Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:- Ubakaji na udhalilishaji wa wanawake na watoto nchini bado ni tatizo kubwa:- Je, Serikali inasema nini katika kupambana na wanaume wanaodhalilisha wanawake na watoto?

Supplementary Question 1

MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana na yenye msingi, nampongeza sana. Hata hivyo, nina maswali yangu mawili ya nyongeza hapa. Swali la kwanza, kwa kuwa ubakaji umekithiri hapa nchini na hasa wanaume ndio chanzo kikuu cha masuala hayo; je, Serikali itachukua hatua gani za kimkakati ili wananchi watokwe na hofu na suala hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali ina mpango gani wa kutunga sheria kali ili kudhibiti ubakaji na udhalilishaji? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeeleza mikakati ambayo Serikali inaifanya kuhakikisha kwamba tunapunguza sana matukio haya ya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto na mikakati naomba niirudie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni kuuhakikisha kwamba mpango mkakati ule ambao tumeuandaa tunausimamia vizuri; Pili, tumeendelea kushirikiana na vyombo vya dola na kuanzisha madawati mbalimbali; Tatu, kuanzisha one stop centre; Nne, ni kutoa elimu kwenye jamii. Tunatambua kwamba matukio mengi ya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto yanafanya karibu sana na wanafamilia. Niendelee kutoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba tusifumbie macho matukio kama haya na tusimalizane nayo katika ngazi ya familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, linahusiana na kwa nini tusitunge sheria kali; sheria tulizokuwa nazo za mwenendo wa adhabu na Sheria ya Mtoto na Sheria ya Masuala ya Kujamiiana zinajitosheleza kabisa na hatua zilizokuwepo pale zinatosha kabisa kuchukua hatua kwa wale wote ambao wanafanya matukio kama haya.

Name

Dr. Immaculate Sware Semesi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:- Ubakaji na udhalilishaji wa wanawake na watoto nchini bado ni tatizo kubwa:- Je, Serikali inasema nini katika kupambana na wanaume wanaodhalilisha wanawake na watoto?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Watanzania wanawake watatu kati ya kumi na mwanaume mmoja kati ya kumi wamekuwa waki-experience hii kunyanyaswa kijinsia, kikatili (sexual abuse). Idadi hii inaweza ikawa kubwa zaidi kwa sababu moja, watu wengi hawatoi taarifa, sasa Serikali imekuja na mikakati mbalimbali ya kurekebisha hili, lakini tatizo sugu ni kwamba taarifa hazifiki kwenye mamlaka husika. Sasa Serikali itakuja lini na mkakati mahususi wa kuhakikisha kwamba taarifa zinapelekwa kwenye mamlaka husika ili tatizo hili lipate ufumbuzi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ukiangalia kabla hatujazindua mpango mkakati tulikuwa tuna changamoto ya utoaji wa taarifa. Kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, matukio kama haya yalikuwa yanafanywa na watu wako karibu sana na familia. Sasa ukiangalia takwimu zetu kuanzia baada ya kuzindua mpango mkakati wetu, utoaji wa taarifa wa matukio umezidi kuongezeka. Hili linaweza likamaanisha mambo mawili; moja, matukio yanaongezeka, lakini pili, linaweza likawa linamaanisha kwamba utoaji wa taarifa umeongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kutoa rai kwa jamii kwamba vyombo vya dola viko imara na tunashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi. Pia nitoe rai kwa wananchi kwamba badala ya kumalizana na masuala haya ya udhalilishaji wa kijinsia majumbani, twende kwenye vyombo vya dola ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.