu haifanyi kazi. Hiyo ndiyo ambayo inamfanya daktari aweze kujua mgonjwa huyu ameathiriwa kiasi gani.
Je, ni lini Wizara itachukua hatua za dharura na za muhimu kabisa kuweza kuhakikisha mashine hii inafanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wapo watumishi katika Kitengo cha Saratani mmoja anaitwa Christopher; huyu amehamishwa Temeke; na mwingine ni Sefue ambaye amehamishwa Hospitali ya Amana. Hao walikuwa ni wataalam wazuri, wamesomeshwa katika Kitengo cha Mionzi. Watu hawa wamehamishwa, wamepelekwa katika Hospitali ambazo hawafanyi kazi wanayotakiwa kwa mujibu wa taaluma yao! Ni lini Waziri anayehusika atalifuatilia suala hili ili hatua zinazostahili zichukuliwe?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza hatua za dharura. Serikali tayari imekwishachukua hatua za dharura kufanya matengenezo ya mashine anayoizungumzia. Kwa maana hiyo, hapa ninapozungumza hakuna mashine hata moja ambayo haifanyi kazi pale Ocean Road. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, Serikali kupitia agizo alilotoa Mheshimiwa Waziri wa Afya, mara ya kwanza tu alipoenda kujitambulisha kwenye Hospitali hii, imetenga shilingi bilioni nne kwa ajili ya kukamilisha ununuzi wa mashine ya LINAC (Linear Accelerator) pamoja na CT Simulator ambayo inapanga utaratibu wa matibabu ya saratani kwa wagonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi hivi shilingi bilioni 2.5 zimeahidiwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa ajili ya kuanza mchakato wa ununuzi wa mashine hizo. Hivyo, ile kero anayoizungumzia Mheshimiwa Rashid Ali Abdallah ya matibabu, tunaifahamu na Mheshimiwa Waziri alitoa machozi mara ya kwanza alipokuwa pale na ametoa maelekezo ambayo tunayatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu hawa watumishi waliohamishwa. Ni kweli walihamishwa, lakini walihamishwa kwa taratibu za kiutumishi, suala hilo tunalifahamu na tayari tumechukua taratibu za kuunda Kamati Maalum ambayo inachunguza kama walihamishwa kwa fitina ama walihamishwa kwa taratibu za kiutumishi ambazo zilifuatwa. Kwa maana hiyo, kama itabainika kuna matatizo yalijitokeza tutachukua hatua za kuwarudisha.
Hata hivyo, kuondoka kwao pale hakujaleta upungufu wowote wa matibabu katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road.