Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Primary Question

MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:- Ili Mtu au Kampuni iweze kufanya biashara ya Mazao ya Misitu anapaswa kusajiliwa:- (a) Je, ni kwa nini usajili huu hufanywa kila mwaka? (b) Je, Serikali haioni kwa kufanya hivyo kunaongezea walipa kodi mzigo? (c) Je, usajili huu hauwezi kufanywa pale tu mtu au Kampuni inapoanza biashara kwa mara ya kwanza na anapoendelea aweze kuhuisha badala ya kusajiliwa upya kila mwaka.

Supplementary Question 1

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002, ilizuia usafirishaji wa mazao ya misitu ambayo hayajachakatwa ikiwemo asali, mbao na hata wanyamapori. Naomba kuuliza swali langu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya zuio hilo Serikali imeruhusu kusafirisha mbao ya sentimita 15 tu unene na wakati huo wadau na masoko yanahitaji zaidi ya sentimita 15. Je, Serikali iko tayari sasa kuwaruhusu wafanyabiashara ambao wanafanya export ya mbao hizi, wakiwemo wafanyabiashara wa mitiki, pine na mbao za miche ya asili angalau wafikie katika sentimita 20 ili nao wapate tija na kushindana na wafanyabiashara wenzao katika masoko?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi na Wilaya nzima ya Manyoni, imezuia uvunaji wa mbao na mazao ya misitu kwa ujumla, Je, Serikali sasa ipo tayari kushirikiana na Halmashauri yangu mpya ya Itigi uvunaji uendelee, badala ya watu sasa kuiba ili walipe kodi za Serikali na maduhuli na pia kusaidia pato la Halmashauri wakati misitu ipo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ambayo ameitaja Sheria Namba 14 ya mwaka 2002, Serikali iliweka utaratibu kwa uvunaji wa mazao mbalimbali ya misitu kama alivyoyataja na kwa uchache ni pamoja na miti ya mitiki, pamoja na ya pine, napenda kusisitiza kwamba pale ambapo Sheria ipo na ilikwishawekwa na Serikali, ni wajibu wetu kufuata masharti ya Sheria hiyo katika kipindi chote ambacho Sheria hiyo bado imesimama.
Mheshimiwa Naibu Spika, iwapo kuna mawazo mengine mapya ambayo ni mazuri, ya kujenga kwa maslahi ya Taifa, basi ni budi kufuata utaratibu wa kawaida wa kisheria kuweza kurekebisha sheria ili kuweza kunufaika na mawazo mapya kama yapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, uvunaji wa mazao ya misitu katika Jimbo la Manyoni Magharibi na Wilaya Manyoni kwa ujumla ulizuiliwa kwa sababu za msingi za uhifadhi. Pale unapoendelea kuvuna unatakiwa uvune ukizingatia sharti la uvunaji endelevu, kama utaendelea kuvuna bila kuzingatia masharti ya uvunaji endelevu, ukakiuka masharti sustainability maana yake ni kwamba utakosa kila kitu kwa sababu misitu hiyo inaweza kupotea kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunapokea maoni yake na kwamba sasa tutakwenda kufanya utafiti wa kisayansi kwenda kuangalia kama zuio hilo sasa limepitwa na wakati, inawezekana msitu huo sasa umeweza kupata hadhi ambayo inawezekana kabisa tukaendelea kuvuna badala ya kusimamisha kama tulivyosimamisha hapo awali. Tutaongozwa na utafiti wa kisayansi ili tuweze kuona kwamba, sasa tunaweza kuendelea kuvuna.