Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. ESTER M. MMASI) aliuliza:- Baadhi ya vyuo vikuu nchini vimekuwa na utamaduni wa kutozingatia miongozo ya Serikali Kuu katika kuongoza na kusimamia vyuo vikuu nchini na hata kupeleka kupuuzwa kwa stahiki za wafanyakazi wa elimu ya juu kwa kisingizio cha elimu ya juu inajiongoza na kujisimamia yenyewe chini ya University Charter:- Je, ni nini kauli ya Serikali katika hili?

Supplementary Question 1

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, napenda kuiuliza Serikali, je, imepangaje kusaidia vyuo vikuu vijiendeshe kwa mujibu wa sheria za nchi lakini bila kuathiri uhuru wa utoaji wa taaluma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ubora wa elimu inayotolewa na vyuo vikuu vyetu imekuwa ni ya kutia mashaka na inashindwa kuwaandaa vijana kujiajiri lakini pia kushindana kimataifa. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuboresha mitaala ya elimu ya vyuo vikuu? (Makofi)

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaheshimu uhuru wa vyuo vikuu (academic freedom) na mara nyingi sana Serikali haitaingilia namna vyuo vikuu vinavyoendeshwa. Hata hivyo, uhuru huo lazima ufanyiwe kazi ndani ya sheria. Kwa hiyo, vyuo vyote vinatakiwa viwe na uhuru lakini uhuru wake uko kwenye mipaka ambayo imewekwa na sheria, kanuni na taratibu. Ndiyo maana chuo kikuu chochote, kiwe cha Serikali au binafsi ambacho hakifuati sheria, kanuni, taratibu na miongozo hatutasita kukichukulia hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili kwamba ni namna gani tunajaribu kuboresha quality ya elimu katika vyuo vikuu vyetu, jibu lake linafanana na hilo ambalo nimeshatoa kwamba Tume ya Vyuo Vikuu ambayo ndiyo hasa imepewa kazi ya kuhakikisha kwamba inadhibiti ubora wa elimu katika vyuo vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia itaendelea kuhakikisha kwamba taratibu zile zinafuatwa na ndiyo maana tunafanya tathmini ya kila mara na vyuo vikuu vile ambavyo havitakuwa vimefuata taratibu zile vitafungiwa. Ndiyo maana kwa mwaka huu vyuo 19 vimefungiwa na programu 75 za vyuo 22 zimesitishwa. Tunachosema tu ni kwamba ili tuweze kuwa na ubora unaotakiwa, tutaendelea kuchukua hatua ili elimu yetu iendelee kuwa bora.