Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Alfredina Apolinary Kahigi

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ALFREDINA A. KAHIGI (K.n.y. MHE. NURU A. BAFADHILI) aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha vijana wetu wanakuwa na maadili pamoja na silka na desturi za Kitanzania kama walivyo wazazi wao?

Supplementary Question 1

MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kwa kuwa luninga zinapoteza watoto wetu katika kupotosha watoto wetu katika maadili, je, Serikali ina mkakati gani wa kutusaidia katika suala hili?
Swali la pili, kuna changamoto katika wasanii wa muziki hasa katika nyimbo zao zina matusi, je, Serikali itatusaidiaje kwa sababu wanawake wanavaaa mavazi ambayo hayana staha Serikali itatusaidiaje kusudi waweze kuacha mambo hayo?(Makofi)

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi kuweza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri sana, tumefaidika sana kama Wizara tunapopata maswali kama haya ningeweza pia kuweza kumshauri Mheshimiwa Waziri kama kuna uwezekano Mheshimiwa Nuru Awadhi aweze kuwa Balozi wa Maadili katika Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameelezea kwamba luninga zinasaidia sana katika kupotosha mmomonyoko wa maadili katika Taifa letu na mimi niseme kwa namna moja ama nyingine nakubaliana na mawazo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyasema, lakini hilo huwa linatokea tu pale ambapo kunakuwa hakuna chombo maalum cha kuweza kusimamia maudhui mbalimbali ambayo yanarusha na vyombo vyetu vya luninga. Kwa kutambua hilo na ndiyo maana Serikali imeunda vyombo viwili ambavyo ni TCRA pamoja na Bodi ya Filamu ambavyo vyote hivi vina lengo kubwa la kuhakikisha kwamba vinasimamia maudhui yanayorushwa katika vyombo vyetu vya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba pamoja na changamoto hizo, Wizara tumeendelea kuhamasisha jamii kwa ujumla kuhakikisha kwamba suala la maadili ni suala ambalo lazima jamiii kwa ujumla wetu kuendelea kulifanyia kazi siyo suala tu la Serikali kama ambavyo nimejibu kwenye jibu la msingi kwamba ni suala ambalo la Serikali, lakini vilevile pamoja na jamii nzima kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, habari njema ni kwamba Wizara kwa sasa hivi imeandaa kanuni mbili ambazo tunaamini kabisa kwamba kanuni hizo ambazo ni kanuni zinazosimamia maudhui katika redio, maudhui katika mitandao ya kijamii na tunaamini kabisa kwamba kwa kupitia kanuni hizi itakuwa ni muarobaini wa kuhakikisha kwamba mmomonyoko wa maadili katika Taifa letu unadhibitiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipende kuchukua nafasi kuweza kuomba vyombo vyote vya habari viweze kuzingatia kanuni hizo ili kuhakikisha kwamba tunatunza maadili ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili ametaka pia kuweza kujua kwamba kumekuwa na tatizo la nyimbo ambazo haziendani na maadili ya Taifa letu hususani wanawake ambao wanavaa mavazi ambayo siyo ya staha.
Mheshimiwa Spika, mimi niseme kwamba sisi kama Serikali tunatambua kwamba tuna changamoto hiyo na kitu ambacho tumekifanya kwa sababu tuna vyombo vyetu viwili ambavyo ni vyombo vinasimamia maudhui kwa wasanii kwa maana ya BASATA pamoja na Bodi ya Filamu. Hivi vyombo viwili vimekuwa vikisisitiza mara kwa mara kuhakikisha kwamba wasanii kabla hawajatoa nyimbo zao wanapeleka nyimbo zao BASATA, wanapeleka video zao Bodi ya Filamu ili ziweze kuhaririwa na ziweze kupewa madaraja.

Mheshimiwa Spika, jambo la kusikitisha ni kwamba...
Mimi nikushukuru lakini niseme kwamba tumekuwa tuna changamoto kubwa sana k wasanii wetu hawapeleki nyimbo zao kwenda kuhaliliwa BASATA naomba kuchukue nafasi hii kuweza kuwaambia kwamba wasanii wote wahakikishe kwamba wanapeleka nyimbo zao BASATA ili ziweze kuhaririwa kabla hawajaanza kuchukuliwa hatua. Ahsante. (Makofi)

Name

Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Primary Question

MHE. ALFREDINA A. KAHIGI (K.n.y. MHE. NURU A. BAFADHILI) aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha vijana wetu wanakuwa na maadili pamoja na silka na desturi za Kitanzania kama walivyo wazazi wao?

Supplementary Question 2

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana ushoga usagaji na kutukuna matusi mithili ya bomu la nyuklia siyo maadili yetu na desturi ya Mtanzania, lakini vitendo hivyo vimekithiri kartika mitandao yetu ya kijamii. Kwa mfano, wapo mashoga maarufu wanajitangaza katika mitandao yetu ya kijamii na siyo utamaduni wa Kitanzania; kwa mfano kuna mtu mmoja maarufu anaitwa James Delicious.
Mheshimiwa Spika, kuna vikundi vya matusi kabisa katika mitandao ya kijamii. Mfano kuna team Wema, team Zari, team Diamond, team Shilole, hawa wamekuwa wakitukana matusi katika mitandao ya kijamii.
Je, nini kauli ya Serikali kutokana na hili kwa sababu linachangia kwa kiwango kikubwa sana kuharibu maadili na utamaduni wa Kitanzania? (Makofi)

Name

Dr. Harrison George Mwakyembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Answer

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Tulitunga Sheria ya EPOCA mwaka 2010 lakini tulikosa Kanuni za kuweza kubana hasa maudhui upande wa mitandao. Tumeshatunga hizo Kanuni na sasa hivi hizo Kanuni zimeanza kufanya kazi. Naomba nitoe taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba kuna baadhi ya wasanii wetu ambao walianza kufanya uhuni uhuni ndani ya mitandao, jana tumeweza kumkamata mwanamuziki nyota Tanzania, Diamond tumemfikisha polisi na anahojiwa kutokana na picha alizozirusha. Vilevile imebidi hata Binti Nandy naye apelekwe polisi kuhojiwa. Tunaangalia namna ya kuwapeleka mahakamani.
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe wito kwa vijana wote nchini, mitandao siyo kokoro la kupeleka uchafu wote ambao umezuiwa na sheria zingine. Hii nchi ina utamaduni wake. Tunahitaji kulinda kizazi cha leo, kesho na kesho kutwa cha Taifa hili. Ahsante. (Makofi)

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. ALFREDINA A. KAHIGI (K.n.y. MHE. NURU A. BAFADHILI) aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha vijana wetu wanakuwa na maadili pamoja na silka na desturi za Kitanzania kama walivyo wazazi wao?

Supplementary Question 3

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumza mmomonyoko wa maadili kwa vijana mara nyingi tunazungumza habari ya vijana wasanii, wanaocheza filamu, wanamuziki na kadhalika. Lakini mmomonyoko pia mkubwa sana upo kwa vijana wa mitaani na hawa mara nying ni kwa sababu ya kukata tamaa.
Sasa naomba niiulize Serikali, pamoja na mifuko mbalimbali ya kuwaendeleza vijana, ni mkakati gani ambao Serikali inao ili kuwasaidia kisaikolojia na namna vilevile ya kuweza kuona matumaini katika maisha yao vijana waache kuingia kwenye tabia ambazo kwa kweli zinasababisha mmomonyoko mkubwa sana wa maadili? (Makofi)

Name

Dr. Harrison George Mwakyembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Answer

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii na ninakushukuru kwa kujibu sehemu ya hilo swali kwamba huu ni wajibu wa jamii nzima. (Makofi). Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imekuja kwa nguvu sana na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu ili Watanzania wathamini kazi. Kazi ndiyo ufunguo wa kila kitu ningeomba Watanzania wote tushirikiane kuhakikisha kwamba kila mtu Tanzania anafanya kazi, mambo ya njia za mpito kuweza kuishi hayana nafasi tena ndiyo yanayozua matatizo.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili wazazi tuna nafasi kubwa sana kuweza kubadilisha hii hali kwa upande wa watoto wetu tukiweka mbele suala la kazi kama tulivyokuwa tunafanya wakati wa uhuru ambapo tulikuwa tunasema uhuru ni kazi na leo ni hapa kazi tu. Ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kwanza niungane na Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe kwa kukubaliana naye kwamba suala la kubadilisha utaratibu wa mfumo wa maisha kwa vijana pamoja na kwamba ni suala la jamii kwa ujumla, lakini napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba pia kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tumeandaa programu mbalimbali ambazo tunashirikiana na Halmashauri za Wilaya kuhakikisha Halmashauri zetu Idara za Vijana zinajipanga kutoa elimu ya kubadilisha mawazo na mtazamo kwa vijana ili kuwasaidia kujenga mtazamo mpya wa kujiajiri na kuondoka katika tabia za kupoteza muda kwenye vijiwe na kuingia kwenye shughuli ndogondogo za kuweza kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tusaidiane kwa pamoja na Halmashauri zetu, hasa wale vijana ambao wamekuwa wakipoteza muda mwingi kwenye vijiwe. Wageuze vijiwe vyao kuwa ni shughuli za kiuchumi badala ya kutumia vijiwe kuwa ni maeneo ya kupoteza muda. Mifuko ya kuwawezesha hao vijana kupitia Idara ya Vijana kwenye Halmashauri zetu ipo na Serikali tumeshajiandaa na Wabunge ambao wapo tayari tutafanya nao kazi hiyo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)