Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Mradi wa machinjio ya kisasa wa Ngerewara uliopo Manispaa ya Iringa umekuwa ni wa muda mrefu sana toka umeanza. Je, ni lini Serikali italeta fedha za kutosha ili kumaliza mradi huo?

Supplementary Question 1

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza nianze kumshukuru Waziri kwa majibu yake, lakini naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa huu mradi ni muhimu sana na una tija sana katika manispaa yetu na ni mradi ambao kwa kweli toka mwaka 2008 umeanzishwa na ni chanzo kizuri sana cha mapato kama ambavyo amesema kwenye jibu lake. Pia tulikuwa tunategemea kwamba kama ungekamilika, ungeweza kutoa ajira zaidi ya 200 katika Manispaa na katika Mkoa mzima wa Iringa. Katika majibu yake, Serikali bado haijatoa commitment ya mradi huu kwa sababu tulikuwa tunategemea kwamba kama mradi huu ungekamilika kwa wakati…
Je, hiyo pesa ambayo inahitajika katika mradi huu Serikali inaji-commit vipi maana ni mradi ambao tunategemea kwamba utaweza kusaidia hata miradi mingine katika manispaa yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba kwanza nimpongeze Balozi wa Comoro, Mheshimiwa Mabumba kwa sababu aliweza kuwaalika wafugaji wanaotoka Tanzania kwenda kuona fursa zilizoko katika nchi ya Comoro na kwa kweli tuliona kuna soko kubwa sana la nyama, ng’ombe na la mbuzi. Je, Serikali sasa inawasaidiaje wafugaji kuunganishwa na masoko hayo katika nchi hiyo ya Comoro au nchi nyingine ili iweze kuleta tija katika nchi yetu? (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza amezungumzia juu ya commitment ya Serikali katika kuhakikisha kwamba mradi huu wa machinjio ya Manispaa ya Iringa unaweza kupata pesa na hatimaye unakuwa ni chanzo cha mapato cha Halmashauri na kuzalisha ajira. Nimpongeze sana Mheshimiwa Ritta Kabati kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya watu wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yeye mwenyewe Mheshimiwa Ritta Kabati unafuatilia vizuri ataona kwamba hivi sasa Serikali imekuwa ikifanya miradi ya kielelezo ya kusaidia Halmashauri zetu ziweze kujizalishia kipato chao wao wenyewe. Nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa aliyokwishaianza kwa ajili ya Maispaa za Mkoa wa Dar es Salaam na kwingineko katika Taifa letu. Zimetolewa pesa nyingi kwa ajili ya miradi ya kielelezo ikiwemo ya machinjio kama machinjio ya Vingunguti imepata pesa nyingi ili iweze kufanya vizuri na kuwa na tija. Nina imani kwamba baada ya kumaliza Dar es Salaam vilevile Serikali inaweza ikafanya kazi ya kuelekea katika maeneo mengine ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ameuliza juu ya namna sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tulivyojipanga katika kuhakikisha wafugaji wetu wanapata masoko. Kama Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine watakuwa wafuatiliaji wazuri wataona kazi kubwa tunayoifanya. Katika kuhakikisha tunatangaza mifugo yetu na tunapata soko nje sisi katika Wizara tuna Idara inayoitwa Idara ya Huduma za Mifugo na Masoko na tunayo Bodi ya Nyama ambayo kazi yake ni kutafuta masoko nje ya nchi na kuitangaza nyama yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, tunatoa ushauri na kuangalia ubora wa nyama yetu ili iweze kupata masoko nje. Kusema ukweli hivi sasa tumekuwa tukipata masoko makubwa sana. Katika mwaka wa 2004 tulikuwa tunauza tani zisizozidi tatu, mwaka wa 2016/2017 tumeuza zaidi ya tani 1,000 za nyama nje ya nchi kutoka Tanzania. Mkakati wetu ni kuhakikisha tusiingize nyama ndani ya Taifa letu, badala yake sisi tuwe na uwezo wa kutoa nyama nje ya nchi. Kwa hiyo, tunaomba Waheshimiwa Wabunge, watuunge mkono kuhakikisha jambo hili kama Wizara tunaendelea nalo na tunaweza kufanikisha ajenda yetu ya Tanzania ya Viwanda hasa ile inayohusu mazao yetu ya nyama na samaki.

Name

Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Primary Question

MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Mradi wa machinjio ya kisasa wa Ngerewara uliopo Manispaa ya Iringa umekuwa ni wa muda mrefu sana toka umeanza. Je, ni lini Serikali italeta fedha za kutosha ili kumaliza mradi huo?

Supplementary Question 2

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Kibiti ina mifugo mingi ya ng’ombe. Je, Serikali ina mpango gani wa kuijengea machinjio ya kisasa, malambo na majosho ili kuondoa migogoro baina ya wakulima na wafugaji? (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba Halmashauri ya Kibiti ina mifugo mingi sasa, ni ukweli mifugo mingi imehamia katika Mkoa wetu wa Pwani, Wilaya za Mkuranga, Kibiti, Rufiji, Kisarawe zimepata mifugo mingi sana mara baada ya Serikali kukubaliana kuhamishia mifugo kutoka katika Bonde la Ihefu na kuhamia katika Mikoa ya Kusini na sisi tumepata neema hiyo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Ungando, kwa namna ambavyo tumejipanga katika Wizara ya Mifugo, tunataka tuhakikishe mfugo hii iende kuwa ni fursa kubwa sana kwetu sisi watu wa Mkoa wa Pwani. Ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha wa 2018/2019 ambao bajeti yake tunakwenda kuisoma hapa karibuni ataona haya aliyoyauliza ikiwemo ya malambo na majosho, yatakwenda pale katika maeneo yetu ya Wilaya za Mkuranga, Rufiji na Kibiti, ni kwa sababu ya wingi wa mifugo tuliyokuwa nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tuna mifugo mingi sana na mkakati pia ni kuhakikisha tunapata eneo la uchinjaji na ku-process nyama. Hii ni kwa sababu pia tuna advantage kubwa ya kuwa karibu na soko la hiyo nyama yenyewe maana nyama kuitoa Kibiti, Rufiji, Mkuranga ama Kisarawe ni rahisi zaidi kuipeleka Dar es Salaam kuliko eneo lingine katika nchi.

Name

Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Mradi wa machinjio ya kisasa wa Ngerewara uliopo Manispaa ya Iringa umekuwa ni wa muda mrefu sana toka umeanza. Je, ni lini Serikali italeta fedha za kutosha ili kumaliza mradi huo?

Supplementary Question 3

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba na mimi nimuulize Mheshimiwa Naibu swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyeiti, kwa kuwa machinjio ya Mazizini ni machafu sana na mazingira yake yako tete na yanahatarisha hata maisha ya watumiaji na Halmashauri pia haipati mapato kutokana na machinjio hayo. Je, Serikali ina mikakati gani kuboresha machinjio haya ya Mazizini ili na Halmashauri nayo ipate kipato?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba naomba tu nijibu kwa ujumla kwa sababu sijafahamu kwamba hayo machinjio ya Mazizini anazungumzia Halmashauri gani, lakini naomba nimhakikishie kwamba Wizara yetu imeendelea kuhakikisha kwamba machinjio yote yawe safi. Ndiyo maana sasa hivi tuna operation maalum ya ukaguzi ya kuhakikisha tunaweka utaratibu mzuri wa tasnia nzima ya mifugo ya nyama kuanzia katika machinjio na hata huko katika minada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tumekuwa tukilifanyia usimamizi wa karibu kabisa ili tuweze kupata ithibati ya nyama yetu kwa sababu biashara hii ya nyama haiishii kwetu sisi wenyewe, ni sheria za kimataifa zinazoongozwa na Shirika la Kimataifa la Mifugo (OIE). Kwa hiyo, tunasimamia vizuri na nataka nimhakikishie tutafika Mazizini na kuhakikisha ya kwamba machinjio yale yanakuwa ya viwango kwa maana ya usafi ili nyama yetu inayotoka pale iweze kuwa bora wa mlaji.

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Primary Question

MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Mradi wa machinjio ya kisasa wa Ngerewara uliopo Manispaa ya Iringa umekuwa ni wa muda mrefu sana toka umeanza. Je, ni lini Serikali italeta fedha za kutosha ili kumaliza mradi huo?

Supplementary Question 4

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Longido katika harakati za kujiongezea mapato ya ndani ya kuinua kipato cha wananchi wake walijenga mnada wa mifugo katika Kata ya Kimokouwa inayopakana na Kata ya Namanga iliyoko mpakani mwa Kenya na Tanzania ili pia kuwatengenezea wachuuzi wa mifugo mazingira rafiki ya kuweza kufanya biashara ya mipakani (cross border trade) na kwa kuwa baada ya Halmashauri kumaliza mnada ule wakaanza kuhamasisha wananchi waliokuwa wanapitisha ng’ombe maporini kupeleka kuuza katika minada ya Kenya ambayo ndiyo inayutumika katika maeneo ya Longido, jana Waziri akaenda akatoa maagizo ya kuwapangia bei ya kulitumia soko lile kitendo ambacho kimewakera wananchi…
Naomba Waziri mwenye dhamana aliyekwenda jana kutoa directives za bei ya mifugo atoe kauli itakayowafanya wananchi wa Longido na Halmashauri kuelewa kwamba soko hili ambalo wamejenga kwa nguvu zao wenyewe na wafadhili bila Wizara kuwekeza hata shilingi watatoa justification gani ya kwenda kulitwaa na kulipangia bei ambayo sio rafiki ni kandamizi, hii ni sawa na kuvuna usichopanda?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tasnia hii ya mifugo inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zake. Tunafahamu kwamba Longido kumejengwa mnada kupitia miradi ya Serikali kupitia ule Mradi wa MIVAF unaosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnada ule kimkakati uko mpakani na sisi katika tasnia hii ya mifugo kama Taifa kwa mwaka mmoja kwa tathmini tuliyoifanya ng’ombe 1,600,000 wanatoroshwa kwenda nje ya nchi. Pia tunapoteza jumla ya shilingi 263,000,000,000 kama Taifa ikiwa ni mapato yetu yanayotokana na tasnia hii ya mifugo hasa export royalty.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie Mheshimiwa Kiruswa kwa sababu nafahamu kwamba ni Mbunge makini na ana timu makini iliyoko kule ya DC na Mtendaji kwa maana ya Mkurugenzi, watupe ushirikiano. Hatufanyi jambo hili kwa ajili ya kuwakomoa, tunafanya jambo hili kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za nchi yetu lakini tunafanya jambo hili kwa ajili ya kuhakikisha Taifa letu linanufaika na rasilimali zake. Ahsante sana.