Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Primary Question

MHE. SEIF K. GULAMALI aliuliza:- Tanzania tuna ushindani mkubwa wa Kampuni za Simu na katika Jimbo la Manonga maeneo kama ya Kata ya Mwashiku, Ngulu, Kitangari, Sungwizi, Mwamala, Uswaya, Tambarale na Igoweko hayana minara ya mawasiliano. Je, ni lini Serikali itazielekeza Kampuni za Simu kusimamia minara yao kwenye maeneo ambayo hayana mtandao wa mawasiliano?

Supplementary Question 1

MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza; nina maswali (a) na (b).
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kuwa kati ya kata 19 zilizoko ndani ya jimbo la Manonga kata tisa hazina mawasiliano, kwa maana ya vijiji vyote vilivyoko ndani ya zile kata tisa, je, Serikali haioni kuwa katika maeneo hayo wananchi hawatendewi haki kwa sababu wanakosa mawasiliano? Na je, Serikali kutokana na majibu yake inatuhakikishiaje kuwa mpaka Novemba itakuwa tayari maeneo hayo yamepata minara ya simu katika maeneo yaliyotajwa?
Mheshimiwa Spika, swali b je Waziri atakuwa tayari tuongozane naye ili awezekwenda kujionea hizo kata ambazo hazina mawasiliano ya simu? Kama yuko tayari ni lini ili aweze kuona adha ambazo wananchi wanazipata? Ahsante.

Name

Eng. Edwin Amandus Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali kwenye jibu la msingi Serikali inakiri kuwa kati ya kata 19, kata 10 zinamawasiliano na kata tisa hazina mawasiliano. Kwetu sisi hayo ni mafanikio makubwa na tutahakikisha kata tisa zilizobaki ambazo ni chini ya asilimia 50 tunazifikishia mawasiliano katika kipindi hiki cha miaka mitano itakapofika mwaka 2020 hilo litakamilika na tutalikamilisha kwa kutumia mkataba tulionao na kampuni ya Viettel kwa kuwa tuna mkataba nao, lakini vilevile Mfuko wetu wa Mawasiliano kwa Wote.
Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge umefika ofisini tumekutana na wataalam, bahati nzuri hivi vyote tuliviorodhesha na sasa unafahamu, labda ni vizuri tu na wananchi wako wakafahamu kwamba kata hizo zote tisa tumeshazichukua na tutazifanyia kazi katika kipindi kifupi kijacho.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kufika katika eneo lake na kuzipitia hizo kata.
Mheshimiwa Spika, kama utakumbuka ndani ya Bunge lako Tukufu alipouliza swali lake la nyongeza nilimjibu kwamba mimi siamini kijiji kama Machinja hakina mawasiliano kwa sababu watu ni wengi sana. na nitumie nafasi hii kuyafahamisha makampuni ya simu tunamaeneo mengi yenye watu wengi sana, mahala ambapo pana biashara kubwa. Maeneo hayo hatuhitaji fedha ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote yaende katika maeneo hayo. Kwa sababu maeneo hayo ni yakibiashara, yana watu wengi na mkipeleka mawasiliano mtapata fedha za kutosha. Its economically viable.
Kwa hiyo karibuni sana Waheshmiwa Wabunge tupeane taarifa maeneo ambayo yana watu wengi sana center kubwa sana makampuni yenyewe yaende tusitumie hela zetu za Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Hela hizi za mfuko wa mawasiliano kwa wote tuzitumie katika maeneo ambayo hayavutii kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, nitakuja katika lengo hilo hilo la kuhamasisha makampuni kwanza yaje, lakini pili tuone UCSAF itafanyaje kazi kama ambavyo tulikuahidi ulipofika ofisini na tukakutana na wataalam. Hongera sana Mheshimiwa kwa kufuatilia suala hili kwa umakini sana.