Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Innocent Sebba Bilakwate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyerwa

Primary Question

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:- Serikali imezuia biashara ya BUTURA na wanunuzi wa kahawa kwa watu binafsi (moja kwa moja kwa wakulima) na kuagiza yote iuzwe kwa Vyama vya Msingi wakati vyama kama KDCU vilishindwa kuwapa bei nzuri wakulima:- • Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha inakuja na mbinu mpya ya kuwapa bei nzuri wakulima wa kahawa? • Je, ni hatua zipi zimechukuliwa haraka ili kuhakikisha wale walioua Vyama vya Ushirika wanashtakiwa?

Supplementary Question 1

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Naipongeza Serikali kwa jitihada zake kuhakikisha inaboresha zao la kahawa.
Mheshimiwa Spika, kwenye zao la kahawa kulikuwa na kodi nyingi na Serikali imejitahidi kuondoa kodi 17, lakini hizi kodi hazimnufaishi mkulima moja kwa moja zinawalenga wafanyabiasha. Je, Serikali imejipanga vipi kuondoa hizi kodi ambazo zinamgusa moja kwa moja mkulima ili aweze kupata bei nzuri ya kahawa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mara nyingi mkulima anapoanza kulima, kupalilia mpaka kuvuna hasaidiwi kitu chochote, mwisho anaanza kukatwa kodi na mambo mengine. Je, Serikali imejipanga vipi kumsaidia huyu mkulima ili iweke miundombinu mizuri kuanzia anapolima akiwa shambani mpaka kwenye mnada? (Makofi)

Name

Dr. Mary Machuche Mwanjelwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo anafuatilia kwa ukaribu sana zao hili la kahawa ambalo linalimwa pia kwa wingi katika Jimbo lake lile la Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye maswali yake mawili ya nyongeza, katika swali lake la kwanza, ni kweli kwamba Serikali tumeliona hili na ndiyo maana tumeanzisha ule utaratibu wa kuuza kahawa mnadani moja kwa moja kupitia Vyama vyetu vya Ushirika. Vilevile Serikali tumepunguza tozo ya mauzo ya mazao kupitia cess au farm gate price kutoka asilimia 5 hadi asilimia 3.
Mheshimiwa Spika, swali lake lile la pili ni kwamba zao la kahawa linategemea sana na muonjo ule wa kahawa. Kwa maana hiyo, katika kuweka ubora wa miundombinu pia na ubora wa zao lenyewe, ni kwamba kulekule shambani wakulima wanapaswa kutumia zile CPU kwa ajili ya kuchakata zile kahawa kwa sababu kahawa mbichi hairuhusiwi, hivyo iweze kuanikwa na kusafishwa vizuri, kabla haijapelekwa kukobolewa kule kwenye curing.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)