Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:- Kituo cha Watoto wenye ulemavu cha Buhangija kimekuwa kikijiendesha kwa kusuasua:- Je, Serikali ipo tayari kupeleka fedha kwa asilimia mia moja katika kituo hiki hasa ikizingatiwa kuwa kinachukua watoto kutoka Kanda yote ya Ziwa?

Supplementary Question 1

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo amejibu lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa kituo hiki cha Buhangija kimekuwa na msongamano kutokana na wimbi kubwa la mauaji ya Albino na kukifanya kituo hiki kuwa na watoto wengi zaidi na hatimaye watoto wale kuweza kuishi pale shuleni. Je, ni lini Serikali itakiangalia kituo hiki na kukipelekea fedha ya kutosha ili kiondokane na tatizo kubwa la chakula linalokuwa linakikumba kituo hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itapeleka Walimu wa kutosha kwa ajili ya watoto wasioona, wasiosikia na wasiosema? Ahsante.

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Azza kwa kazi nzuri anayoifanya na tumekuwa tukishirikiana sana katika kuhudumia watoto katika kituo hicho. Kwa kweli namshukuru sana Mheshimiwa Azza na nadhani wananchi wa Shinyanga wanasikia pongezi hizi za Serikali kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini maswali yaliyoulizwa na Mheshimiwa Azza Hilal ni maswali ya msingi na swali la kwanza angependa kujua ni kwa namna gani sasa Serikali itaendelea kuhudumia vizuri kituo hicho na hasa kuhakikisha wale watoto wanapata chakula kinachotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali la msingi, tulipata shida kubwa sana wakati ule ambapo mauaji ya wenzetu wenye ualbino yalipokuwa yamekithiri katika nchi yetu ya Tanzania, wengi wenye ualbino waliona pale ni mahali pekee na salama kwao, kwa hiyo wengi walikimbilia hapo haikuwa shule tena, ilikuwa ni kituo cha kuwahifadhi wenye ualbino watu wazima, vijana pamoja na hao watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, baada ya Serikali kufanya kazi nzuri ya kudhibiti mauaji hayo, tumeshafanya utaratibu na tumeweza kuwaondoa wale watu wazima na vijana ambao siyo wanafunzi kutoka hiyo idadi ya 407 mpaka idadi hiyo ya 228 na sasa basi huduma hizo nyingine zinapatikana vizuri na sisi kama Serikali tutaendelea kusimamia chakula na mahitaji mengine yapatikane sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kwamba kituo hicho kinapatiwa fedha za kutosha, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu na Mheshimiwa Azza Hillal tumeshaanza mkakati wa kuhakikisha pale panakuwa mahali salama na mahali panapostahili. Kwa kuanzia tumeshapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho na tutaendelea kupeleka mahitaji mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi juzi mmeona Mheshimiwa Waziri Mkuu amepokea vifaa mbalimbali kwa ajili ya mafunzo ya wenye ulamavu kwenye taasisi zetu, kwa hiyo na kituo hicho tutazingatia kukipa huduma zote zinazostahili kwa mujibu wa taratibu za Serikali.