Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:- Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo kwa njia ya vocha kwa lengo la kuwasaidia wakulima, lakini utaratibu ukiwanufaisha Mawakala wa Mbolea kuliko wakulima ambao ndio walengwa. Je, Serikali inachukua hatua gani ya kuweza kubadilisha utaratibu huo na kuja na utaratibu mwingine utakaoweza kuwasaidia wakulima?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza naipongeza Serikali kwa kubadilisha utaratibu wa awali kwa sababu utaratibu wa awali wakulima waikuwa hawanufaiki. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa msimu wa mvua katika maeneo mbalimbali hapa nchini unatofautiana, kwa mfano, katika Mkoa wa Kigoma mvua za kupandia ni za mwezi wa Oktoba. Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima mapema zaidi kuliko ilivyo sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, wapo mawakala waliofanya kazi kubwa ya kusambaza mbolea kwa wakulima. Na kati ya mawakala hao wapo waliofanya kazi kwa uadilifu mkubwa na uaminifu, lakini wapo ambao hawakuwa waaminifu na Serikali ilituma watu kwenda kuhakiki madeni kwa mawakala hao nchi nzima.
Je, ni lini Serikali itawalipa mawakala waliofanya kazi kwa uadilifu, ili waweze kulipa madeni waliyokopa katika benki mbalimbali, wakiwemo mawakala wanawake ambao wanateseka sana kudai pesa zao? (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la kuhusu utofauti wa misimu ya mvua na mbolea kuwafikia wakulima kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba Wizara ya Kilimo inatambua kwamba pembejeo ya mbolea ni kati ya virutubisho muhimu sana, ili kumfanya mkulima wa Kitanzania aweze kulima kilimo cha tija. Sasa katika mpango wa Wizara ni kuhakikisha kwamba katika mfumo huu mpya ambao tunakwenda nao wa bulk procurement mbolea hizi ziweze kuwafikia wakulima kwa wakati, ili waweze kutumia kwa ajili ya kilimo chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa sababu ya Maputo Declaration ya mwaka 2003 ambayo katika Ukanda wa Nchi za Kusini mwa Afrika imesema kwamba Tanzania ni kati ya nchi ambazo zinatumia kiwango kidogo cha virutubisho kwa hekta moja ambayo kwa mujibu wa Declaration hii inapaswa kila hekta moja vitumike virutubisho kilo 50 na sisi tupo katika kilo 19. Kwa hiyo, kwa kuona umuhimu huo Serikali sasa itahakikisha kwamba, mbolea hii inawafikia wakulima kwa wakati, ili waweze kulima kilimo cha tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili amezungumza kuhusu uhakiki wa malipo ya mawakala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Waziri wa Kilimo wakati wa bajeti yake ni kweli, wako mawakala ambao walifanya kazi hii kwa uaminifu, lakini ambao bado hawajalipwa malipo yao. Tayari Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshaiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kufanya uhakiki kwa Mikoa yote 26, isipokuwa Dar es Salaam peke yake ili ndani ya mwezi mmoja mawakala hawa ambao walisambaza pembejeo waweze kulipwa pesa zao. (Makofi)

Name

Dr. Immaculate Sware Semesi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:- Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo kwa njia ya vocha kwa lengo la kuwasaidia wakulima, lakini utaratibu ukiwanufaisha Mawakala wa Mbolea kuliko wakulima ambao ndio walengwa. Je, Serikali inachukua hatua gani ya kuweza kubadilisha utaratibu huo na kuja na utaratibu mwingine utakaoweza kuwasaidia wakulima?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa tunaona dhahiri kwamba kilimo kinazidi kurudi nyuma badala ya kusonga mbele, na kwa kuwa tumekuwa sasa wakulima hasa wale wa vijijini wanategemea mbegu za kununua na sio mbegu za asili na mbegu hizi zinaenda sambamba na upatikanaji wa mbolea. Siku hizi kuna mbolea ya kulimia, kuvunia na kadhalika, wakati kilimo cha zamani cha asili tulikuwa tunatumia mfano, mbolea za samadi na mbegu zenye ubora.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kurudi nyuma na kujitathmini kwamba tunakoenda siko, tuangalie zile system za zamani za kilimo ziboreshwe zaidi ili wakulima wapate manufaa ya mazao yao? Ahsante. (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI,VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa ushauri ambao ameutoa na kama Serikali tumeuchukua.
Katika mpango wa Serikali katika huu mfumo mpya unaokuja wa bulk procurement Serikali itaagiza kwa wingi mbolea ya kupandia ambayo ni DIP na mbolea ya kukuzia ambayo ni urea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea nyinginezo kwa maana ya NPK, MOP, SA na Bio fertilizers na folia zile za maji, hizi zitakuja katika utaratibu wa kawaida. Vilevile ndani ya Wizara ya Kilimo yupo Wakala wa Mbegu ambaye kazi yake ni udhibiti wa mbegu bora ambaye ni ASA na yeye tutamtumia ili wakulima wetu wafanye kilimo chenye tija.