Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Primary Question

MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:- Maeneo ya Kibiti, Bungu, Jaribu Mpakani na Nyamisati katika Jimbo la Kibiti yanakuwa kwa haraka sana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu. (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupanga mipango miji? (b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mitandao na kuchonga barabara za mitaa?

Supplementary Question 1

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; Serikali ina mpango gani wa kuajiri watumishi wa sekta ya ardhi ikiwemo Kibiti ambako kuna watumishi wachache?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia vifaa vya upimaji katika Wilaya mpya ya Kibiti kwa sababu mapato yake ya ndani yamekuwa madogo sana?

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchache wa watumishi wa ardhi, naomba nimsihi Mheshimiwa Mbunge na ninaamini kabisa ana nia njema na amekuwa akipigania wananchi wa jimbo lake; katika ikama ambayo itakuwa imewekwa na halmashauri yake ni vizuri wakaonesha uhitaji wake na halafu utaratibu wa kuwaajiri watumishi wa ardhi kama ambavyo ilikuwa kwa watumishi wengine ikafuatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, uwezo wa Halmashauri ni mdogo kwa hiyo wanaomba vifaa vya kupimia ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi ambayo ndiyo Wizara yenye dhamana kwa kujua iko haja kubwa ya kuhakikisha kwamba ardhi inapimwa katika maeneo yote na Wilaya zote, juzi juzi Serikali kwa kupitia Wizara ya Ardhi wameweka katika mpango wa kuhakikisha kwamba Wilaya zote zinanunuliwa vipima ardhi ili iweze kurahisisha suala hili. Naamini na wao watakuwa wanufaika.

Name

Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:- Maeneo ya Kibiti, Bungu, Jaribu Mpakani na Nyamisati katika Jimbo la Kibiti yanakuwa kwa haraka sana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu. (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupanga mipango miji? (b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mitandao na kuchonga barabara za mitaa?

Supplementary Question 2

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa tatizo lililopo katika jimbo la Kibiti linafanana na baadhi ya maeneo katika mji wa Dodoma, kwamba baadhi ya mitaa mfano Nkuhungu, Ilazo, Makole barabara zake za mitaa zipo katika hali duni sana. Je, Serikali itarekebisha lini barabara hizi ukizingatia kwamba sasa hivi Dodoma ni Makao Makuu? Ahsante.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu wazi hoja anayozungumza Mheshimiwa Fatma Toufiq kwamba ni kweli ni hoja halisia. Hii ni kwa sababu mji wetu wa Dodoma sasa hivi kwa maamuzi sahihi yaliyofanywa Serikali ni Makao Makuu yetu. Hata hivyo kupitia miradi yetu ambayo tunaendelea nayo hapa Dodoma, sawasawa na miradi ambayo tunaendelea nayo katika miji saba katika ile Strategic City Project; kazi hii inaendelea awamu kwa awamu. Wabunge nadhani mnakuwa ni mashahidi. Wabunge waliofika mwaka 2010 hapa Dodoma wakifanya ulinganifu na hali ilivyo hivi sasa ni tofauti sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tutaendelea kujenga miundombinu hii. Sasa hivi kuna ring road karibuni zitakuwa tatu. Kuna hii ambayo hata ukifika kule inakatisha, vilevile tuna barabara zetu za mitaa na wataalam wetu wanaendelea na kazi hiyo. Lengo letu ni kwamba tukifika mwaka 2020 Jiji la Dodoma litakuwa ni tofauti sana kwa sababu mpango wetu huo ambao unaenda mpaka mwaka 2020 utahakikisha mji wa Dodoma wote mitaa yake yote itakuwa na kiwango cha barabara za lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo si lami peke yake isipokuwa tutapeleka na mataa pamoja na mifereji yote ya kuondoa maji kuhakikisha jiji hili linakuwa jiji la mfano ambao ndio mpango hasa wa Serikali yetu ilivyoamua.