Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:- Kukosekana kwa Madaktari Bingwa na wataalam wengine katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma kunafanya wagonjwa wengi kupewa rufaa ambazo zingeweza kushughulikiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa:- Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari Bingwa na wataalam wengine wa kutosha katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma?

Supplementary Question 1

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa maijibu mazuri, ametupa faraja watu wa Kigoma. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Hospitali hii ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni ni hospitali kubwa ukizingatia Kigoma tuko mpakani, inahudumia wananchi zaidi ya milioni mbili, lakini mpaka sasa hatuna vifaa muhimu kama CT-scan na vile vya kupimia saratani ya kizazi kwa wanawake. Naomba majibu ya Waziri, ni lini mtatuletea vifaa hivi katika hospitali hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mkoa wa Kigoma umekuwa ukikumbwa na changamoto nyingi za magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu hasa katika Wilaya yangu ya Kigoma Vijijini. Nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha wanamaliza tatizo la kipindupindu ndani ya Mkoa wa Kigoma? Ahsante.

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, S wali lake la kwanza ameuliza ni lini Serikali itapeleka mashine ya CT-scan na vipimo vya kupima saratani. Niseme tu kwamba kwa mujibu wa mpango wa Serikali na aina ya huduma ambazo zinatolewa, sasa hivi katika ngazi za Hospitali za Rufaa za Mikoa, hatuna mpango wa kuweka CT-scan kwa sababu, moja, mashine hizi kwanza ni za gharama kubwa lakini pili zinahitaji utaalam ambao kwa sasa hivi katika ngazi za rufaa za mikoa hatuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi katika mikakati yetu ni kwamba mashine za aina ya CT-scan upatikanaji wake unaanzia katika Hospitali za Rufaa za Kanda. Hata hivyo, vipimo kwa ajili ya dalili za awali za saratani ya shingo ya uzazi vyote vinapatikana hadi katika ngazi ya vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi ambao wanatusikiliza kwamba huduma hizi zinapatikana. Kwa wale wanawake ambao hatujawagusa katika chanjo hizi, huduma hizi tumezisogeza, zaidi ya vituo 1,000 ndani ya nchi hii vifaa hivi vinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili limehusiana na suala la kipindupindu. Ugonjwa wa kipindupindu ni mtambuka na sisi kama Wizara ya Afya ambao tunasimamia masuala yote ya afya, tunaendelea kushirikiana na mamlaka katika ngazi ya mkoa na halmashauri kuhakikisha kwamba mikakati yote ambayo sisi tumeiweka ya kutokomeza ugonjwa huu inatekelezwa kwa maana ya kutoa dawa, vipimo, kutibu maji na kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na ugonjwa wa kipindupindu.

Name

Abdulaziz Mohamed Abood

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Mjini

Primary Question

MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:- Kukosekana kwa Madaktari Bingwa na wataalam wengine katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma kunafanya wagonjwa wengi kupewa rufaa ambazo zingeweza kushughulikiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa:- Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari Bingwa na wataalam wengine wa kutosha katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma?

Supplementary Question 2

MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ipo katikati ya barabara za Iringa, Mbeya, Dodoma na ajali nyingi zinatokea lakini mpaka leo kuna matatizo ya X-ray machine. Je, ni lini Serikali itaipatia uwezo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro X-ray machine kwa sababu ajali nyingi huwa zinatokea katika barabara hizi? (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ni moja kati ya hospitali 10 ambazo tutazipatia mashine ya X-ray. Tunatarajia ifikapo mwezi Juni mwaka huu mashine hii itapatikana.

Name

Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Primary Question

MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:- Kukosekana kwa Madaktari Bingwa na wataalam wengine katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma kunafanya wagonjwa wengi kupewa rufaa ambazo zingeweza kushughulikiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa:- Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari Bingwa na wataalam wengine wa kutosha katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma?

Supplementary Question 3

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kukosekana kwa Madaktari Bingwa na wataalam wengine katika Hospitali ya Kigoma kunaakisi hali halisi ilivyo katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda ambayo inafanya kazi kama hospitali ya mkoa. Je, ni lini Serikali itatusaidia Madaktari na wataalam wengine?

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze amekuwa anafuatilia sana masuala kuhusiana na afya katika eneo lake la Mpanda. Pia nimhakikishie tu kwamba kadri Serikali itakapokuwa tunapata watumishi na tunatarajia mwezi Julai mwaka huu tutapata watumishi wengine wa ziada, Hospitali ya Mpanda ambayo na mimi nimeshaitembelea na natambua changamoto zake itakuwa ni moja ya hospitali zitakazopata watumishi. Sambasamba na hilo, Serikali imejielekeza sasa katika ujenzi wa hospitali mpya kubwa ya rufaa katika Mkoa wake wa Katavi.

Name

Susan Anselm Jerome Lyimo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:- Kukosekana kwa Madaktari Bingwa na wataalam wengine katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma kunafanya wagonjwa wengi kupewa rufaa ambazo zingeweza kushughulikiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa:- Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari Bingwa na wataalam wengine wa kutosha katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma?

Supplementary Question 4

MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wizara ya Afya haijaanza jana wala juzi. Nimesikitika sana kusikia Mheshimiwa Waziri akisema sasa ndiyo wanafanya tathmini ya kujua Madaktari Bingwa ni wangapi ili waweze kuwapanga. Swali langu, hawaoni huu ni uzembe mkubwa kwamba walipaswa kuwa na kanzidata au database ya Madaktari Bingwa ili kusiwe na tatizo hili kwa sababu kila siku tunauliza na tunaambiwa kuna tatizo? Hawaoni huo ni uzembe kwamba walipaswa kuwa nayo?

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Lyimo ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambao nao wanasimamia sekta hii ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa maana ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekabidhiwa hospitali hizi za rufaa za mikoa mwishoni mwa mwaka jana wakati wa uzinduzi wa Hospitali ya Mloganzila. Tunatambua idadi ya Madaktari tuliokuwa nao na tunakuwa na mikakati ya kuhakikisha kwamba tunapata watumishi wa afya wa kutosha. Kwa hiyo, si uzembe, kila kitu ni mikakati ambayo Serikali tumeendelea kujiwekea na tutaendelea kuzihudumia na kuwapatia watumishi wa kutosha kadri uwezo wa Serikali unavyoruhusu.