Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:- Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2015/2016 wanawake 85 Mkoani Singida walipoteza maisha kutokana na vifo vya uzazi. Aidha, inaelezwa kitaalam asilimia 35 ya vifo hivyo vinaweza kuzuiliwa iwapo huduma za uzazi wa mpango zitazingatiwa na kuimarishwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha elimu na huduma za afya ya uzazi wa mpango kwani utumiaji wa huduma hizo kwa sasa unatekelezwa kwa asilimia 19 wakati wastani wa kitaifa ni asilimia 27?

Supplementary Question 1

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa takwimu zinaonesha Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni na moja ya sababu ni kutokuimarishwa kwa elimu ya uzazi wa mpango.
Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuanzisha kampeni ya kitaifa ili kuwawezesha wanafunzi na hasa wa kike kuanzia shule za msingi hadi sekondari kuweza kujitambua na kuepukana na mimba za utotoni? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa hospitali za Mkoa wa Singida pamoja na vituo vya afya vina uhaba mkubwa wa wataalam na vifaatiba. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha hospitali na vituo vya afya vya Mkoa wa Singida vinapatiwa wataalam na vifaatiba vya kutosha ili kuziwezesha hospitali hizo kufanya kazi kwa ufanisi na kuokoa vifo vya akinamama wajawazito na watoto? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Aisharose Matembe kwa kuwa mpiganaji mkubwa sana wa masuala ya afya ya akina mama na watoto katika Mkoa wa Singida na kwa Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba tuna changamoto kubwa sana ya mimba za utotoni na takwimu ambazo tunazo zinaonyesha kwamba wastani wa asilimia 27 ya vijana ambao wapo kati ya miaka 15 mpaka 19 aidha, wameshapata watoto au ni wajawazito, hii idadi ni kubwa sana na baadhi ya Mikoa inakaribia asilimia 50. Kwa kutambua hilo, Serikali imeweka mkakati na Wizara tumeanzisha kampeni inayoitwa “Mimi ni Msichana, Najitambua, Elimu Ndio Mpango Mzima.” Hii kampeni tayari tumeshaizindua na inaendelea kusambaa nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, ndani ya Wizara sasa hivi tunakamilisha kuandaa mkakati wa afya ya uzazi kwa vijana, ambao itatoa dira na mwelekeo wa nini tunahitaji kufanya hususan katika yale maeneo ambayo mimba za utotoni zimeshamiri. Sambamba na hilo, tumeanzisha club katika maeneo mbalimbali hususan katika shule za sekondari kuwajengea uwezo vijana wetu hususan mabinti wa kike kujitambua na kuhakikisha kwamba wanapata elimu ya kutosha kuhusiana na elimu ya uzazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, tafiti zimethibitisha kwamba tunapomnyanyua mwanamke kiuchumi vilevile tunazuia uwezekano wa wale mabinti kupata mimba za utotoni, sambamba na hili kuna miradi ambayo tunaifanyia upembuzi yakinifu sasa hivi ambayo itatoa fedha kidogo kuwajengea uwezo wale mabinti especially wale ambao wapo nje ya mfumo wa shule kuweza kujikimu kimapato na hii ni moja ya mkakati ambao tumeuona umekuwa na tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka huu wa fedha tumeweza kuongeza bajeti ya mpango wa afya ya uzazi kutoka shilingi bilioni tano mpaka shilingi bilioni 18. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza nini mkakati wa Serikali kuongeza wataalam na vifaatiba. Katika mwaka huu wa fedha, bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaatiba ni bilioni 269 na nimeongelea hapa bajeti ambayo tumeiweka katika family planning kutoka bilioni tano mpaka bilioni 18. Tatizo siyo fedha, tatizo niwaombe Waheshimiwa Wabunge watusaidie ni kuwahimiza waganga wetu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kwamba wanaagiza vifaa na dawa ambazo zinahusiana na masuala ya uzazi wa mpango.
Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa ni tabia ya baadhi ya watoa kutoagiza vifaa hivi kwa sababu wanaona kwamba havina tija au havitoki haraka katika hospitali zao, lakini ni sehemu ya tiba muhimu na dawa muhimu sana hususan katika upande wa uzazi wa mpango, lakini Serikali itaendelea kutoa elimu hiyo na kuhamasisha watoa huduma kuhakikisha kwamba wanaagiza dawa hizo na sisi kama bohari ya dawa tunazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni kweli tumekuwa na changamoto ya uhaba wa watumishi na tunaamini kwamba kadri vibali vinapopatikana tutakuwa tunaongeza wigo wa watoa huduma katika hospitali hizi. (Makofi)

Name

Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:- Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2015/2016 wanawake 85 Mkoani Singida walipoteza maisha kutokana na vifo vya uzazi. Aidha, inaelezwa kitaalam asilimia 35 ya vifo hivyo vinaweza kuzuiliwa iwapo huduma za uzazi wa mpango zitazingatiwa na kuimarishwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha elimu na huduma za afya ya uzazi wa mpango kwani utumiaji wa huduma hizo kwa sasa unatekelezwa kwa asilimia 19 wakati wastani wa kitaifa ni asilimia 27?

Supplementary Question 2

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi naomba nimuulize Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Hospitali za Mikoa ya Dar es Salaam, kwenye wodi za akina mama kumekuwa na msongamano mkubwa sana wa mama wajawazito, wengine wanalala wawili na wengine wanalala chini.
Je, Serikali ina jitihada gani za maksudi kuhakikisha hizi wodi za akina mama zinakuwa na mpangilio maalum, mama mjamzito anavyofikishwa hospitalini apate kitanda cha peke yake, kwa sababu wako wawili na kulala watu wawili pia inachangia kuambukiza maradhi? Je, Serikali ina mkakati gani…

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaboresha mnyororo wa utoaji wa huduma za afya kwa kuboresha mifumo ya rufaa na moja ya mikakati ni hii ambayo tumeendelea kuisema na nimeigusia hapa kuboresha vituo vya afya, hospitali za Wilaya na hospitali za Rufaa za Mikoa ili ziweze kutoa huduma za uzazi salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema jana, kwangu siyo faraja sana kusikia kwamba wakina mama 100 wamezaa katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili. Tunachotaka kuona pale Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ni case zile ambazo zipo complicated, kesi nyingine zote sasa hivi tumejenga uwezo katika vituo vyetu vya afya, hospitali zetu za Wilaya na Hospitali za Rufaa za Mikoa ili ziweze kutoa huduma. Nitoe rai kwa wananchi kuzitumia hospitali zetu hizi. (Makofi)

Name

Joshua Samwel Nassari

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arumeru-Mashariki

Primary Question

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:- Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2015/2016 wanawake 85 Mkoani Singida walipoteza maisha kutokana na vifo vya uzazi. Aidha, inaelezwa kitaalam asilimia 35 ya vifo hivyo vinaweza kuzuiliwa iwapo huduma za uzazi wa mpango zitazingatiwa na kuimarishwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha elimu na huduma za afya ya uzazi wa mpango kwani utumiaji wa huduma hizo kwa sasa unatekelezwa kwa asilimia 19 wakati wastani wa kitaifa ni asilimia 27?

Supplementary Question 3

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashuhudia wanawake wengi wakati wanapojifungua wanapata maradhi ya fistula, je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha wanawake hawa wanaojifungua wanaepukana na maradhi haya ya fistula?(Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa swali zuri ambalo ameuliza Mheshimiwa Munira.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamke kupata fistula maana yake ni kwamba hakupata huduma nzuri wakati alipokuwa anakaribia kujifungua na hiyo ndiyo tafsiri yake kubwa ya msingi, kwa sababu fistula haipaswi kutokea kama mwanamke alipata uangalizi mzuri wakati anajifungua. Katika changamoto hiyo tumeiona, tunaendelea kuboresha utoaji wa huduma, kutoa elimu kwa watoa huduma wa afya, vilevile kuhakikisha kwamba tunazisogeza huduma za dharura za kumtoa mtoto tumboni karibu zaidi na wananchi ili hali ile ambayo inatokana na mwanamke kukaa labor kwa muda mrefu tuondokane nayo.