Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani endelevu wa kudhibiti ongezeko la watu hapa nchini, iendane na uwezo wa Serikali kupeleka huduma muhimu na za msingi kwa watu wake na wananchi kwa ukamilifu?

Supplementary Question 1

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwepo sera ya kudhibiti ongezeko la watu ya mwaka 1992 na kufanyiwa maboresho mwaka 2006, bado kwa maeneo ya vijijini wazazi na familia nyingi wamekuwa wanazaa watoto wengi kwa madai kwamba kila mtoto anakuja na riziki yake. Matokeo yake watoto wanaishi katika hali ya mazingira magumu na wengi wao wanaishia kuwa watoto wa mitaani kwa sababu wanakosa huduma zote muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali hii ambayo ni hali halisi, Serikali sasa iko tayari kutangaza ukomo wa watoto katika familia angalau tano au saba ili watoto wanaozaliwa kila mtoto apate elimu inayotakiwa, apate huduma za afya, apate mambo yote ambayo anastahili katika maisha yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; njia mojawapo inayotumiwa na Serikali kudhibiti ongezeko la watu ni kuwepo kwa uzazi salama. Maeneo ya vijijini bado wanaopata uzazi salama ni wachache kwa sababu vituo vya afya ni vichache, zahanati ni chache hakuna mobile clinic, kwa sababu wengi wao hawapati hii huduma jinsi inavyostahili hali ambayo wanaendelea kuzaa bila kuwepo na mpango. Serikali sasa iko tayari pamoja na juhudi zote ambazo zimeelezwa kwenye jibu la msingi kuhakikisha kwamba kule ambako hakuna zahanati, hakuna vituo vya afya, kuwepo mobile clinic za kutosha na wapelekwe watalaam, pikipiki za kutosha…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio swali, kuhakikisha kwamba elimu ya uzazi salama inawafikia kina mama wote vijijini na mijini? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza kwamba Serikali kutangaza ukomo wa idadi ya watoto, napenda kumwambia Mheshimiwa Sakaya na Bunge lako Tukufu kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba suala hili la ongezeko la idadi ya watu nchini ni suala mtambuka na ni suala la kijamii. Kusema Serikali iweze kutoa tamko la watu kupata idadi ya watoto naamini haitokuwa sahihi kijamii na kulingana na tamaduni za Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili kuhusu kutokuwa na vituo katika baadhi ya vijiji vyetu tunaona jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba vituo hivi vinajengwa katika kila Kata yetu pamoja na zahanati katika kila Kijiji. Pia kuna ongezeko kubwa la mobile clinic katika vijiji vyetu ambayo Serikali imeanza kutekeleza na ni imani yangu akinamama watapata huduma ya uzazi salama kwa wakati muafaka.