Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIA N. KANGOYE aliuliza:- Kumekuwa na changamoto nyingi katika uvuvi wa Ziwa Victoria unaosababisha malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa uvuvi. Je, Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha inamaliza malalamiko hayo?

Supplementary Question 1

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa naishukuru Wizara kwa lengo lake la kutoa semina kwa Waheshimiwa Wabunge kwa uelewa wa masuala ya uvuvi, lakini kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mwanza ambao wananufaika na uvuvi wa Ziwa Victoria ambao wengi wao ni wanawake na vijana, napenda kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa changamoto nyingi za uvuvi zinatokana na sera na sheria zilizopitwa na wakati ikiwemo Sheria ya mwaka 1972 inayohusisha masuala ya nyavu; je, ni lini Serikali itakaa kuzipitia sheria hizi kwa lengo la kuzirekebisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; licha ya Ziwa Victoria kutumika na nchi tatu, yaani Tanzania, Kenya na Uganda, bado kila nchi imekuwa na sera zake juu ya uvuvi. Je, ni lini Serikali itaanzisha mchakato kuhakikisha kwamba kunakuwa na sera moja ya uvuvi katika Ziwa Victoria yaani One Lake, One Policy? (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Maria Kangoye kwa kuweza kusimamia vyema kabisa maslahi mapana ya wananchi waliomtuma wa Mkoa wa Mwanza wakiwemo vijana na akina mama. Hongera sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameniuliza maswali mawili; la kwanza ni juu ya mapitio na maboresho ya Sheria ya Uvuvi. Naomba nimhakikishie kwamba sheria ile aliyoitaja ya mwaka 1970, Sheria Namba 6 ya Uvuvi tayari ilishaboreshwa, ndiyo maana tuna Sheria Namba 22 ya mwaka 2003 ambayo inakwenda na kanuni zake za mwaka 2009 ambayo na yenyewe sasa tuko katika hatua ya kuiboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tunavyozungumza, wataalam wetu katika ngazi ya Serikali, IMTC kwa maana Makatibu Wakuu wanaijadili na baadaye itaingia katika vikao vyetu vya Baraza la Mawaziri ili kuweza kuboreshwa zaidi na hatimaye kwa maslahi mapana ya sekta hii ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtoe hofu Mheshimiwa Maria Kangoye kwamba Sheria yetu ya Uvuvi kabla ya mwaka huu wa 2018 haujakamilika, tutahakikisha kwamba inaingia humu Bungeni kwa ajili ya kuweza kupata baraka na kuboreshwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni juu ya sera moja ya uvuvi, kwa maana ya kwamba Ziwa Victoria ni ziwa ambalo liko shared na nchi tatu, kwa maana ya Tanzania, Kenya na Uganda ambapo sisi kama Tanzania ndio tunaomiliki eneo kubwa la Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli na nimwambie tu kwamba katika siku ya tarehe 2 Machi, 2018 Mawaziri wa nchi hizi tatu akiwepo Waziri wetu Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina alishiriki katika kikao ambacho kilikwenda na maazimio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya maazimio makubwa kabisa ni kuhakikisha kwamba katika kila nchi, zile taasisi zetu za utafiti zinafanya utafiti na kuweza ku- compromise (kuweza kwenda kwa pamoja) juu ya sera zetu, sheria zetu ili zisiweze kugongana; ili wavuvi wote wanaoshiriki shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria wawe wanajua kwamba sheria hii hapa Tanzania, Kenya au Uganda ni sawasawa bila kuvunja sheria za nchi nyingine.