Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER A. MAHAWE (K.n.y. MHE. ESTER M. MMASI) aliuliza:- Serikali imekuwa na juhudi mbalimbali za kuinua kiwango cha ajira zisizo rasmi nchini. Je, nini mpango wa Serikali katika kuwawezesha vijana wahitimu waweze kuingia rasmi kwenye sekta ya kilimo na ufugaji?

Supplementary Question 1

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wahenga wanasema samaki mkunje angali mbichi. Nakumbuka zamani tulikuwa tunajifunza masomo ya kilimo katika shule za msingi na sekondari nchini, lakini kwa bahati mbaya sana masomo hayo yakafutwa. Sasa labda tupate Kauli ya Wizara ya Elimu ni kwa nini masomo haya yalifutwa na tunategemea vijana baada ya kumaliza vyuo vikuu ndio wanaoweza kupata sasa ajira kupitia kilimo na ufugaji wakati hawakuandaliwa tangu mwanzo?
Swali la pili ambalo linasema ni maeneo gani hasa yaliyoandaliwa na yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo kwa ajili ya vijana hawa wanapohitimu masomo yao ya Vyuo Vikuu na kukosa ajira katika maeneo mengine? Ahsante.

Name

Antony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajibu swali la pili, la kwanza atajibu Mheshimiwa Waziri wa Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameuliza kama kuna maeneo ambayo yamekwishakutengwa kwa ajili ya shughuli hizi za vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014 Novemba, Ofisi ya Waziri Mkuu ilifanya kikao na Wakuu wa Mikoa wote wa nchi nzima hapa Dodoma. Katika kikao hicho iliamuliwa kwamba kila Mkoa uende kutenga maeneo maalum ambayo tutayaita Youth Special Economic Zones, ni Ukanda Maalum wa Uchumi kwa ajili ya Vijana, lengo lake ni kuwafanya vijana hawa wahitimu na vijana wengine wote wa Kitanzania ambao wangependa kufanya shughuli ya ujasiriamali, lakini wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maeneo ili kupitia utaratibu huu waweze kupatiwa maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka hivi sasa tayari Mikoa mingi imekwishatenga maeneo haya na zimekwishatengwa tayari ekari 85,000 nchi nzima kwa ajili ya shughuli za vijana.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ningependa kujibu swali la Mheshimiwa Ester Mahawe, kuhusiana na Serikali kufuta masomo ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali haijafuta masomo ya kilimo, masomo ya kilimo bado yanafundishwa shuleni na hata katika matokeo ya wanafunzi wanaoenda Kidato cha Tano ambayo Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ameyatangaza juzi wapo wanafunzi waliochaguliwwa kwenda kusoma combination zenye kilimo. Vilevile Serikali na Chuo Kikuu Maalum cha Kilimo cha Sokoine na Serikali ina mpango wa kuendelea kuimarisha masomo ya kilimo katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na kuongeza udahili katika vyuo vikuu kwa sababu tunatambua kwamba, kilimo ndio uti wa mgongo wa maendeleo ya Taifa hili. (Makofi)

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER A. MAHAWE (K.n.y. MHE. ESTER M. MMASI) aliuliza:- Serikali imekuwa na juhudi mbalimbali za kuinua kiwango cha ajira zisizo rasmi nchini. Je, nini mpango wa Serikali katika kuwawezesha vijana wahitimu waweze kuingia rasmi kwenye sekta ya kilimo na ufugaji?

Supplementary Question 2

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kwa kuwa swali la msingi linazungumzia ajira kwa vijana, kumekuwa na utaratibu wa baadhi ya makampuni kuajiri watu kutoka nje, yakiwemo makampuni ya ulinzi na kuwafanya vijana wa Kitanzania kutengwa kuonekana kwamba, wao hawana uwezo.
Je, Serikali haioni kuendelea kuajiri watu kutoka nje ni kuweka nchi yetu hatarini, badala ya kuajiri vijana wa Kitanzania?

Name

Antony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, imetungwa Sheria ya Uratibu wa Ajira kwa Wageni ambayo na sisi kama Wizara, tunaisimamia. Nataka nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika utekelezaji wa sheria hii tunahakikisha nafasi nyingi sana zinashikwa na wazawa, ili kuweza kulinda ajira za Watanzania. Kama kuna jambo lolote limetokea kinyume chake hapo, basi tutaelekeza Maafisa wetu wa kazi waende kufanya ukaguzi na wale wote ambao wameingia kinyume cha utaratibu waweze kuchukuliwa hatua ili vijana wetu waweze kupata nafasi za ajira.

Name

Susan Anselm Jerome Lyimo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER A. MAHAWE (K.n.y. MHE. ESTER M. MMASI) aliuliza:- Serikali imekuwa na juhudi mbalimbali za kuinua kiwango cha ajira zisizo rasmi nchini. Je, nini mpango wa Serikali katika kuwawezesha vijana wahitimu waweze kuingia rasmi kwenye sekta ya kilimo na ufugaji?

Supplementary Question 3

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba uchumi wa nchi yetu ungekua zaidi kama tungewekeza kwenye kilimo, lakini tunaona kwamba kilimo chetu kinaendelea kuporomoka. Huko nyuma kilikuwa kinaingiza asilimia nne, lakini sasa hivi kimeshuka mpaka asilimia 1.7. Sasa nilikuwa naomba kujua Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba, vijana hawa wanajiajiri kwenye mashamba ili kuweza kukuza uchumi wetu? Kwa sababu vijana wapo wamezagaa, lakini mapori, mashamba yako makubwa, lakini hakuna chochote kinachoendelea. Je, Serikali kupitia ofisi yako ina mkakati gani?

Name

Antony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu tumeandaa mpango mkakati wa Kitaifa, it is a national strategy ya kuwaingiza vijana katika kilimo. Katika mpango huu malengo makubwa ni kuyatumia yale mashamba makubwa ya Serikali ambayo hayatumiki kwa ajili ya shughuli za kilimo kwa vijana.
Kwa hiyo, tunaamini kabisa katika mpango huu kwa muungano huu kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo, tutafanya kazi pamoja ili maeneo haya sasa tuweze kuwapatia vijana wa nchi hii wakafanye shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisema, narudia mara nyingine tena leo ya kwamba moja kati ya kazi ambayo tunaanza nayo mapema kabisa tumeamua katika eneo la Mkulazi na Mbigili pale Morogoro ambako Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF wanakwenda kujenga Kiwanda cha Sukari tutawafanya vijana wa nchi hii kuwa ndio out growers ambao watasaidia kulima miwa kwa ajili ya kukilisha kiwanda. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwa kupitia mkakati huu vijana wengi zaidi watapata ajira na waweze kujiajiri.(Makofi)

Name

Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Primary Question

MHE. ESTER A. MAHAWE (K.n.y. MHE. ESTER M. MMASI) aliuliza:- Serikali imekuwa na juhudi mbalimbali za kuinua kiwango cha ajira zisizo rasmi nchini. Je, nini mpango wa Serikali katika kuwawezesha vijana wahitimu waweze kuingia rasmi kwenye sekta ya kilimo na ufugaji?

Supplementary Question 4

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Asilimia 67 ya Watanzania wako kwenye ajra ya kilimo na kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kuna mikopo inayotolewa na ndani ya Halmashauri tunatenga asilimia tano kwa ajili ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua upande wa Serikali ni lini watabadilisha hiyo sheria ili ukomo wa umri kwa vijana katika kukopa usiwepo kwa sababu, kumekuwa na changamoto, wengine wamefikia miaka 45 miaka 50, lakini bado wanahitaji mikopo, lakini wanakwamishwa na suala la umri. Ni lini Serikali itabadilisha hiyo sheria?

Name

Antony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kuhusu lini tutabadilisha umri, hili ni suala la kisera. Siwezi kulisema hapa moja kwa moja, lakini definition ya kijana si ya Tanzania peke yake ni definition ya kidunia na sisi tunakwenda katika definition ambayo inazungumzwa na ILO, lakini kama kuna mahitaji hayo nafikiri baadae, kupitia sera na mahitaji mbalimbali, jambo hilo linaweza likaangaliwa upya, lakini kwa sasa bado tunabaki kuwa na umri huo kuanzia miaka 15 mpaka 35.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la uwezeshaji; kwenye uwezeshaji ukiacha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao ndio una-limit umri, mifuko mingine bado iko zaidi ya mifuko 19 ya uwezeshaji ambayo yenyewe haiangalii umri. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Mbunge uendelee tu kuwapa elimu wananchi waelewe mifuko mingine ya uwezeshaji ili waweze kuitumia kwa ajili ya kuweza kujiwezesha. (Makofi)