Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amina Saleh Athuman Mollel

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:- Utekaji nyara na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) vilikithiri kwenye miaka ya 2000 hali iliyopelekea Serikali kuanzisha kambi maalum kwa ajili ya usalama wao. (a) Je, Serikali imeanzisha kambi ngapi mpaka sasa na ni katika Mikoa na Wilaya zipi? (b) Je, ni watu wangapi wenye ulemavu wa ngozi wanaoishi katika makambi hayo?

Supplementary Question 1

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa baadhi ya watoto wanaosoma katika kituo hiki au Shule ya Buhangija wengi wao wametelekezwa kabisa na wazazi wao, kwa maana ya kwamba wazazi wakati ule wa mauaji waliwafikisha watoto wao getini katika ile shule na kuwaacha; na hivi sasa wakati wa likizo na muda wote yamekuwa ni makazi yao katika kituo hiki; Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba angalu siku moja basi, watoto hawa wanawapata wazazi wao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia swali langu la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu ameeleza idadi ya watu wenye ulemavu wa ngozi waishio kwenye shule ya Buhangija; je, ina mpango gani pia wa kuhahakisha kwamba tunapata idadi kamili ya watu wenye ualbino na hata watu wengine wenye ulemavu ili basi tunapopanga au tunapotunga sera/ sheria kujua kwamba idadi kamili ya watu wenye ulemavu Serikali iweze kupeleka maendeleo? Ahsante.

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho kilikuwa kinafanywa na Serikali baada ya kutokea lile wimbi la mauaji kwa watu wenye ualbino ilikuwa ni kunusuru maisha yao kama nilivyosema, kwa kuweka kwenye vituo mbalimbali, lakini sasa hivi kitu ambacho kimefanyika Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na vitongoji pia na halmashauri ambako wanatoka iliweza kuangalia jinsi gani hawa watu wanaweza wakarudishwa kwenye familia zao kwa kuangalia usalama na kama ile hali inakuwa imeisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa upande wa Kituo cha Buhangija na vituo vingine, Serikali ambacho inafanya sasa hivi ni kutembelea hivi vituo, lakini kama Mheshimiwa Mbunge alivyouliza, kama itabainika kwamba kuna watoto wako kwenye hivi vituo, basi Serikali itafanya utaratibu wa kuwapata wazazi wao ama walezi wao ama familia zao na kuweza kuwarejesha kwenye familia zao ama wakati wa likizo sasa waweze kurudi kwenye famila zao kama ambavyo ilivyo kwa watoto wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nilijibu kwenye swali la Mheshimiwa Khadija Nassir na wakati pia natoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwamba sensa inafanyika kila baada ya miaka kumi. Ilifanyika mwaka 2012, lakini pia itafanyika mwaka 2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu kwa kuona umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi za watu wenye ulemavu kwa ujumla wake, wakiwemo watu wenye ualbino, basi inaandaa mpango ambapo yaani inafanya majadiliano ya ndani kwa kuona kwamba ni jinsi gani sasa tunaweza tukapata takwimu hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshaweka mipango, kwa hiyo, tutawatumia Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vijiji ili kuweza kupata takwimu sahihi za watu wenye ulemavu. Ahsante. (Makofi)