Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA IKUPA ALEX aliuliza:- Kumekuwa na ongezeko la ombaomba au utegemezi kwa watu wenye ulemavu nchini:- Je, ni kwa nini Serikali isiwawezeshe kiuchumi watu wenye ulemavu kwa kuwapa upendeleo wa zabuni za kazi mbalimbali, kama vile kuzoa takataka, usafi wa vyoo, ushonaji na kadhalika kwenye Halmashauri?

Supplementary Question 1

MHE. STELLA IKUPA ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza:
(a) Je, ni lini Serikali itaziagiza Halmashauri na Manispaa, kutenga fungu maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu kama ilivyo ile asilimia 10 kwa wanawake na vijana?
(c) Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kufanya zoezi la utambuzi kwa watu wenye ulemavu, aina ya ulemavu walionao, pamoja na hali zao kiuchumi ili zinapotokea fursa iwe rahisi kuwafikia walengwa?

Name

Dr. Abdallah Saleh Possi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kuhusu kutenga asilimia ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Kwanza niseme kabisa natambua utaratibu wa sasa wa kutenga asilimia 10 kwa maendeleo ya wanawake na vijana ulifanywa kutokana na kutambua tatizo la kuachwa nyuma kwa makundi haya muhimu. Falsafa hiyo hiyo inajengeka kwa watu wenye ulemavu. Hivyo basi, Serikali kwa kupitia taratibu zake za kiutawala na kisheria itaanza utaratibu wa kuutekeleza mpango huu pale hali itakaporuhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya mpango huo haujaanza kutekelezwa, nitoe wito kwamba katika asilimia hii 10 ya vijana na wanawake, basi kipaumbele maalum kitolewe kwa watu wenye ulemavu kwa mujibu wa Sheria Namba T isa (9) ya Mwaka 2010 kama nilivyoelezea kwa mujibu wa Kifungu cha tatu (3), pia kwa mujibu wa Kifungu namba 34(2), lakini pia kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inasema maana ya kubagua haitoizuia Serikali kuchukua hatua za makusudi ili kutatua matatizo mahsusi katika jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni wajibu wa Taasisi za Serikali kupitia Katiba na kupitia vifungu hivyo nilivyovitaja kutoa kipaumbele maalum kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili, kuhusu zoezi la utambuzi. Hapa kuna mawili; kwanza, tayari nilishazindua kazidata yenye taarifa za watu wenye ulemavu. Kazidata hiyo itatumika kufanya mambo mbalimbali ikiwemo utambuzi wa watu wenye ulemavu na mahitaji yao na inatarajiwa pale fedha itakapopatikana na hali ya teknolojia itakapoendelea, kazidata hii iunganishwe pia na kazidata nyingine zinazohusiana na taarifa ya hali ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niongeze kitu kimoja, kwamba tayari Serikali imeshatoa maagizo ya kuundwa kwa Kamati za Watu Wenye Ulemavu katika Halmashauri mbalimbali. Kamati hizi ndizo zitafanya kazi nzuri ya kuzishauri Halmashauri kuhusiana na mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu. Hivyo, kupitia Bunge hili nisisitize kutekelezwa kwa agizo hilo la Serikali la kuundwa kwa Kamati Maalum za Watu Wenye Ulemavu katika ngazi mbalimbali za Serikali za Mitaa.