Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA (K.n.y. MHE. PHILIPO A. MULUGO) aliuliza:- Wilaya ya Songwe ina jumla ya vijiji 43 lakini mpaka sasa hakuna kijiji hata kimoja chenye umeme kwa mpango wa umeme wa REA toka awamu ya kwanza na ya pili:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inatoa upendeleo maalum kwa vijiji vya wilaya hii mpya katika awamu ya tatu ya REA?

Supplementary Question 1

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Wizara. Nikiri kweli kuwa wamefanya kazi nzuri ila katika haya majibu kuna Kijiji cha Mbuyuni bado hakijapata umeme pamoja na kuwa kimeorodheshwa kuwa kimo kwenye orodha ya vilivyopatiwa umeme.
Mheshimiwa Spika, tatizo lingine ni umeme uliokwenda Idunde umeruka Vijiji vya Rukwa na Kapalala; Je, ni lini Serikali itahakikisha hivi vijiji vilivyobaki vya Kapalala, Mbuyuni na Rukwa vitapatiwa umeme ikiwa ni pamoja na vijiji vya Kata ya Ikukwa ambayo ni karibu sana na Jimbo la Songwe navyo vitapatiwa umeme?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nakiri kuwa Serikali imefanya kazi nzuri ya kupeleka umeme vijijini, lakini kwa mazingira ya vijijini wanahitaji vilevile huduma kutoka TANESCO; Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa kutakuwa na huduma kwa wateja ambazo zitakuwa karibu huko vijijini ili waweze kupata huduma pamoja na hii huduma nzuri iliyofanyika kwa mpango wa REA? Mheshimiwa Spika, ahsante.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na namshukuru sana Mheshimiwa Njeza kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Nampongeza pia kwa kazi nzuri kwenye Jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, katika maswali yake la kwanza amejielekeza kwenye Kijiji cha Mbuyuni ambacho anasema kiko kwenye orodha ya vijiji vyenye umeme, lakini pia hakina umeme. Naomba hili nilichukue ili tuweze kufuatilia takwimu hii na nitampa majibu ya uhakika.
Mheshimiwa Spika, pia, katika swali lake hilo alielekeza vijiji ambavyo vimerukwa ikiwemo vijiji vya Kata ya Ikukwe. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi vijiji vyote vilivyosalia 7,873 nchi nzima vitapata miundombinu ya umeme kwa mizunguko. Mzunguko wa kwanza na mzunguko wa pili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, vile 3,559 vya mzunguko wa kwanza kazi inaendelea mpaka Julai, 2019 kisha tunaanza mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili. Kwa hiyo naomba nimthibitishe Mbunge maeneo ambayo yaliyosalia yatapatiwa miundombinu ya umeme kupitia REA awamu ya tatu mzunguko wa pili.
Mheshimiwa Spika, ameuliza suala la namna gani wananchi wa maeneo ya vijijini watapata huduma ya TANESCO. Naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kuwa, kazi ya kupeleka miundombinu ya umeme inahusu vijiji vyote na tunatambua baadhi ya vijiji viko mbali na ofisi zetu za TANESCO ambazo ziko kila Wilaya, tumeielekeza TANESCO kufungua ofisi ndogo ndogo kwenye miji mikubwa na miji ambayo iko karibu na maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuthibitishie hilo linafanyika na tumeshapokea orodha ya ofisi za TANESCO ndogondogo mpya ambazo zingine zitajengwa lakini pia tumeomba pale ambapo, maana yake ujenzi ni suala la muda mrefu, lakini pale ambapo kuna maeneo ya vijiji kwenye Kata kuna Ofisi za Watendaji wa Kata, basi kipindi ambacho wataanza kuunganisha wateja tumeomba TANESCO waende kutumia hizo ofisi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wetu na nia ni kurahisisha utoaji wa huduma hizi kwa wananchi wa vijijini. Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)