Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:- Ardhi ikipimwa huwa na thamani na hivyo kuwafanya wamiliki kupata mikopo katika taasisi za kifedha na kuwekeza katika uchumi. Katika Jimbo la Tarime Mjini ni Kata mbili tu za Bomani na Sabasaba ndizo ambazo ardhi yake imepimwa kwa asilimia 75 kati ya kata nane zilizopo, hii inatokana na upungufu mkubwa wa wataalam wa kupima ardhi. Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam wa kutosha ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tarime kuweza kupima ardhi kwa kata sita zilizosalia ili wananchi wa Tarime Mjini waweze kunufaika na ardhi yao?

Supplementary Question 1

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nashukuru kwamba, Wizara inatambua kwamba Mji wa Tarime unatakiwa kupimwa, lakini pia inatambua kwamba una upungufu wa watumishi. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maeneo mengi ya Mji wa Tarime yalikwishaandaliwa ramani ya Mipango Miji, lakini mpaka sasa hivi hayajapimwa, na kwa kuwa wananchi wanaendelea kujenga kiholela na kuharibu ramani ambayo tulikwishaandaa hapo awali, ni kwa nini sasa Serikali msiweze kuunda kikosi kazi kwa ajili tu ya kuja kupima maeneo yote ambayo yameshaandaliwa ramani ya mipango miji ili sasa tusiharibu hii ramani ambayo imeshaandaliwa?
Swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Mji wa Tarime haina vifaa vya kuweza kupima ardhi na tumekuwa tukikodi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, na kwa kuwa, Halmashauri ya Mji wa Tarime hatuna fedha za kuweza kununua vifaa hivi ambavyo vinauzwa bei ghali sana, ni kwa nini sasa Serikali isiweze kufadhili ununuzi wa vifaa hivi ili kuweza kupima maeneo mengi zaidi na kuweza kuharakisha umilikishaji wa ardhi kwa wananchi? (Makofi)

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anasema maeneo mengi ya Tarime yalikuwa yamepimwa, yana michoro tayari, lakini upimaji wake pengine haujakamilika na yameanza kuvamiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali hilo naomba nijibu kwamba kwanza niwaombe Halmashauri yenyewe husika kwa sababu ndio kwanza inazidi kukua sasa hivi, kama maeneo yale hayajakamilika katika upimaji niombe Halmashauri iwe makini katika kulinda yale maeneo yasivamiwe, kwa sababu katika maeneo yote yenye michoro wananchi wanapovamia, hapatakuwa na upimaji mpya. Maana yake wakikutwa wamevamia kiwanja kimoja watu wawili/watatu, maana yake pale lazima mmoja itabidi apishe apewe kile kiwanja na mwingine atafutiwe eneo lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanya lile eneo lisiingiliwe na watu wengi zaidi niwaombe sana Halmashauri kwanza wakamilishe ile taratibu kwa sababu ni jukumu pia la Halmashauri, lakini watasaidiwa pia na Ofisi yetu ya Kanda ambayo sasa hivi wamesogezewa, itakuwa iko Simiyu. Kwa hiyo, tukishafanya hivyo tutakuwa tumelinda yale maeneo. Urasimishaji unaofanyika hauwezi kufanyika katika yale maeneo ambayo tayari yalikuwa yamepimwa, unafanyika katika maeneo ambayo yapo katika ule utaratibu upo.
Kwa hiyo, suala la kuwa na vikosi kazi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, kazi hii inafanyika haraka ni jukumu pia la Kanda husika kwa sababu, tunaweza tukatumia Wataalam walioko katika Halmashauri jirani wakiratibiwa na Ofisi ya Kanda, suala hilo linaweza likafanyika na inawezekana kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la vifaa; suala hili nilishalijibu pia katika majibu ya nyuma katika Bunge hili. Niombe sana Wizara haiwezi kununua vifaa vya upimaji katika Halmashauri zote, ni jukumu la kila Halmashauri kuweka bajeti zake, Wizara imejipanga katika Kanda zake na vifaa vile katika Kanda vinaweza kutumika katika Halmashauri yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi vifaa vile vina bei kubwa sana, lakini ninaomba na nimekuwa nikielekeza wale wenzetu walioko kwenye Kanda, kila mmoja ana Halmashauri zake ni kiasi cha kupanga utaratibu mzuri, mkiwa na vikosi kazi ambavyo vinaweza vikasaidia katika kwenda Halmashauri moja baada ya nyingine itaturahisishia katika kupunguza kero ya upimaji.
Kwa hiyo, naomba pamoja na private sector ambao wanatumika, bado Ofisi zetu za Kanda kwa kutumia watumishi katika Halmashauri kwenye Mkoa husika tunaweza tukapunguza tatizo hilo. (Makofi)