Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Shukuru Jumanne Kawambwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Primary Question

MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:- Upanuzi wa barabara kutoka mita 22.5 hadi 30 kutoka katikati ya barabara umesababisha baadhi ya wananchi katika Kitongoji cha Sanzale, Kata ya Magomeni kufuatwa na barabara na nyumba zao kuwekwa X:- Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hao?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, pamoja na shukrani kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu hayo ambayo amenipa.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, eneo lile la Kitongoji cha Sanzale ni Bagamoyo Mjini na wananchi hawa wamewekewa alama za “X” miaka nane imepita, hawawezi kukarabati nyumba zao, hawawezi kujenga upya, hawawezi kufanya chochote na majibu ni kwamba watafidiwa pale maeneo yatakapohitajika. Je, ni lini maeneo hayo yatahitajika kwa sababu wananchi hawa psychologically wameendelea kupata matatizo makubwa sana? Wafanye nini maana wanaishi na watoto wao katika nyumba ambazo zimewekewa “X” lakini hawajui lini watalipwa fidia.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika barabara ya Makofia - Mlandizi ambayo imo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 pia katika Ilani ya mwaka 2015 kujengwa kwa kiwango cha lami. Wananchi hawa wanapenda kujua fidia zao zitalipwa lini?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASLIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kawambwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Kawambwa kwa kufuatilia sana maendeleo ya Bagamoyo kwa ujumla wake. Natambua kwamba kutakuwa na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na hivyo hizi barabara ambazo Mheshimiwa Mbunge anazitaja ni muhimu kweli. Yeye mwenyewe anatambua kwamba zipo harakati za awali ambazo zimefanyika ili kuhakikisha kwamba fidia kwa wananchi wake zinalipwa mapema.
Mheshimiwa Spika, swali lake anasema ni lini sasa tutalipa fidia hiyo. Niseme kwamba harakati za ujenzi wa barabara ya lami kwa barabara ambazo zinaingia Bagamoyo zinaendelea na hatua za tathmini zimeshafanyika na kwa vile zina hatua mbalimbali, kwa upande wa TANROADS tumeshafanya jukumu letu na tunaendelea kuwasiliana ili kuweza kupata fedha ili wakati wowote tuweze kuwalipa wananchi hawa.
Mheshimiwa Spika, najua kwa eneo hili amelitaja mahsusi Mheshimiwa Mbunge, wapo wakazi wasiozidi 20 ambao wanahitaji kufanyiwa malipo ya compensation. Kwa hiyo, nikuombe tu Mheshimiwa Mbunge na Ndugu zangu wananchi wa Bagamoyo eneo hili wavute subira wakati wowote tutafanya zoezi la kuweza kuwalipa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anauliza juu ya compesation kwenye barabara hii inayotoka maeneo ya Mlandizi kuja Bagamoyo. Kama nilivyosema barabara hii ni muhimu sana kwa ajili ya kuja kutoa huduma katika Bandari ya Bagamoyo itakapojengwa hii ikiwa ni pamoja na eneo lingine kuja Bagamoyo ukitokea Kibaha, maeneo ya Vikawe kuja Mapinga na kwenyewe harakati zinaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, natambua Ilani ya mwaka 2010 ya Chama cha Mapinduzi na Ilani ya mwaka 2015 imetaja kupanua barabara hii. Kwa hatua ambazo tumefikia wananchi wameshapata valuation form wazijaze, wazirudishe halafu Serikali tutasimamia kwa haraka ili wananchi hawa pia waweze kulipwa kulingana na sheria inavyotaka.

Name

Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:- Upanuzi wa barabara kutoka mita 22.5 hadi 30 kutoka katikati ya barabara umesababisha baadhi ya wananchi katika Kitongoji cha Sanzale, Kata ya Magomeni kufuatwa na barabara na nyumba zao kuwekwa X:- Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hao?

Supplementary Question 2

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, majanga mengi sasa hivi yanasababishwa na binadamu zaidi ya asilimia 96 ikiwepo kwenda kinyume na uumbaji wa dunia ya Mwenyezi Mungu. Sheria hii ya tangu mwaka 1932 mpaka 2007 kwa kiasi kikubwa ni uharibifu mkubwa wa mazingira na hasa barabara za vijijini. International Standard na vigezo vyake vya ujenzi wa barabara huwezi uka-upgrade barabara kutoka stage moja kwenda stage nyingine za vijijini ukafanya mita 60.
Mheshimiwa Spika, barabara hizi zinazoenda vijijini, kwa mfano barabara ya Kawawa - Pakula, Jimbo la Vunjo na barabara ya Himo na Himo - Mwika, kwa nini mnaamua kuchukua mashamba bila fidia na siyo standard? Barabara zinajengwa kwenda juu na siyo kupanua tu kwa horizontally?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ELIAS KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbatia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, nitumie nafasi hii kulipongeza Bunge kwa kutunga Sheria hii Na.13 ya mwaka 2007 ambayo kwa kweli ilizingatia sana mabadiliko, ukiisoma Sheria ya mwaka 1932 utaona namna ilivyokuwa. Kwanza ilikuwa ni ndogo sana, ilikuwa na kama section saba tu na ilikuwa inatoa mamlaka makubwa sana kwa wale watekelezaji wa ujenzi wa barabara wanaweza wakafanya maamuzi, sheria iliyowaruhusu. Mabadiliko haya yaliyokuja mwaka 1969 na baadaye kuja hii Sheria Na.13 imetoa nafasi kwa Mamlaka zetu za Barabara kuweza kuzingatia maeneo maalum na kuweza kufanya declaration ya ujenzi wa barabara. Hivyo, sheria ipo vizuri ni vema tu tuendelee kuitekeleza.
Mheshimiwa Spika, nimueleze Mheshimiwa Mbatia niseme kwamba Serikali inalipa fidia kulingana na sheria zilizopo pia lazima tuangalie na mamlaka zetu katika halmashauri. Mamlaka za Barabara zipo kwenye Halmashauri zetu, kwa mfano, sasa hivi tunayo TARURA na TANROADS kwa upande wa Serikali Kuu.
Mheshimiwa Spika, ni muhimu tu tukatazama sheria zote, Sheria za Barabara pamoja na sheria za kusimamia mamlaka zetu ili wananchi waweze kupata haki. Kama jambo hili linaweza kuwa mahsusi Mheshimiwa Mbunge alilete tulizungumze tuone namna nzuri ya kulishughulikia lakini Serikali ina nia thabiti ya kuwalipa wananchi fidia kulingana na sheria zilizopo.