Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:- Serikali ina mamlaka ya kutwaa ardhi na kubadilisha matumizi na kwa kufanya hivyo, Serikali inawajibika kusimamia na kuhakikisha wananchi wanaopisha matumizi mapya ya ardhi wanalipwa fidia stahiki ikiwa ni pamoja na kuwapa maeneo mbadala ili kuweza kuendeleza shughuli zao:- Je, ni kwa nini Serikali imeshindwa kuwalipa fidia wananchi wa Kata za Nyamisangura na Nkende waliopo Halmashauri ya Mji wa Tarime ambao ardhi yao ilichukuliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu mwaka 2007?

Supplementary Question 1

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kweli majibu yaliyopatikana leo, ni dhahiri kabisa hata Serikali haijui mipaka ya Kata. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwa kinywa kwamba wanatwaa ardhi kwa kufuata Sheria ya mwaka 1999 na kwa kuwa JWTZ hawakufuata sheria, mwanzoni waliomba hifadhi ya miezi mitatu katika Kata ya Nkende, walivyopewa wakaamua kuhodhi na Kata ya Nyamisangura na Nkende na Nyamisangura, siyo eneo la Nyandoto. Kikosi cha Jeshi kinatakiwa kukaa Kata ya Nyandoto na siyo Nyamisangura na Nkende.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa sababu hawakufuata Sheria ya mwaka 1999, kama alivyotamka mwenyewe, haoni sasa kwamba ni dhahiri wananchi hawa wanatakiwa kuhodhi maeneo yao kama mlivyoyateka mwaka 2008 mpaka sasa hivi, mwaache waendeleze shughuli zao za kiuchumi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Waziri anasema kwamba wanaenda kukamilisha utathmini, ifahamike kwamba waliwazuia wananchi hawa kufanya shughuli za maendeleo kuanzia mwaka 2008, hawafanyi shughuli zozote za maendeleo. Sasa hiyo tathmini ambayo Waziri anakiri kwamba anaenda kuikamilisha mwaka huu, napenda kujua na wananchi wa Tarime wajue kwamba mtazingatia hali halisi ya mwaka 2007, ambapo Wanajeshi hao waliwakataza wananchi wasifanye shughuli zozote za maendeleo; nyumba zimebomoka, vyoo vimebomoka, mashamba yameshakuwa chakavu sasa hivi ni ardhi tu; huo utathmini ambao mnaenda kuufanya sasa hivi, unazingatia vigezo vipi? Ahsante.

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunakiri kwamba wananchi walizuiliwa kuendelea na shughuli za uchumi kwa sababu ya kuweka Kiteule cha Jeshi.
Napenda Mheshimiwa Mbunge aelewe kwamba amani na usalama katika eneo nalo ni muhimu kwa ajili ya shughuli za uchumi. Kwa hiyo, maelewano yalifanyika kwamba wananchi wapishe Jeshi hapo kwa ajili ya shughuli za usalama ili na wao waweze kupata fidia.
Kwa hiyo, hatua tuliyofikia ni nzuri naweza nikasema, kwa sababu sasa tunasema kwamba fedha za uthamini zimeshapatikana na zimeshatumwa kwenye Halmashauri. Ni jukumu la Halmashauri kukamilisha uthamini ili wananchi hao waweze kulipwa fidia inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu tathmini kuchukua viwango vya mwaka 2007 au sasa, kwa mtazamo ni kwamba viwango vya sasa vitakuwa vikubwa zaidi kuliko mwaka 2007.
Kwa hiyo, tunachosema tu ni kwamba, kwasababu uthamini huu unafanywa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya, ni vyema Mheshimiwa Mbunge ukashirikiana na Halmashuri yako pamoja na watendaji wa Wizara yangu ili kuweza kupata tathmini stahiki bila ya mtu yeyote kuonewa. Kama kweli kuna nyumba ambazo zilikuwepo ambazo zimebomoka, tutalizingatia hilo ili kila mtu aweze kupata fidia yake anayostahili.