Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Silvestry Fransis Koka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Mjini

Primary Question

MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:- Mradi wa umeme wa 400KV kutoka Kinyerezi hadi Arusha umepita maeneo mengi ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na Jimbo la Kibaha Mjini, uthamini wa mali za waathirika ulishafanyika toka mwaka 2015. Je, Serikali itawalipa lini wananchi hawa?

Supplementary Question 1

MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea ikiwa ni pamoja na hii ya umeme, pia Waheshimiwa Mawaziri kwa kazi kubwa wanayofanya kufuatilia miradi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kulipa fidia ni kuwawezesha wananchi wanaoathirika na miradi hii mikubwa ya maendeleo ili waweze kupata fedha za kuweza kufanya shughuli nyingine mbadala za kiuchumi wanapopisha maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia zimekuwa zikichelewa sana, wakati mwingine takribani mpaka miaka mitano huku wananchi hawa wakitaabika bila kuweza kufanya shughuli mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mawili ya nyongeza. nafahamu uhakiki wa tathmini na hususan katika maeneo ya Kibaha Mjini, Vijijini na mpaka Chalinze ulikwishakamilika toka 2017.

MHE. SILVESTRY F. KOKA: Je, ni lini sasa kwa uhakika wananchi hawa watalipwa fedha zao?
Swali la pili, Serikali sasa haioni kwamba kuna haja ya kufanya maandalizi ya malipo haya mapema ili tathmini ikishafanyika wananchi waweze kupata malipo yao mapema bila kupata usumbufu na malalamiko makubwa? Ahsante.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, Koka. Kwanza napenda kumshukuru sana na kumpongeza kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia miradi yetu kwenye sekta ya nishati na hususan katika suala hili la fidia kwa mradi huu wa Kinyerezi hadi Arusha, pia tumepokea pongezi zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo swali letu la msingi limesema kwamba fidia hii ya shilingi bilioni 21.56 zimetengwa kwa mwaka huu wa fedha 2017/2018. Ni matarajio yetu kwa kuwa uhakiki wa fidia hii umekamilika na matarajio yetu kwamba mwisho wa mwaka huu wa fedha, pesa hizi zitalipwa na naomba niendelee kuwashukuru wananchi wa maeneo ya Kisarawe, Kinyerezi yenyewe, Kibaha, Chalinze kwa uvumilivu wao. Napenda niwathibitishie Serikali italipa fidia hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili; tunapokea huo ushauri na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kweli nia ni hiyo ya kuona kwamba maeneo wanayochukua kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa, wananchi wanawezeshwa. Ndiyo maana wakati wa bajeti tutaomba atuunge mkono. Tumetenga kabisa kiwango kikubwa tu cha fidia kwa miradi mikubwa ambayo inatarajiwa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha huo 2018/2019 na kuendelea. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Name

Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:- Mradi wa umeme wa 400KV kutoka Kinyerezi hadi Arusha umepita maeneo mengi ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na Jimbo la Kibaha Mjini, uthamini wa mali za waathirika ulishafanyika toka mwaka 2015. Je, Serikali itawalipa lini wananchi hawa?

Supplementary Question 2

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa umeme wa 400KV ni mkubwa sana na unahitaji transfoma zenye ubora wa hali ya juu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutumia transfoma zetu za kiwanda cha TANELEC cha Arusha ambazo zina ubora wa hali ya juu?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa na ninamshukuru sana Mheshimiwa Catherine na ninampongeza pia kwa kufuatilia masuala ya nishati akiwa pia ni Mjumbe wetu wa Kamati ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba umeme unaosafirishwa kwa njia hii ya msongo wa 400KV ni mkubwa na kwa kuwa ni mkubwa, Wizara yetu ya Nishati ilishatoa maelekezo kwamba kuanzia sasa vifaa vyote vinavyotumika kwenye miradi ya umeme vinatakiwa kutoka kwenye viwanda vyetu vya ndani na kimojawapo ni Kiwanda na TANALEC-Arusha. Mara kadhaa takribani kama zaidi ya mara mbili Mheshimiwa Waziri amefanya ziara katika kiwanda kile. Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha transfoma kama 10,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niendelee kutoa wito kwa Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya umeme nchini pamoja na Shirika la umeme, TANESCO kwamba bado agizo letu liko pale pale, vifaa vyote vitoke ndani ya nchi na viwanda vyetu vina uwezo na mara kadhaa tumekutana navyo na vimetuthibitishia. Ahsante.

Name

Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Primary Question

MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:- Mradi wa umeme wa 400KV kutoka Kinyerezi hadi Arusha umepita maeneo mengi ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na Jimbo la Kibaha Mjini, uthamini wa mali za waathirika ulishafanyika toka mwaka 2015. Je, Serikali itawalipa lini wananchi hawa?

Supplementary Question 3

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza; wakati wa upanuzi wa Kiwanda cha Umeme cha Liwale wakati wanapanua ile plant yao, walichukua mashamba ya wananchi ambapo mpaka leo hii zaidi ya miaka mitano wananchi wale hawajui hatima ya malipo yao. Nini kauli ya Serikali namna ya kuwalipa wale wananchi mashamba yao?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Kuchauka kwa swali la nyongeza na ninampongeza pia kwa kazi zake, lakini nataka niseme kwamba suala la fidia kwa mashamba ambayo yamechukuliwa kwa upanuzi wa kituo cha kuzalisha umeme Liwale, naomba kwa kuwa kwa takwimu kwa sasa hivi sina, naomba nilichukue.
Naomba tu nimpe Mheshimiwa Mbunge taarifa ya nyongeza kwamba kwa sasa kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa laini ya msongo wa Kv 132 inayotoka Kituo cha Kuzalisha Umeme Mozambique, nataka nimthibitishie na jitihada ambazo zinaendelea za Wizara kuhakikisha Mikoa ya Kusini, Lindi na Mtwara inapata umeme kutoka Gridi ya Taifa kwamba kwa hivi karibuni Wilaya ya Liwale itapata umeme kupitia kituo hicho na kwamba hata yale matumizi ya mafuta ya kuzalishia umeme Wilaya ya Liwale yatapungua na umeme utapatikana kwa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la fidia nitalichukua, baada ya Bunge hili tutalifanyia mchakato wa kupata taarifa ya uhakika. Ahsante. (Makofi)