Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari ambapo matibabu yake ni ya muda mrefu. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa dawa za ugonjwa wa kisukari bure kama ilivyofanya kwa ugonjwa wa kifua kikuu?

Supplementary Question 1

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri ameonesha kwamba huduma hizi sasa zinaanza kutolewa kuanzia Hospitali ya Wilaya, na ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wetu wengi wapo vijijini.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha huduma hizi katika vituo vya afya ili kupunguza adha ya wananchi wetu kutembea kwenda Hospitali ya Wilaya?
Swali la pili, miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na kisukari, hivi sasa kuna ujenzi unaoendelea wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini kule Mtwara, amesema kwamba hospitali za rufaa za kanda zitatoa vilevile huduma hii katika ngazi ya kanda.
Je, Serikali imejiandaaje sasa itakapofunguliwa Hospitali ya Kanda ya Kusini ambayo inajengwa Mtwara, kwamba huduma ya saratani pia itatolewa katika hospitali hiyo ili kuwapunguzia adha Wanamtwara kwenda Hospitali ya Ocean Road iliyopo Dar es Salaam? (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Abdallah Chikota kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya na kwa kuwapigania wananchi wake wa Jimbo lake na Mkoa wa Mtwara katika masuala yote yanayohusiana na afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa sana la magonjwa yasiyoambukizwa, siyo tu kisukari, lakini hata vilevile kiharusi, masuala ya pressure, magonjwa ya figo. Serikali inaendelea na utaratibu wa kujenga uwezo katika mnyororo wake wa utoaji wa huduma, sasa hivi tuko katika ngazi ya Wilaya lakini tunaendelea kuboresha kushuka katika ngazi ya vituo vya afya na mwisho tutashuka mpaka katika dispensaries.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu kwamba huduma za awali kwa magonjwa kama haya ya upimaji wa sukari, upimaji wa pressure, yote yanafanyika katika ngazi zote za mnyororo, lakini dawa kwa mfano, insulin ambazo zinahitaji utaalam zaidi zinapatikana katika ngazi ya Wilaya. Lakini tutaendelea kuboresha utaratibu huu kadri tutakapokuwa tunajenga uwezo katika mnyororo wetu wa utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza, je, Serikali itakuwa tayari kuanzisha huduma za saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ambayo inajengwa Mtwara. Kwa mujibu wa taratibu katika ngazi hiyo ya Rufaa ya Kanda, moja ya huduma ni pamoja na upatikanaji wa huduma za saratani. Kwa hiyo, pindi hospitali hii itakapokuwa tayari huduma hiyo nayo tutaiweka. (Makofi)

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari ambapo matibabu yake ni ya muda mrefu. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa dawa za ugonjwa wa kisukari bure kama ilivyofanya kwa ugonjwa wa kifua kikuu?

Supplementary Question 2

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza:
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa letu linakabiliwa na tatizo kubwa ambalo kimsingi ni janga la utapiamlo na lishe iliyopitiliza, hii lishe iliyopitiliza ndiyo chimbuko sasa la magonjwa kama kisukari na magonjwa ya moyo.
Je, Serikali ipo tayari kwa maksudi kabisa kuandaa semina kwa Bunge zima ili Wabunge hawa wakielimika iwe chachu ya kutoa elimu kwa jamii nchini?(Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kitandula ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge, Masuala ya Lishe, kwa kusimamia vizuri masuala ya lishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumekuwa na changamoto kubwa sana ya utapiamlo pamoja na suala la lishe iliyopitiliza ambayo kwa lugha ya kitaalam tunaita viribatumbo (obesity) na sisi kama Serikali tumeweka mkakati ambao ni jumuishi na ambao ulizinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka jana, ambao unashirikisha sekta zote kuhakikisha kwamba tunajenga Tanzania yenye lishe. Wizara tupo tayari kutoa semina kwa Wabunge ili kuwajengea uwezo na uelewa na wao kwenda kusemea masuala ya lishe na viribatumbo katika jamii wanazotoka.(Makofi)