Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:- Kutokana na kuongezeka kwa matangazo ya biashara kwenye vyombo vya habari, upo uwezekano wa baadhi ya matangazo hayo kuwakera na kuleta hisia tofauti kwa baadhi ya watu na hasa watoto kutokana na maudhui mabaya ya baadhi ya matangazo haya. (a) Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuunda chombo cha kusimamia maudhui ya matangazo ya kibiashara ili kuweka na kusimamia taratibu na kanuni za matangazo? (b) Je, ni idara gani ya Serikali inahusika moja kwa moja na malalamiko ya wananchi dhidi ya kampuni na taasisi zinazotoa matangazo yenye athari kwa jamii? (c) Je, ni hatua gani zinachukuliwa dhidi ya kampuni hizo?

Supplementary Question 1

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kuna Kamati ya Maudhui, siku za karibuni tumekuwa tukishuhudia wasanii wetu wengi wakifungiwa nyimbo zao, wasanii ambao wamehangaika kutafuta pesa za kurekodi kwa shida na ukizingatia kuna uhaba wa ajira.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akatuambia Kamati hiyo ya Maudhui imeshindwa kazi, kwa sababu wamekuwa wanaachia mpaka nyimbo zinatoka ndiyo wanakuja kuwafungia wasanii wetu? (Makofi)

Name

Dr. Harrison George Mwakyembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Answer

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kila Taifa lina utamaduni wake na lazima liulinde kwa udi na uvumba. Tunachokifanya sio kwamba tuna vita na wasanii wetu, hapana! Lengo letu ni kulinda maadili ambayo katika kipindi hiki cha utandawazi na maendeleo ya kasi ya kiteknolojia na habari, kuna mmomonyoko mkubwa sana wa maadili katika nchi yetu ni lazima tuchukue hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya hapa siyo kitu cha pekee duniani, kila mtu anafanya hivyo na hawa wasanii wetu tumeshawasamehe wasirudie tena. Nitoe mfano mmoja mdogo…

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamuziki Rick Ross ambaye amepiga muziki pamoja na kijana wetu nyota wa muziki Diamond hapa, wimbo wao huu wa wakawaka, huyo mwanamuziki miezi michache iliyopita amepata matatizo Marekani kwa kuimba wimbo unaoitwa U.O.E.N.O ambao maudhui yake yanaleta picha ya kwamba anaunga mkono ubakaji. Marekani nzima akina mama walikuja juu, wimbo ukaondolewa kwenye televisions zote, lakini na yule kijana akaomba radhi kwa wanawake wote kwamba amewaudhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tumekuwa kokoro, tupokee kila kitu, kwa sababu hatuna utamaduni. Baba wa Taifa alisema mwaka 1962, Taifa lisilo na utamaduni wake ni Taifa mfu nasi hatuwezi kukubali kuwa Taifa mfu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yanayotokea Tanzania yanatokea duniani kote. Nitoe tu maelezo kidogo, maana Viongozi wetu hapa wanalalamika ni kwa sababu dunia pana hawajaielewa. Davido mwanamuziki maarufu duniani ambaye amepiga na kijana wetu Diamond hapa kafungiwa nyimbo zake mbili na Nigerian Broadcasting Corporation mwaka huu. Siyo huyo tu, Wizkid kafungiwa nyimbo zake, Nine Eyes kafungiwa nyimbo zake, sijasikia Wabunge wa Nigeria wakilalamikia sheria zao wenyewe, sisi ni Wabunge kazi yetu kubwa ni kuhakikisha jamii inaheshimu, inalinda sheria za nchi na tutaendelea... (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano wa mwisho, Koffi Olomide amepiga wimbo unaitwa Ekotite, huu wimbo ni marufuku kupigwa Congo (DRC)…

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge mnaosafiri kwenda Congo, unaambiwa tukupigie wimbo gani ukisema Ekotite watakushangaa! Huo wimbo ni matusi wameufungia. Sisi hapa Wabunge tunakuwa wa kwanza kuruhusu nchi yetu iwe kokoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, BBC ambayo iko Uingereza ambako ndugu zangu wanadhani ndiko mwanzo wa ustaarabu, wamefungia nyimbo 237 katika historia yao, hapa tunalalamika nyimbo mbili kufungiwa. Tutaendelea kufungia kulinda utamaduni wa nchi yetu. Ahsante. (Makofi)