Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:- Pamoja na kuishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kumwondolea mkulima matatizo ya zao la tumbaku:- • Je, Serikali imechukua hatua zipi katika kuimarisha utendaji kazi wa Bodi mpya ya Tumbaku ili ifanye kazi kikamilifu? • Je, Serikali inawahakikishiaje wakulima wa tumbaku upatikanaji wa mbolea kwa wakati?

Supplementary Question 1

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize maswali ya nyongeza, lakini kabla sijafanya hivyo, kwa ruhusa yako, kwanza naomba nichukue nafasi kwa niaba ya wananchi wa Urambo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kupitia Ofisi yake ya Rais, Manejimenti ya Utumishi kwa kauli aliyoitoa hivi karibuni, Mheshimiwa George Mkuchika, Waziri Mhusika, ya kuwarudisha kazini Watendaji wa Vijiji na Madereva waliokuwa wameachishwa kazi kutokana na elimu yao ya darasa la saba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuwarudisha kazini na kuamrisha walipwe mishahara yao yote ambayo wameikosa katika kipindi walichokuwa wamesimamishwa ni ishara na ushahidi tosha kwamba Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi ni sikivu. Tunaiomba Serikali yetu iendelee kuwasikiliza wanyonge na kuwatengenezea yale ambayo wanaona hayakwenda sawa. Ahsante sana Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyotoa lakini pia kuishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Waziri Mkuu mwenyewe kwa kuunda Bodi ya Tumbaku mpya ambayo imeanza kazi vizuri. Ombi langu tu kwa Serikali ni kuiwezesha kwa kuipa vifaa zaidi kama komputa na kadhalika, lakini pia ateuliwe Mwenyekiti ambaye naamini atakuwa ana uzoefu na zao la tumbaku.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikiombwa na wakulima wa tumbaku kutafuta wanunuzi zaidi wa tumbaku ili walime tumbaku zaidi lakini pia ilete ushindani wa bei ili mkulima wa tumbaku anufaike na zao lake, nataka kujua suala hili limefikia wapi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali haiwezi kuagiza mbolea kwa wingi hasa NPK ili mbolea hiyo iwafikie wakulima mapema kuliko kama ilivyokuwa kipindi kilichopita? Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Mary Machuche Mwanjelwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mama yangu Mwalimu Margaret Simwanza Sitta kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia suala hili la zao la tumbaku kule Tabora na Tanzania nzima kwa muda mrefu kuhakikisha kwamba zao hili linakuwa na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija katika maswali yake mawili ya nyongeza ni kweli kabisa Bodi ya Tumbaku haina Bodi ya Wakurugenzi lakini imezinduliwa Disemba, 2017 na sasa hivi tunakaimu Mwenyekiti, ni miezi mitatu tu tangu imezinduliwa. Kwa hiyo, tunaamini kabisa Mheshimiwa Rais akiridhia kuteua Mwenyekiti basi na Bodi hii itaongeza tija katika utendaji wake wa kazi.
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye swali lake hilohilo la nyongeza kuhusu ku-monopolize hii biashara ya tumbaku ni kwamba kama Serikali sasa hivi tuna makampuni manne tu ambayo yananunua tumbaku lakini tuko kwenye majadiliano na Zimbabwe, Misri, China na Vietnam. Vilevile Serikali ya Indonesia kupitia Kampuni ya Star International wao wameshakubali pia kununua tumbaku yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nikija katika swali lake la pili kuhusu ununuzi wa mbolea kwa pamoja, sisi kama Serikali tuna mbolea ya DAP pamoja na UREA ambayo yenyewe ndiyo iko katika mfumo ule wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja, NPK haiko katika mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu na Mheshimiwa Mbunge kwamba mbolea hii ya NPK ambayo inatumika sana katika zao la tumbaku pia tunalichukua suala lake tutalifanyia kazi na hasa ukizingatia kwamba mbolea ya NPK mwaka jana ilitumika tu asilimia 21 ukilinganisha na ile ya UREA ambayo ilitumika asilimia 46. Kwa hiyo, wazo lako Mheshimiwa Mbunge ni zuri tunalipokea ili kuhakikisha kwamba mbolea inafika kwa wakulima kwa msimu. Mheshimiwa Spika, ahsante.