Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rukia Ahmed Kassim

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:- Je, Serikali imejipanga vipi kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto?

Supplementary Question 1

MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa vitendo hivi vinapotokea mara nyingi ushahidi wa awali haupatikani. Je, Serikali imejipanga vipi kutoa taaluma kwa wananchi nini kifanyike mara tu linapotokea jambo hili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali inachukua hatua za kutosha dhidi ya udhalilishaji huu lakini bado vitendo hivi vinaendelea kwa kasi kubwa katika jamii zetu. Je, Serikali haioni kwamba adhabu inayotolewa ni ndogo hivyo basi ilete sheria hapa Bungeni tuipitishe yeyote atakayepatikana na hatia ya kubaka mtoto mdogo ahasiwe? (Makofi/Kicheko)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, matukio mengi ya udhalilishaji sasa hivi yanakuwa reported na hii inaonesha kwamba mwamko wa jamii nao umeongezeka. Tumepanua wigo sana kupitia Idara zetu za Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii pamoja na Jeshi la Polisi kwa kuanzisha Madawati ya kuweza kutoa taarifa kuhusiana na suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini matukio mengi ya udhalilishaji dhidi ya watoto yamedhihirisha kwamba yanafanywa na watu wa karibu wa familia. Naendelea kutoa rai kwa wanajamii na familia kuyatolea taarifa punde yale matukio yanapotokea na sisi ndani ya Wizara ya Afya pamoja na Jeshi la Polisi tumejipanga vizuri kuyashughulikia kwa uharaka zaidi pindi yanapotokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi kwa mujibu wa sheria udhalilishaji wa mtoto adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni tano na kifungo kisichozidi miezi sita ama vyote kufanyika kwa wakati mmoja. Sambamba na hilo, Serikali itaendelea kutafakari kwa kadri inavyoona inafaa kama kuna umuhimu wa kuongeza adhabu kutokana na matukio kama hayo.

Name

Faida Mohammed Bakar

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:- Je, Serikali imejipanga vipi kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto?

Supplementary Question 2

MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hili tatizo la udhalilishaji wa watoto sasa hivi limekuwa ni sugu ama ni donda ndugu yaani ni zaidi ya kila kitu na sisi wazazi inatuuma sana. Unaweza ukamuona mtoto anatoka mafunza mwanamume anamdhalilisha mtoto mchanga, hii iko sana kule kwetu Zanzibar, inauma sana maana hata wazazi wenyewe wengine wanawaingilia watoto wao. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa watu kama hao wanaofanya udhalilishaji wa watoto wetu hasa ikizingatiwa kwamba wakifanyiwa tatizo hilo wanaficha na wanamalizana wenyewe kule nyumbani hawapeleki taarifa kunakohusika? (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Faida Bakar ambalo amelielezea kwa hisia kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria na Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, mtoto ana haki zake tano na naomba nizinukuu kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge. Mtoto ana haki ya kuishi; kulindwa; kuendelezwa; kushirikishwa na kutobaguliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambasamba na hilo, Serikali inakemea sana udhalilishaji wowote wa kijinsia dhidi ya mtoto. Ndiyo maana tumesema kwamba tumeweka mkakati wa kiserikali wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha 2020/2021 na lengo na kusudio ni kuhakikisha kwamba tunatokomeza kabisa ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimetoka kusema kwamba udhalilishaji mwingi unafanyika katika ngazi ya familia. Naomba nitoe rai kwetu sisi Wabunge wote na jamii yote ambayo inaendelea kutusikiliza, tusiyafumbie macho matukio na udhalilishaji wowote dhidi ya wanawake na watoto na sisi kama Serikali tutaendelea kushirikiana na jamii kuchukua hatua za haraka kwa wote wanaofanya matukio kama haya.

Name

Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Primary Question

MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:- Je, Serikali imejipanga vipi kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto?

Supplementary Question 3

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Udhalilishwaji wa watoto ni pamoja na watoto wa kike kutopata mahali pa kujisitiri katika shule zetu za msingi na sekondari. Serikali ilishatoa kauli kwamba shule zetu ziwe na vyumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri wanapokuwa mashuleni lakini vyumba hivyo mpaka sasa havijakamilika. Ni kwa nini Serikali imeshindwa kusimamia kauli yake yenyewe wakati watoto wa kike wamekuwa wakidhalilika katika mazingira yao ya masomo?

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba watoto wa kike ambao wako shule wanahitaji sehemu ya kujisitiri wakati wakiwa katika siku zao. Niseme tu kwamba hili tumeshaanza kulifanyia kazi kwa kushirikiana na wenzetu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Elimu. Katika vyoo ambavyo sasa hivi tumeanza kuvijenga kwenye baadhi ya shule tumeshaweka utaratibu huo wa kuwa na vyumba na vyoo maalum kwa ajili ya watoto wa kike.

Name

Rose Cyprian Tweve

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:- Je, Serikali imejipanga vipi kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto?

Supplementary Question 4

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na mikakati mizuri ambapo Wizara inahakikisha tunatokomeza hivi vitendo vya ubakaji nadhani Walimu wana nafasi kubwa ya malezi ya watoto wetu. Kwa nini tusiweke kipengele maalum kwenye mitaala yao jinsi ya kubaini na kuwafanyia counseling hawa watoto mara wanapobaini kuwa wamebakwa? Nakushukuru sana.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli jambo hili kwanza linakera na linaudhi lakini si muda mrefu tulikuwa na kikao cha Maafisa Elimu wote wa Mikoa na Wilaya na jambo hilo tumeliwekea msisitizo hasa katika suala zima la kuhakikisha kwamba, watoto wa kike wanalindwa. Hata hivyo, ushauri wa Mheshimiwa ni mzuri, Serikali tumeuchukua na tutakwenda kuufanyia kazi kwa kadri tutakavyoona inafaa.

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:- Je, Serikali imejipanga vipi kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto?

Supplementary Question 5

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Wakati Mheshimiwa Naibu Waziri anajibu alitueleza kwamba kuna Madawati ya Jinsia 117. Hii inaonesha dhahiri kwamba kuna Wilaya nyingine hazina haya Madawati ya Jinsia. Ni ukweli kabisa kwamba kiwango cha ubakaji kwa maana ya watoto wa kike lakini na ulawiti wa watoto wa kiume kimekuwa kikiongezeka sana na tunajua sheria zipo. Ni kwa nini hawa watu wanaendelea kufanya hivi labda ni kutokana na mianya ambayo ipo kuanzia kwenye Jeshi la Polisi na kwingineko.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua kwa sababu sheria zipo lakini bado vitendo hivi vinaendelea, ni kwa nini sasa Serikali isije na njia mbadala kama tiba kabla ya hili tukio kutokea, kuwafanyia kama counseling hao wanaotenda kwa maana kwenye maeneo husika wazazi au jamii husika ili tuwe na tiba mbadala kabla ya tukio kutokea kwa sababu tunaona haya mambo yanatokea na sheria zipo ni kwa nini msibuni …

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inafanya njia mbadala nyingi tu na niweke tu kumbukumbu sawa kwamba Madawati ni zaidi ya 417 na kwenye Vituo vya Polisi vyote tumeweka Madawati ya aina hiyo ili kuongeza idadi iwe kubwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu njia mbadala, kama Serikali tumeendelea kuongeza jitihada za kutoa elimu licha ya hatua kali tunazozichukua. Ndiyo maana tunaendelea kuwasihi hata viongozi wa kiroho kwenye nyumba za ibada kuendelea kutoa elimu hiyo kwa sababu matukio haya maeneo mengi yanaambatana na imani za kishirikina. Wengine wanaamini wakifanya hivi watapata utajiri, wengine wanakuwa na kesi wanaamini wakifanya hivyo watakuwa wamesafishika kwenye kesi hizo na wengine wanaamini watapona magonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, jamii kwa ujumla wake katika maeneo tofauti tofauti tumeona tupanue elimu hasa hasa zikiwepo nyumba hizo za ibada kwa sababu maeneo ambapo nyumba za ibada watu wameshika sana mienendo ya Kimungu matukio haya ya kikatili yamekuwa pungufu zaidi. Kule ambapo kuna imani nyingi za kishirikina ndiko ambapo matukio haya ya ajabu ajabu yamekuwa yakiendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya kazi hiyo kuwapa viongozi wa kiimani tunaendelea kutoa rai kwa wananchi kutoa taarifa ili sisi kwa upande wa Serikali tuweze kuchukua hatua kali kwa wale watakaobainika wamefanya hivyo.

Name

Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Primary Question

MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:- Je, Serikali imejipanga vipi kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto?

Supplementary Question 6

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Walimu ndiyo wanaowalea watoto wetu shuleni na ndiyo wanaotegemewa zaidi kuwa walinzi wa watoto hawa wanapokuwa shuleni. Hata hivyo, baadhi ya Walimu ndiyo wamekuwa na tabia za kuwadhalilisha watoto kwa vitendo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kuwa kuna suala la elimu, mtoto yule anakuwa mwoga kutoa taarifa pale anapodhalilishwa na Mwalimu. Serikali ina mkakati gani wa kuwapa watoto elimu ili wawe na ujasiri wa kuripoti vile vitendo ambavyo wanafanyiwa na baadhi ya Walimu? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Prof. Joyce Lazaro Ndalichako

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Answer

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali imeweka utaratibu shuleni wa kuwawezesha watoto wa kike kuwa na ujasiri wa kuripoti matukio ya udhalilishaji ambayo yanafanyika yaani life skills na pia tumeanzisha club mbalimbali za kuwawezesha watoto kuwa na ujasiri wa kuweza kuripoti matukio hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie fursa hii kuomba na kuwasihi watoto wasiwe na uwoga wowote kwa sababu Serikali yao inawalinda. Pale ambapo anafanyiwa vitendo ambavyo ni kinyume na matakwa ya Serikali, watoe taarifa na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote wanaodhalilisha watoto na kuwasababishia wasisome shuleni kwa amani. (Makofi)

Name

Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:- Je, Serikali imejipanga vipi kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto?

Supplementary Question 7

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuwaadhibu wale wote wanaofanya vitendo vya udhalilishaji, lakini watoto hawa wanaofanyiwa udhalilishaji wanapata madhara ikiwemo kuambukizwa magonjwa na kupewa mimba. Je, Serikali ina jitihada gani za kuhakikisha watoto hawa ambao wamepata maradhi au wamepata mimba wanasaidiwa ili kutimiza ndoto zao za maisha? (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua ambazo nimetoka kuzieleza na ambazo Waheshimiwa Mawaziri wametoka kuzisema za kuchukua hatua kuhusiana na wahusika ambao wanafanya matendo hayo ya udhalilishaji, nami niendelee kutoa rai tu, changamoto ya kuyafikisha mashauri haya Mahakamani mojawapo ni kwamba ndugu na wazazi wa watoto wale wanakubaliana na mtuhumiwa kuyamaliza mashauri yao nje ya Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba udhalilishaji wowote wa mwanamke na mtoto masuala haya yasimaliziwe mtaani, badala yake yaweze kufikishwa katika vyombo vya dola. Sisi kama Wizara na Serikali tutaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kwamba matibabu kwa wale ambao watakutwa wameathirika na virusi vya UKIMWI, kwa sababu huduma za tiba ya UKIMWI zinatolewa bure na Serikali na pale itakapothibitika kwamba binti yule ameweza kupata ujauzito basi huduma za afya kwa wajawazito ni bure kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007.

Name

Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Primary Question

MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:- Je, Serikali imejipanga vipi kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto?

Supplementary Question 8

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa swali la msingi linazungumzia kuhusu kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto na kwa kuwa takwimu zinaonesha kwamba kila watoto sita wanaozaliwa watoto wanne sio wa baba mhusika. Je, Serikali inaonaje kuhusu udhalilishaji wa akinababa kwa kubambikiziwa watoto ambao siyo wa kwao ki-genetic? (Makofi/Kicheko)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke kumbukumbu sahihi ili hii dhana ili isizidi kuenea. Si kweli kwamba watoto sita katika watoto wetu tuliokuwa nao wote si wa baba ama wazazi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke vizuri jambo hili. Takwimu ile ilikuwa inatokana na wale waliopeleka vipimo vyao kwa ajili ya vinasaba kutambua uhalali wa mzazi. (Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila mpangilio)

Naomba Waheshimiwa Wabunge mnisikilize, nataka tuelewane vizuri. Ni sawasawa unaenda katika wodi ya TB unataka kujua maambukizi ya wagonjwa wa TB katika wodi ya TB. Wale wote waliopeleka sample maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni wale ambao tayari wana wasiwasi kuhusiana na uzazi wa wale watoto na ndiyo maana hicho kiwango kilichopatikana kikawa hicho, lakini siyo kwamba kwa ujumla wetu Tanzania nzima watoto wengi hususan kwa akina baba siyo watoto wao, siyo kweli!
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiweke hiyo taarifa wazi ili sasa Wabunge na especially wanaume tusianze kukimbia majukumu yetu ya msingi. Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.