Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Wilaya ya Lushoto haina Chuo cha Ufundi (VETA) na kuna vijana wengi waliohitimu elimu ya msingi na sekondari:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Chuo cha Ufundi (VETA) ili vijana hao waweze kupata elimu ya ufundi ya kuwasaidia katika kujiajiri?

Supplementary Question 1

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Chuo cha VETA kiko mbali sana na Wilaya ya Lushoto na hii imesababisha vijana wengi wa Lushoto kukosa fursa ya kujiajiri na kuajiriwa, je, Serikali haioni kwamba imefikia wakati sasa kuchukua hatua za haraka ili kuwajengea chuo hicho vijana wa Lushoto waweze kupata elimu hiyo ya ufundi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali pili, kwa kuwa kuna majengo ya TBA na majengo yale yana karakana ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto. Je, Serikali haioni sasa kuwa kuna haja ya kurudisha majengo hayo katika Wizara ya Elimu kwa nia ya kufungua Chuo cha VETA katika majengo hayo ili vijana wa Lushoto waliokosa elimu hiyo ya ufundi kwa muda mrefu waweze kuipata sasa? (Makofi)

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni lini Serikali itajenga Chuo cha Ufundi Stadi Lushoto, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, Serikali itaendelea kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi katika wilaya na mikoa yote kadri fedha zitakavyopatikana. Kwa hiyo, kwa sasa nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zikipatikana Serikali itajenga Chuo cha Ufundi Lushoto kama itakavyofanya katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu majengo ya TBA kama ni wakati sasa wa kurudishwa Wizara ya Elimu ili yaweze kutumiwa kama Chuo cha VETA, naomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba hili linawezekana lakini wao waanzishe mchakato katika ngazi yao ya halmashauri, wawasiliane na TBA. Wakishapata yale majengo kwa maana ya wakiruhusiwa, sisi Wizara ya Elimu tuko tayari kuja kuyakagua na kuangalia kama yanafaa kuwa VETA na hatimaye tukiona yanafaa hatuna kipingamizi, tutahakikisha kwamba majengo yale yanageuzwa kuwa VETA.